TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SERIKALI YA MTAA KUWACHUKULIA HATUA WANANCHI WANAOACHA VISIMA VYA MAJI WAZI BILA USALAMA KWA WATOTO

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mkoani mjini Geita wakifunika kisima kwa vipande vya mabati na mbao baada ya tukio la Mtoto Mathias Nestory(3)kutumbukia kwenye kisima hicho na kufariki dunia.

Salum Maige,Geita.

Serikali ya mtaa wa Mkoani Halmashauri ya mji wa Geita,mkoani Geita,imewataka wakazi wa mtaa huo kuhakikisha wanakuwa walinzi kwa watoto wadogo na kutumia mifuniko imara kwenye visima vya maji vilipo kwenye makazi yao.

Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Salvatory Daniel siku chache baada ya tukio la mtoto wa miaka mitatu kufariki dunia katika mtaa huo kwa kuzama ndani ya kisima kilichopo nyumbani kwao.

Mtoto huyo aliyekuwa akiitwa Mathias Nestory alifariki Novemba 6,mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada ya kutumbukia kwenye kisima kinachokisia kuwa na urefu wa futi 30.

Kutokana na tukio hilo,Mwenyekiti Daniel amewataka wananchi wake kuhakikisha visima vyote vilivyopo kwenye makazi yao vinakuwa na mifuniko imara ili kuwa salama kwa uhai wa watoto wadogo.

Jamani tukio hili ni la kusikitisha,tuweni walinzi kwa watoto hivi visima ambavyo havina mifuniko imara vinahatarisha usalama wa watoto wetu,ona huyu mtoto amepoteza maisha kwa uzembe wa kutofunika hiki kisima”alisema mwenyekiti huo.

Pia,amewataka wananchi hao kutoa taarifa wanapoona visima vikiwa wazi ili waweze kuchukua hatua kwa wamiliki wa visima hivyo kwani vimekuwa hatarishi kwa watoto wadogo.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ni kwamba inasemekana mtoto huyo alitumbukia kwenye kisima hicho wakati akifuatilia ndala yake aina ya yebo iliyokuwa imetumbukia ndani ya kisima hicho.

Kisima cha maji kilichosababisha Mtoto Mathias Albart(3)kufariki dunia baada ya kutumbukia ndani ya kisima hicho alipokuwa akifuatilia ndala yake aina yeboyebo iliyokuwa imezama ndani.

Inavyoonekana maana tuliona yeboyebo yake ndani ya kisima sasa nafikiri alikuwa anajaribu kwenda kuitoa ndala hiyo,naona ndo akawa amezam sasa”alisimlia Jeremia Chibuga ambaye alijitoa ndani ya kisima kumtoa mtoto huyo.

Chibuga alisema kuwa,mtoto huyo ni mtoto wa dada yake na kwamba alipewa taarifa za tukio na kufika kwenye familia ya dada yake na kukuta mtoto akiwa ndani ya kisima ambapo alichukua uamzi wa kuingia kwenye kisima hicho kwa lengo la kumuokoa.

Hata hivyo juhudi za kumtoa ndani ya kisima hicho akiwa hai hazikufanikiwa kutokana na kukaa kwa muda mrefu kwenye kisima na hivyo aliopolewa akiwa tayari ameshafariki.

Maana nilikuta kamba juu ya kisima ,naona walijaribu kumtoa wakashindwa,hivyo nilivua nguo nikaingia ndani ya kisima ingawa hali haikuwa nzuri kuna hewa ya ukaa,nilifika nikajifunga kamba nikambeba mtoto mtoto ndipo watu waliokuwa nje wakanivuta kunitoa nje”

“Licha ya kufanikiwa kumtoa mtoto alikuwa ameshafariki ingawa wengine walisema bado hajafa ,ndipo tulichukua bajaji tukampeleka Hospitali ya Geita lakini tulipofika wakasema ameshafarikia”alisema Chibuga.

Baba mzazi wa mtoto huyo ,Nestory Albart alisema,alipokea taarifa za tukio hilo kwa njia ya simu akiwa kazini kwake akiarifiwa kwamba mwanae Mathias ametumbukia kisima na tayari ameshafariki dunia.

“Dah,nimeumia sana,imekuwa ghafla mno,hiki kisima sikujua kama kipo wazi maana mwanamke ndiye huwa anachota maji,nahisi mwenye nyumba wetu alikuwa anajua,lakini sasa hakuwa ameweka mfuniko mwingine,lakini mfuniko mwanzo ulikuwepo”alisema  Albart.

Juhudi za kuzungumza na jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita hazikufanikiwa mara moja kutokana na kuwa kwenye majukumu mengine ikiwemo kushiriki katika zoezi uokozi wa ajali ya ndege iliyotokea Novemba 6,mwaka huu huko mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments