TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MAOFISA WATENDAJI KATA WAPEWA MAJUKUMU KUPAMBANA NA UDUMAVU KWA WATOTO

Mkuu wa wilaya ya Chato Martha Mkupasi akitoa maelekezo kwa Maofisa watendaji wa Kata kwenda kusimamia mpango wa serikali wa Kupambana na Utapiamlo na Udumavu kwa watoto baada ya kusaini Mkataba wa Lishe.

Salum Maige,Chato.

Maafisa Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya wilaya ya Chato Mkoani Geita wamepewa jukumu la kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutokomeza janga la Utapiamlo na Udumavu kwenye Maeneo yao baada ya kusainisha Mikataba ya Lishe.

Wilaya ya Chato inazo kata 23 ambapo watendaji wake wamehusika katika kuingia mkataba na Halmashauri hiyo wa Kutokomeza Tatizo la Utapiamlo na Udumavu,tatizo linalotajwa linatokana na kundi hilo la watoto kukosa Lishe bora.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mandia Kihio amesema kuwa,mpango huo wanakwenda kuupa msukumo kuanzia kwa watoto wa madarasa ya awali,shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha watoto wanapata chakula cha kutosha wakiwa shuleni na kwenye makazi yao.

Kihio amefafanua kuwa,kwenye Halmashauri ya wilaya ya Chato inataka kutokomeza  utapiamlo na Udumavu na kwamba mpango uliopo ni kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni na nyumbani wanakoishi.

Vile vile tutahamasisha jamii kuhakikisha wazazi na walezi huko majumbani wanawapatia watoto chakula cha kutosha ili kutomomeza tatizo la utapiamlo na Udumavu kwa watoto..kwani kundi hili likikosa chakula cha kutosha tutaathiri Taifa la kesho”anasema Kihio.

Kundi linalotajwa kuathirika na Utapiamlo na Udumavu ni kundi la watoto chini ya miaka mitano kutokana na kushindwa kupata chakula kwa wakati na wazazi kutolipa kipaumbele suala hilo.

Ikumbukwe kuwa awali Utiaji saini wa Mikataba ya Lishe kwa watendaji wa serikali  Ulianzia kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan kwa wakuu wa Mikoa nchini Kote ambao imefika hatua ya ngazi ya Kata kwa maofisa watendaji.

Watendaji wa Kata 23 Katika wilaya ya Chato wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Martha Mkupasi wakati akiwapa maelekezo ya kwenda kusimamia Lishe kwenye Maeneo yao Kabla ya Kusaini Mkataba wa Lishe.

Utiaji Saini wa Mikataba hiyo ulishuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Chato Marthea Mkupasi ambapo amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa kila mmoja aliyeingia katika makubaliano ya mkataba huo ili kwenda kuwalinda watoto dhidi ya janga la Utapiamlo na Udumavu.

Mkupasi amewataka maofisa hao walioingia kwenye Mkataba huo kwenda kutekeleza kwa Vitendo Mikataba hiyo ya Lishe ili kufikia malengo ya serikali ya kuthibiti tatizo la utapiamlo na Udumavu kwa kundi la watoto.

“Hakuna kulegalega,watoto wale ndo Taifa la kesho,Mtoto akidumaa hawezi kufanya kazi baadae na hata uwezo wake atakapoanza shule utakuwa mdogo sana,hawezi kuwa kiongozi ama mtumishi lakini tukisimamia imara suala hili tutakuwa na watoto imara” anasema Mkupasi na Kuongeza kuwa.

“Ni imani yangu kwamba kizazi chetu kitakuwa bora watafanya vizuri madarasani lakini pia watakuwa ni viongozi bora kaika maslahi mapana ya Taifa letu”

Kwa Mujibu wa Afisa Lishe Mkoani Geita Riziki Mbilinyi ni kwamba Mwaka 2021/22 takribani Halmashauri nne za Mkoa huo ikiwemo Halmashauri ya wilaya ya Chato hazikupanga bajeti kwa ajili ya watoto chini ya miaka mitano ambayo kila mtoto ni sh.1,000.

Akizungumzia tatizo la Utapiamlo katika Mkoa wa Geita Mbilinyi kwenye Utiaji wa Mkataba wa Lishe anasema kwa mwaka jana 2021/2022 takribani halmashauri nne za mkoa wa Geita hazikupanga bajeti kwa ajili ya watoto chini ya miaka mitano, ambayo ni Sh 1,000 kwa kila mtoto.

Mkuu wa wilaya ya Chato Mkoani Geita Martha Mkupasi akimsainisha Mkataba wa Lishe Mmoja wa Maofisa watendaji wa Kata wilayani humo wakati wa kusaini Mkataba wa Lishe kwa watendaji wa kata zote 23.

Katika mkakati wa mkoa wa kukabiliana na Udumavu idara ya lishe inaendelea kuangalia viashiria vya tatizo la lishe na kupima kila robo ya mwaka katika ngazi ya halmashauri na mkoa kupitia vikao vya tathimini.

Hivi karibu akitoa taarifa ya Lishe ya Mkoa Mbilinyi amenukuliwa akisema Kigezo kilichofanya mkoa huo kushindwa kufikia malengo ni fedha, licha ya vigezo vingine kufanikiwa kwa asilimia 80 lakini kwenye kigezo cha fedha ukifikiwa kwa asilimia 50 tu.

Baadhi ya wananchi wilayani Chato wamesema mpango wa serikali ni mzuri lakini unakabiliwa na tatizo la hali ngumu ya uchumu ikiwani pamoja na uzalishaji duni wa chakula unaotokana na ukame unaokabili baadhi ya maeneo.

Evarist Manyama baba wa watoto watatu anayeishi kijiji cha Muganza anasema serikali imekuja na mpambo mzuri lakini unaweza kuathiriwa na ukame unaotokana na kusekana kwa mvua pamoja na kupanda kwa gharama za maisha.

“Ni kweli tatizo hili la utapiamlo lipo kwa baadhi ya familia na linatokana tu na ugumu wa maisha baadhi ya familia kutelekezwa na migogoro ya familia ambapo baadhi ya watoto wanakuwa hawana uhakika wa Chakula “anasema Janeth Mafulu.

Maofisa watendaji hao mara baada ya kusaini mkataba huo wameiahidi serikali ya wilaya hiyo kwamba wataenda kutumia nafasi walizonazo kuhakikisha mpango huo wa serikali wa kutokomeza tatizo la Utapiamlo na Udumavu unafanikiwa.

Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Chato Mandia Kihio na Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Chato Martha Mkupasi akisoma maelezo yaliyoko kwenye Mkataba wa Lishe waliosainisha maofisa watendaji zote 23 za wilaya hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa,Mkoa wa Geita hali ya Lishe si ya kuridhisha kutokana na kuwepo kwa asilimia 38.9 ya Tatizo la udumavu licha ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula cha kutosha  nchini.

Kiwango hicho cha Udumavu ni sawa na takribani ya watoto laki moja wanakabiliwa na Udumavu kwa kukosa lishe bora inayochangiwa na baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuwajibika kuzingatia lishe kwa watoto wao.

Watoto katika umri wa 0-8 wana mahitaji makubwa ya virutubishi kutokana na kwamba wapo katika kipindi cha ukuaji wa haraka na ni kipindi ambacho wanahitaji uangalizi mkubwa katika makuzi yao likiwemo suala la kuwapatia mlo kamili wa chakula ili kukidhi mahitaji ya ukuaji wa miili yao.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments