Wananchi wa Wilaya ya Ukerewe wakimsikiliza Makamu wa Rais Mhe Dkt Philip Mpango (hayupo pichani) alipokuwa akiongea nao wakati alipofanya ziara ya kutembelea mkoa wa Mwanza mwishoni mwa juma. |
Na Mwandishi, UKEREWE.
Zaidi ya mawakala 80 waliokuwa wakikusanya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, ambao walienda kinyume kwa mujibu wa mikataba yao ya ukusanyaji wa mapato hayo wamesitishiwa mikataba yao, kuondolewa kwenye uwakala na kufikishwa kwenye vyombo vya uchunguzi.
Hayo yamebainika ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Makamu wa Rais Mhe. Dk. Philip Mpango alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo na kumuagiza Naibu Waziri wa OR- TAMISEMI David Silinde kukagua mwenendo wa uendeshaji wa halmashauri hiyo kutokana na uwepo wa malalamiko mengi ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Emmanuel Sherembi amesema agizo hilo la Makamu wa Rais alilolitoa Novemba 25, 2022 alipokuwa wilayani humo kwenye ziara ya kikazi ni kweli lilikuwepo na tayari ofisi yake ilikwishalifanyia kazi na wahusika wote walikwishapelekwa kwenye mamlaka za uchunguzi wakiwemo mawakala na watumishi wa umma wasio waadilifu kwenye fedha za serikali.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sherembi amefafanua kwamba mawakala hao ni wale waliobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambao waliohusika na ubadhirifu wa fedha hizo kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018, 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021 ambao tayari alikwishawasilisha majina yao yote katika mamlaka za uchughuzi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) ambapo uchunguzi unaendelea.
“Mawakala hao ni ambao hawakupeleka fedha benki, waliofanya udanganyifu kwa kukusanya mapato chini ya kiwango na wote waliothibitika hawakupeleka fedha benki tumewasitishia mikataba yao na kuondolewa kazini ikiwa sambamba na wale ambao walikuwa wakifanya udanganyifu kwa kukusanya chini ya kiwango wao tumewaamuru warejeshe fedha hizo wengine wamekwisharejesha ambao walishindwa kurejesha tumewapaleka kwenye vyomba vya uchunguzi kwa hatua zaidi,” amesema Sherembi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Sherembi ofisi yake imeendelea kufuatilia utendaji kazi wa wakusanya mapato na pale wanapobainika kukiuka mikataba inachukua hatua mara moja.
Amesema Pamoja na hatua ambazo halmashauri imechukuwa dhidi ya wabadhilifu hao lakini imejiwekea mikakati mbalilmbali ili kuendelea kudhibiti suala hilo la mawakala na watumishi wasiokuwa waadilifu ikiwemo kupata taarifa za kila siku za ukusanyaji wa mapato kwa fedha zilizokusanywa na zilizowekwa benki kupitia ripoti ya posi ya kila siku ya mapato pia jedwali la taarifa na kufanya doria za mara kwa mara.
“Tumeweka katika bajeti jumla ya Shilingi Milioni 500 kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 100 inatokana na mapato ya ndani ya halmashauri na Shilingi Milioni 400 kupitia bajeti ya serikali kuu kwa lengo la kutengeneza vyomba vya usafiri ili kuweza kuyafikia maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukarabati wa boti mbili ambao unaendelea kwa sasa.
Tunaamini kupitia vyombo hivyo vya usafiri vitaimarisha ufuatiliaji wa mapato hasa kwa kufanya doria za mara kwa mara majini kupitia watumishi na maafisa uvuvi walioko katika maeneo hayo hivyo kuweza kudhibiti utoroshaji wa mapato unaofanywa na wafanya biashara wa mazao ya samaki wakiwemo mawakala na watumishi wasiokuwa waaminifu,” amesema Mkurugenzi Sherembi.
Ikumbukwe kuwa halmashauri ya wilaya ya ukerewe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imepanda ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi bilioni 1.7 hadi bilioni 3.086 sawa na asilimia 91.5 ya lengo la mwaka.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Sherembi, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 miradi ya sekta mbalimbali katika halmashauri hiyo imeendelea kutekelezwa kupitia fedha za mapato ya ndani yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.2.
Baadhi ya miradi uliyotekelezwa na halmashauri hiyo ni ujenzi wa kituo cha afya Igalla milioni 490, ujenzi wa vyumba 14 vya madarasa shule ya kwa shule za msingi kiasi cha milioni 140, ukamilishaji wa jengo la utawala sekondari ya Igalla milioni kiasi cha shilingi milioni 10, ujenzi wa mnada awamu ya kwanza Kijiji cha Hamkoko Kata ya Ngoma milioni 40, ujenzi wa chumba cha maabara katika shule ya sekondari Chif Rukumbuzya shilingi milioni 30, kulipa fidia ya ardhi mradi wa shule ya sekondari kakerege kiasi cha shilingi milioni 29.8, utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi milioni 219 kutolewa, ununuzi wa gari mpya aina ya Toyota Hilax na ujenzi wa choo chenye matundu matatu na bafu mbili katika soko la mbao Nakatunguru kiasi cha shilingi milioni 10.
Mwisho.
0 Comments