Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Mpango akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Ukerewe alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza mwishoni mwa juma. |
Na Mwandishi, UKEREWE.
Makamu wa Rais Mhe Dkt Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Afya kufanya uchunguzi wa gharama za ujenzi wa Hospitali ya Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza ili kubaini endapo upo ubadhirifu wa fedha katika mradi huo.
Dkt Mpango alitoa maagizo hayo mwishoni mwa juma alipofanya ziara mkoani Mwanza na kutembelea na kuongea na wananchi na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe.
Mradi huo wa ujenzi wa hospitali hiyo ambapo serikali imekwishapeleka shilingi bilioni 3 katika mradi huo umelenga kuipandisha hadhi hospitali ya Wilaya Nansio kuwa hospitali maalumu ya mkoa kulingana na jiografia ya wilaya ya Ukerewe kuwa na visiwa vingi vilivyo umbali mrefu kufika jiji la Mwanza ambapo ndipo ilipo hospitali ya Mkoa hali inayosababisha changamoto kwa wananchi kusafiri umbali mrefu hasa kwa wagonjwa mahututi.
Mhe Dkt Mpango alitoa agizo hilo baada ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Joseph Mkundi pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza Mhe. Reuben Sixbeth kulalamikia kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ambao wanatarajia uwe mkombozi kwa wananchi hasa kutokana na jiografia ya wilaya hiyo.
Imefahamika kuwa, Mradi huo unasimamiwa na Mhandisi Mshauri na kujengwa na Kampuni ya Suma JKT ambayo iliingia mkataba na Wizara ya Afya.
Hata hivyo CCM Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Ukerewe imekuwa ikibainisha mapungufu kadhaa katika mradi huo hali iliyosababisha Wizara ya Afya kuanza kuyafanyia kazi kwani tayari viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya wamekwishafika kukagua mwenendo wa ujenzi huo akiwemo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe aliyeongozana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dk. Godwin Mollel, ambao waliunda timu ya uchunguzi mwezi Juni mwaka huu 2022 lakini majibu hayajawahi kuwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Denis Mwila.
Mwisho.
0 Comments