Na Urban Epimark, GEITA.
Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Geita imetoa pongezi nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoijali sekta ya elimu nchini ambapo ametoa fedha nyingi kuwezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa ya kutosha kwa wanafunzi watakao anza kidato cha kwanza mwakani mwezi January 2023 katika wilaya ya Geita na kuondoa mzigo kwa wazazi kuchangia ujenzi huo.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Geita Ndg Barnabas Mapande akiiongoza kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Geita leo katika kukagua hatua ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayo jengwa kwa fedha zilizotolewa kwa sekta ya Elimu na Rais Samia katika Halmashauri ya Mji wa Geita na kuridhishwa na viwango vya ubora na kasi ya ujenzi huo na kuashiria kukamilika kwa wakati.
"Tunampongeza Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyo tutoa kimasomaso sisi wananchi wa Geita baada ya kutuletea tena kwa mara ya pili pesa za ujenzi wa vyumba vya madarasa 71, ambapo zitamaliza uhitaji wa madarasa ili kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani January 2023" alisema.
Ndg Mapande ametoa pongezi hizo katika kata za Kalangalala na Kanyala zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Geita na kusema, isingekuwa moyo wa upendo na kujali wa Rais Samia kwa watanzania na kuwaletea pesa za ujenzi, kipindi hiki wazazi na walezi wangekuwa wakisumbuliwa kutoa michango ya kuchangia ujenzi huo.
Ametaja takwinu za mahitaji ya vyumba vya madarasa yaliyokuwa yakihitajika ili kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza jumla yao ikikadiriwa kufikia 7,000 wanao tarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwakani katika wilaya ya Geita, ambapo mahitaji ni vyumba 150 lakini vilivyokuwepo ni 80 tuu, hivyo pakawa na upungufu wa vyumba 70, alifafanua Ndg Mapande.
Katika ziara hiyo iliyo anzia Shule ya Sekondari Kalangalala, Mkuu wa shule hiyo Mwl Godfrey Mahewa aliiambia kamati hiyo kwamba, Kalangalala Sekondari ilipokea mwanzoni mwa mwezi October 2022 kiasi cha pesa shilingi milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 9 vya madarasa na ofisi moja ya waalimu.
Mkuu huyo wa shule aliendelea kufafanua katika taarifa yake kwamba hadi sasa kiasi cha fedha milioni 95.44 zimeshatumika na kiasi kingine cha shilingi milioni 84.54 bado zipo benki na ujenzi umefikia hatua ya kupaua.
Halikadhalika katika Kata ya Kanyala, shule ya sekondari Mkangara, Mkuu wa shule hiyo Mwl Elbert Kamugisha alieleza katika taarifa yake mbele ya kamati ya siasa kwamba mnamo October 02, 2022 shule hiyo ilipokea kiasi cha fedha shilingi milioni 140 za ujenzi wa vyumba vya madarasa 7 ambapo kasi ya ujenzi wake ni nzuri na hatua iliyofikiwa hadi sasa ni asilimia 47% na ujenzi unatarajiwa kukamilika November 27, 2022.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo imeipongeza Halmashauri ya Mji wa Geita kwa mipango mizuri ya matumizi ya fedha zilizo tolewa na Mhe Rais Samia ambapo kamati ya siasa imeridhishwa na ubora wa ujenzi na vifaa vinavyotumika lakini pia kwa kasi kubwa.
Mbali na pongezi hizo kwa Halmashauri hiyo ya Mji wa Geita kamati hiyo imepongeza pia ushirikiano baina ya madiwani na kamati za siasa kwenye kata, kuajiri wenyeji wa maeneo hayo wakiwemo akina baba, akina mama na vijana pamoja na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi katika maeneo hayo na kusema, mpango huo ni wa kizalendo unaotakiwa kupongezwa.
Mwisho.
0 Comments