Kamnda wa jeshi la polisi Mkoa wa Geita ACP Safia Jongo |
Na Mussa Mathias, Geita
Jeshi la polisi mkoani Geita limefanikiwa kukamata bunduki moja aina ya AK 47 inayodaiwa kutumika kumtishia mfanyabiashara mmoja Tegemeo Rashidi (38) Mkazi wa kijiji cha Ihanga kata ya Buziku Wilayani Chato Mkoani hapa kabla ya kuuawa kwake kwa kukatwa na panga na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi .
Kamnda wa jeshi la polisi Mkoa wa Geita ACP Safia Jongo akizungumza na Waandishi wa Habari juzi amesema kuwa mfanyabishara huyo aliuawa kwa kukatwa panga sehemu za mwili wake kichwani na shingoni baada ya kumfunga kwenye pikipiki aliyokuwa akiendesha.
Kamanda huyo alisema kuwa baada kupata taarifa ya mauaji ya mfanyabiashara huyo walianza msako mkali na kufanikiwa kuikamata silaha hiyo ambayo ilikuwa imefichwa kwenye shamba la mahindi .
Kamanda Jongo aliongeza kuwa katika tukio hilo jeshi linawashikilia watuhumiwa wanne mmoja akiwa raia wa Burundi anaedaiwa kuja na silaha hiyo nchini .
Kamanda huyo alisema kuwa jeshi hilo lina washikililia Wahamiaji haramu 48 na watuhumiwa wengine 15 wa mazao ya Misitu katika operesheni maalumu iliyofanyika kwa wiki moja .
Kamanda Jongo alifafanua kuwa katika kipindi cha kuanzia Septemba mosi hadi Oktoba 31 mwaka huu katika zoezi la kusalimisha silaha, mkoa wa Geita umefanikiwa kukamata siraha zilizosalimishwa ikiwemo magobole 18 yaliyosalimishwa kwa hiari lakini ambapo magobole 16 na wamiliki wa magobole hayo walikamatwa baada ya kushindwa kusalimisha kwa hiari kwa kipindi kilicho kuwa kimetolewa na jeshi la polisi nchini .
Pia alisema kuwa katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata gunia 7 za madawa ya kulevya aina ya bangi katika operesheni iliyofanyika ndani ya kipindi kifupi pamoja na vitu mbalimbali ikiwemo Radio ,Televisheni,Simu ,Baiskeli ,Pikipiki, Jiko la Gesi la kupikia pamoja na Nguo.
Jeshi la polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na majeshi ya ulinzi na usalama ili kufichua vitendo vya uharifu vinavyofanyika kwenye maeneo yao. .
Mwisho
0 Comments