Ndg Wanseho Siwale, Mgombea mwanamke wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM (M) Geita kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2027. |
Na Urban Epimark, GEITA.
Hivi karibuni mwishoni mwa juma lililopita, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ulioketi jijini Dodoma ulipitisha majina ya wagombea wa nafasi za uongozi wa CCM ngazi ya mkoa pamoja na jumuiya zake tatu za wanawake, vijana na wazazi.
Katika mkoa wa Geita majina yaliyo wasilishwa Halmashauri Kuu yalikuwa manne likiwemo la mwanamke mmoja na yote yalipitishwa na kurejeshwa tayari kwa uchaguzi mkuu utakao fanyika jumapuli ijayo November 21, 2022.
JE, MWANAMKE HUYO ALIYE PITISHWA NI NANI?
Ndg Wenseho Siwale mkazi wa Mtaa wa Mwatolole, kata ya Buhalahala katika Halmashauri ya Mji wa Geita ndie pekee mwanamke aliye pitishwa katika nafasi hiyo.
Ndg Wensio Siwale mzaliwa wa wilaya ya Mbozi, katika mkoa wa Songwe ambae ni mama wa familia yenye mme na watoto, anayo shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Mwanza (SAUT) aliye hitimu mwaka 2012.
Kabla ya kujiunga SAUT, Ndg Wenseho Siwale alisoma elimu yake ya Sekondari na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 2004 katika shule ya sekondari Mbozi, katika mkoa wa Mbeya lakini kwa sasa ni Songwe.
Baadae aliendelea na masomo ya kidato cha 5 & 6 katika shule sekondari ya wazazi ya Mbalizi, Mbeya na kuhitimu vizuri.
Katika maisha yake yote ya kuwa mwanafunzi akiwa Sekondari na Chuo Kikuu alikuwa kiongozi wa wanafunzi. Katika ya Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Mbalizi alikuwa ndie Dada Mkuu wa shule (Head Girl).
HISTORIA YAKE KATIKA UTUMISHI WA CHAMA.
Histori yake katika utumishi wa chama, Ndg Wenseho Siwale alianza akiwa bado binti mdogo alipokuwa akisoma sekondari wilayani Mbozi katika kata ya Mlowo ambapo alianza kwa nafasi ya Vijana wa Itifaki katika kata hiyo ya Mlowo, wilayani Mbalizi katika mkoa wa Mbeya.
Baadae alionekana ni mbunifu na mwenye ushawishi mkubwa kwa makundi mengine ya chama na jamii kwa ujumla, hivyo chama katika kata hiyo ya Mlowo ikampendekeza kuwa Katibu Mwenezi wake.
MAISHA MAPYA BAADA YA KUHITIMU SHAHADA YAKE SAUT NA KUJA MKOANI GEITA.
Ndg Wenseho Siwale alihitimu masomo yake ya Shahada ya Sheria pale SAUT Mwanza mwaka 2012 na mwaka uliofuata 2013 alikuja mkoani Geita na kujishughulisha na kazi mbalimbali zikiwemo ujasiriamali na pia kuunganisha vikundi vya wanawake na vijana katika kushiriki shughuli za kijamii.
Kipindi hicho pia, Ndg Wenseho Siwale alipata mwenza wake na kufunga nae ndoa na kwa sasa anae mme na watoto yaani ni mama wa familia kwa ujumla.
Akiwa katika harakati za maisha katika Mtaa wa Mwatolole, alianzisha kikundi cha "Mama Chapa Kazi" mwaka huo wa 2013 kilichokuwa na lengo la kuwaunganisha wanawake kuunda vikundi ili kuzikabili changamoto zao kwa pamoja.
Mwaka 2014, Ndg Wensio Siwale alirudi tena chuoni lakini kwa kipindi hiki alijiunga na Chuo cha Taaluma ya Sheria cha Lushoto, yaani Law School of Tanzania ili kujinoa zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
KUANZISHWA KWA NGO YA MAMA NA MAZINGIRA ORGANAZATION (MAMAO)
Baada ya kutoka Shule ya Sheria yaani Law School of Tanzania, Ndg Wenseho Siwale alibaini changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira katika mji wa Geita na viunga vyake ambapo wanawake ndio wahanga wakubwa.
Hii ni pamoja na ukataji miti hovyo katika kutafuta nishati ya kuni za kupikia, kuchafua na kuhatarisha vyanzo vya maji na pia utupaji taka ovyo kunako chafua mazingira na kusababisha milipuko ya magonjwa ya kuhara na kutapika ambayo pia, athari zake kubwa zina mkuta mwanamke wa kawaida.
Kuona haya yote, alianzisha Taasisi isiyokuwa ya kiserikali mwaka 2016 kama kikundi kidogo cha wanawake na mazingira (CBO) ambacho yeye na wanawake wenzake waliendelea nacho hivyo hadi mapema mwaka huu kilipo sajiliwa rasmi kama NGO yenye jina la "Mama na Mazingira Organazation, kifupi MAMAO.
Ndg Wenseho Siwale akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa MAMAO anahimiza muda wote wanawake kutunza mazingira na kuacha kuyachafua na kukata miti ovyo pamoja na kuharibu vyanzo vya maji.
Halikadhalika, Ndg Wenseho Siwale amejiunga na Wanawake wenzake wa Mjini Geita akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita (sasa Dodoma) Mhe Rosemary Senyamule kuunda kikundi cha "Mama Samia na Mazingira" ambacho mbali na kutetea utunzaji mazingira na kupinga ukatili wa kijinsia, kina himiza pia hamasa kwa jamii katika kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.
NDG WENSEHO SIWALE NA UJASIRI WA KUGOMBEA UENYEKITI WA CCM (M) GEITA.
Yeye mwenyewe anakiri wazi wazi kwamba, Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambae ndie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ndio "Role Modal" wake ambae amemtia ndimu (hamasa) ya kugombea uongozi ngazi hii ya juu ya mkoa wa Geita.
Lakini pia anaongeza kwa kusema kwamba, ujasiri mwingine unatoka ndani ya dhamira ya moyo wake tangu akiwa mdogo shuleni, chuoni na sasa katika jamii kama mama wa familia kwamba, mambo yote yanawezekana kwa kumtegemea Mungu mwenywe na kwa kutokata tamaa unapo kutana na magumu.
Ana amini jinsi Rais Samia alivyo sasa katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na anaongoza vyema watanzania tena kwa mafanikio makubwa kwa kuwaunganisha wana CCM wote kuwa kitu kimoja na pia ameweza kuwaunganisha watanzania wote na vyama vyao vya kisiasa na pia kuweza kukaa pamoja na kusikilizana ingali yeye ni mwanamke na mama wa familia, kwa nini yeye Ndg Wenseho Siwale asiweze?
DHAMIRA YA KUGOMBEA NAFASI YA UONGOZI KWA HADHI YA MWENYEKITI WA CCM (M) GEITA.
Ndg Wenseho Siwale anasema, yeye kama kijana mwenye mtizamo mpya katika kuijenga jamii, anaona ipo haja ya yeye kuongoza mapambano ya kuikomboa jamii kwa kushika usukani wa chama mkoa wa Geita na kusonga mbele.
Anaeleza zaidi kwamba, jamii ya sasa inayojengwa na kizazi kipya cha vijana na wanawake ambao pia wengi ni vijana, kinakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira, kukosa ajira, na wengi kuanza kupuuza umuhimu wa kushiriki katika mambo ya siasa ambapo huko ndiko kwenye chimbuko la mawazo mapya ya kuijenga jamii kisha serikali ndio inayo yatekeleza.
Kwa suala la kutunza mazingira, yeye kama kijana lakini pia ni mama wa familia, anadhamiria kulifanya liwe agenda kubwa mno katika mkoa wetu wa Geita.
Kuhimiza kupanda miti kote maeneo ya mjini na vijijini. Kutunza vyanzo vya maji na kuimarisha misitu ya asili ili familia na jamii ziweze kupata maji ya kutosha pamoja na mvua za msimu.
Halikadhalika katika mji wa Geita, jamii bado haijaeleweshwa vya kutosha kuhusu kutupa taka ovyo, kuharibu uoto wa asili ikiwemo majani ya ukoka yanayo zuia mmomonyoko wa ardhi, kujisaidia ovyo haja ndogo maeneo ya uchochoroni ambapo husababisha kusambaa kwa harufu kali na pia kueneza magonjwa ya njia ya mkojo ikiwemo UTI kwa uchafu wa mkojo kusambaa ovyo katika mazingira yetu.
Kuhusu tatizo la Ajira kwa vijana, wanawake na hata akina baba, Ndg Wenseho Siwale anakusudia kuhimiza mpango mzuri wa ujasiriamali na uwezeshwaji mitaji na hata kupata maeneo ya kufanyia biashara katika maeneo yao.
Kuhusu vijana kutoshiriki vya kutosha katika mambo ya siasa kwa kizazi hiki kipya, Ndg Wenseho Siwale anasema,
"Vijana wengi wanamezwa na mifumo ya sasa ya mitandao ya kijamii na hivyo kutoona umuhinu wa kushiriki siasa, hii ni hatari. Siasa ndipo ubunifu ulipo. Mawazo yote ya maendeleo yanaanzia kwenye siasa, hivyo nimeliona hili na nina tamani nilihimize vizuri zaidi nikiwa Mwenyekiti wa chama wa mkoa wetu wa Geita ili niongoze vizuri viongozi wenzangu kuleta mtizamo mpya utakao ondoa makundi kati ya wenye nacho na wasio kuwa nacho na kujenga usawa" ameeleza hivyo.
SHUKRANI KWA KAMATI YA SIASA YA MKOA, AKIWEMO MWENYEKITI ALIYE MALIZA MUDA WAKE NA PIA PONGEZI KWA MWENYEKITI MPYA WA UVCCM GEITA KWA KUSHINDA UCHAGUZI.
Pia Ndg Wenseho Siwale bado hajawasahau kuwashukuru baadhi ya viongozi wa chama katika mkoa wa Geita.
Kwanza anaishukuru kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Geita, kwa kukubali na kupitisha jina lake ili awe mmoja ya wagombea katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita.
Pili, ananshukuru Mwenyekiti wa CCM (M) Geita alie maliza muda wake Ndg Saidi Kalidushi kwa uongozi wake mzuri na kukijenga vyema chama hadi kufikia hapa kilipo sasa.
Tatu, anampongeza Mwenyekiti Mpya UVCCM mkoa wa Geita aliyeshinda uchaguzi mpya ngazi ya mkoa Ndg Manjali Magambo kwa imani aliyopewa na wajumbe wa mkutano huo hadi kumchagua.
Anatoa ushauri kwake ajaribu kushuka hadi chini kwenye ngazi ya shina na mitaa kujua changamoto zinazo wakabili vijana na kuzitatua.
Pia ajitahidi kuonndoa makundi kati ya walio nacho na wale wasio kuwa nacho ili CCM na taasisi zake ibakie kuwa kimbilio la wengi.
OMBI KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA UCHAGUZI CCM (M) GEITA KUMPIGIA KURA NDG WENSEHO SIWALE.
"Mimi Ndg Wenseho Siwale, mkazi wa Mtaa wa Mwatolole, kata ya Buhalahala, tawi namba 6, ninayo heshima na mapenzi makubwa ya kuja mbele yenu ninyi wajunbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa CCM mkoa wa Geita, kuomba kura zenu za ndio ili kunichagua kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM mkoa wa Geita kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2027.
Malengo yangu ikiwa nitachaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM mkoa wa Geita, nitawaunganisha watu wote na makundi yote kuwa wamoja na kuishi bila ubaguzi kwa aliye nacho na asie nacho.
Pia nitahimiza kwa nguvu zangu zote agenda ya utunzaji mazingira, kuhamasisha vijana kujiajiri na pia kuongeza hamasa kwa vijana wa leo kupenda kushiriki katika siasa na kukichagua Chama cha Mapinduzi yaani CCM kuwa kimbilio lao"
Ahsanteni.
"KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI "
Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndg Samia Suluhu Hassan |
Jengo la CCM Makao Makuu Dodoma, panapofanyika vikao vya maamuzi vya CCM. |
Ukumbi mpya wa mikutano wa CCM wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma inapofanyika mikutano mikubwa ya CCM. |
Mwisho.
0 Comments