Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la kujadili nishati safi ya kupikia majumbani iliyoanza jijini Dar es Salaam leo November 01, 2022 |
Na Urban Epimark, DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa wakuu wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam pamoja na Mamlaka ya Maji Safi Dar es Salaam yaani DAWASA kuhakikisha vitalu vyote vya kilimo cha umwagiliaji (Irrigation blocks) vinaondolewa kuanzia leo November 01, 2022 kwenye maeneo ya mto Ruvu ili kunusuru upatikanaji wa kiwango cha maji katika jiji la Dar es Salaam.
Halikadhalika Rais Samia ameagiza serikali kuunda kikosi kazi cha kuchakata sera mpya ya upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia itakayokuwa chini ya uratibu wa ofisi ya Waziri Mkuu, itakayoshirikisha wajumbe kutoka wizara ya nishati, wizara ya maendeleo ya jamii, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo hapa nchini.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kongamano la kitaifa la siku mbili la kujadili upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia majumbani iliyoandaliwa na wizara ya nishati iliyoanza leo kwa siku ya kwanza katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwl Julius Nyerere (JNICC).
"Katika suala la mgao wa maji katika jiji la Dar es Salaam ni matokeo ya usimamizi mbovu wa rasilimali ya maji pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Katika maeneo yanayo uzunguka mto Ruvu, zipo blocks nyingi za kilimo cha umwagiliaji ambazo zinatumia maji mengi na kusababisha upungufu mkubwa wa maji jijini Dar es Salaam.
Natoa maagizo kwa wakuu wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam pamoja na DAWASA mkitoka hapa muende mkaziondoe blocks zote zinazotumia maji eneo la mto Ruvu. Sijui mtatumia Helikopta kuzitambua au sijui mtafanyaje ila ninataka zote ziondoke ili maji kidogo yaliyopo yaweze kupatikana jijini Dar es Salaam" ameagiza Rais Samia.
Kuhusu upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia, Rais Samia ameipongeza wizara ya nishati nchini kwa kuweza kubuni kufanyika kongomano muhimu la kujadili upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ili kunusuru afya za akina mama wanapopika majumbani na pia kunusuru mazingira kwa kukata miti.
Pia ameipongeza kampuni ya Taifa Gas kwa mchango wake mkubwa wa kutoa pesa kiasi cha shilingi milioni 300 kila mwaka kwenda kwa wakala wa misitu nchini (TFS) ili kusaidia kustawisha misitu, lakini akaishauri Taifa Gas kuongeza kidogo mchango huo ili kwa kusaidiana na mfuko maalum utakao tengwa na serikali kwenye bajeti ijayo kuanzia mwakani 2023/2024, uweze kukidhi mahitaji ya kusimamia sera mpya ya nishati ya kupikia itakayo undwa hapa nchini.
Nae Prof. Anah Tibaijuka ambae ni msomi mbobezi katika sekta ya taaluma ya mazingira akiwa mkufunzi vyuo vikuu pamoja na kiongozi serikalini na mtendaji katika mashirika ya umoja wa mataifa ameiambia wizara ya nishati kwamba,
"Mkwamo wa jamii kushindwa kutumia nishati safi ya gesi ya kupikia ni kutokana na serikali kushindwa kudhibiti ongezeko la bei ya ununuzi wa nishati hiyo ya gesi ambapo amesema miaka 5 iliyopita ilikuwa ikiuzwa kwa mtungi shilingi elfu 18 na kupanda hadi sasa shilingi elfu 24, mbali na gharama za mwanzo za kununua mtungi huo ambazo ni wastani wa shilingi elfu 60".
Prof. Tibaijuka ameitaka serikali kupitia kongamano hilo itoke na mkakati wa kunusuru afya za akina mama kutokana na athari za moshi wa kuni na mkaa na pia uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ili kupata nishati hiyo.
Kongamano hilo litaendelea tena leo mchana na pia kwa siku ya pili kesho November 02, 2022 kwa kujadili mada mbalimbali zitakazo saidia kupata sera ya nishati safi na salama ya kupikia majumbani ambapo baada ya miaka 10 ijayo, jamii ya Tanzania iwe imeshafikia asilimia 80 hadi 90 ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia.
Mwisho.
0 Comments