TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

KITUO CHA AFYA KATORO NA CHANGAMOTO YA UHABA WA VITANDA WODI YA WAZAZI

Na Salum Maige,Geita.

Kituo cha Afya Katoro kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Geita,Mkoani Geita kinakabiliwa na uhaba wa Vitanda kwa akina mama wazazi wanaofika kujifungua hali inayosababisha wazazi kulala wawili na watoto wao kwenye Kitanda kimoja.

Hali hiyo inatokana na Kituo hicho kuhudumia idadi kubwa ya wananchi wakiwemo wanaotoka katika maeneo ya wilaya jirani zikiwemo za Mbogwe,Bukombe na  Chato ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu zaidi ya akina mama 1,000 hujifungua kwenye kituo hicho.

Uhaba huo unatajwa kuhatarisha Afya za watoto wachanga wanaozaliwa kutokana na kuwepo kwa uhaba wa vitanda kwenye wodi ya wazazi hivyo hulazimika wakati mwingine kulala wazazi wawili na watoto wao kwenye kitanda kimoja.

Kutokana na changamoto hiyo,Halmashauri ya Geita imelazimika kutoa vitanda 20 na godoro zake pamoja na shuka ikiwa ni hatua za kupunguza changamoto hiyo ambayo imekuwa ikiwaathiri wazazi na watoto wanaozaliwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita John Wanga amesema kuwa,halmashauri imetoa Vifaa hivyo ikiwa ni hatua ya kuondoa au kupunguza tatizo hilo la uhaba wa vitanda linalokikabili kituo hicho.

Ameongeza kuwa,Kituo hicho huhudumia wazazi 30 hadi 40 kwa siku na kwamba Halmashauri iliagiza Vitanda 50 kwa ajili ya kituo hicho lakini vitanda vilivyopokelewa ni vitanda 20 vyenye thamani ya shilingi Milioni 14.

“Mpango wa Kununua Vitanda hivyo ulikuwepo kwa kuleta vitanda 50 lakini tumeanza na hivi vitanda 20 magodoro na mashuka yake wakati tukisubiri vitanda vingine”anasema Mkurugenzi.

Vitanda Wodini.

Mkurugenzi alibainisha kuwa,serikali inao mpango wa kukipandisha hadhi kituo hicho kuwa Hospitali ya wilaya hatua ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto hiyo ya akina mama kulala wawili kwenye Kitanda kimoja na watoto wao.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na Mwandishi wa Habari hizi wamesema tatizo hilo ni kubwa na kwamba linawaathiri na watoto wao kwani mzazi anapojifungua anahitaji kuwa nafasi nzuri ya kupumzika na mtoto wake.

“Tunaomba serikali ilitazame hili tatizo sisi wazazi tunateseka na tunahangaika na hali hii,serikali ilete vitanda ili wazazi tuwe namazingira salama ya kupumzikia mara baada ya kujifungua”anasema Regina Paul.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Katoro Dk.Zakayo Sungura amepongeza hatua ya Mkurugenzi kukabidhi vitanda hivyo huku akithibitisha kuwepo kwa tatizo la wazazi kulala wawili kwenye kitanda kimoja na watoto wao.

Amesema,kwa Miezi Mitatu mfululizo kituo hicho kimekuwa kikipokea wazazi wanaokwenda kujifungua 900  hadi 1,000 ingawa hali hiyo amesema siyo ya kudumu isipokuwa imetokea katika kipindi cha miezi hii mitatu.

“Ni kweli hili tatizo lipo kwa muda mrefu hii ni kutokana na wingi wa watu wanaofika hapa..wengine wanatoka Buseresere Chato.Hivyo wastani kwa miezi mitatu ya nyuma tumekuwa na wastani wa kupokea wazazi 600 hadi 800 lakini baadaye hii miezi mitatu tumepokea wazazi 900 hadi 1,000”anasema Dk. Sungura.

Wazazi wakiwa Wodini baada ya Kujifungua.

Dk.Sungura anasema,Kituo hicho awali kilikuwa na Vitanda 66 na hivyo baada ya kukabidhiwa Vitanda hivyo idadi imeongezeka na kufikia vitanda 86 na kwamba vitanda hivyo vimepunguza kwa kiasi fulani tatizo hilo.

Kwa wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Modest Buchard akizungumzia tatizo hilo amebainisha kuwa linasababishwa na wananchi wengi wanaotoka wilaya za Jirani ikiwemo Chato kufuata huduma ya matibabu kwenye kituo hicho hali inayochangia msongamano wa wazazi na wagonjwa wengine.

Changamoto hiyo inakuja wakati serikali kwa kushirikiana na wadau wa Afya yakiwemo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT – MMMAM).

Progaramu hiyo ni huduma shirikishi ambayo inaangalia maeneo ya afya bora, lishe kamili, ulinzi na usalama, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto tangu akiwa tumboni mpaka anapofikisha miaka minane.

Hivyo hatua ya Halmashauri ya wilaya ya Geita kuona tatizo hilo na kuanza kulifanyia kazi kwa kutoa Vitanda hivyo ni moja ya utekelezaji wa malengo ya Programu hiyo iliyozinduliwa disemba mwaka jana mjini Dodoma.

Kimsingi PJT-MMMAM imeyalenga zaidi maisha ya mtoto aliye na umri sifuri yaani tokea siku mimba inatungwa hadi atakapofikisha miaka minane. Kipindi kinachotajwa kuwa muhimu katika makuzi sahihi ya mtoto kwa kuwa ndicho kipindi pia muhimu katika ubongo wake.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments