Na Urban Epimark, MWANZA.
Serikali imeagiza vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hapa nchini viunganishwe na Mkongo wa Taifa ili kupunguza gharama za uendeshaji huku wahitimu wa chuo hicho wameaswa kutumia vema elimu wanayopata kuleta tija kwa Taifa.
Hayo yamesemwa Jijini Mwanza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Mpango wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambapo alikuwa Mgeni Rasmi.
Aidha, Mhe. Mpango ameagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha mpango huo unafanyika haraka wa kuviinaunganishaa vituo hivyp na mkongo wa Taifa haraka ili kuwezesha matumizi ya TEHAMA na kupunguza mzigo wa gharama kwa wanavyuo pamoja na uendeshaji kwa upande wa uongozi.
"Vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria viunganishwe na mkongo wa Taifa na hili naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha linafanyika haraka ili kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji," ameongeza Mhe. Dkt Mpango.
Awali akiongea katika mahafali hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, alisema Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimetengewa fedha kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu pamoja na kusomesha wahadhiri na pia kufanikisha miradi mingine.
Sehemu ya wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wakiwa katika Mahafali ya 41 ya Chuo hicho yaliyofanyika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo November 24, 2022 |
"Serikali kwa kutambua mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kupeleka elimu kwa jamii kupitia mradi wa HEET tutajenga maabara saba katika mikoa ya Njombe, Arusha, Dodoma na Mwanza" alisema Waziri Mkenda.
Halikadhalika mikoa mingine itakayo nufaika na fedha hizo ni pamoja na Kigoma, Mtwara na Pwani.
Waziri Mkenda alifafanua zaidi kwamba fedha hizo zitawezesha chuo hicho kujikita zaidi katika tafiti za kisayansi kulingana na shughuli na mahitaji muhimu ya eneo husika.
Wakati huo huo Waziri Mkenda ameongeza kwa kusema kwamba Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8/= kwa ajili ya kujenga vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Yanzania katika mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Simiyu na Manyara ambapo mikoa hii ilikuwa ikitumia majengo ya kukodi kwa gharama kubwa.
Zaidi ya Wahitimu 4,000 wametunukiwa Shahada mbalimbali za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, zikiwemo Shahada za Umahiri na Uzamivu wakiwemo pia wanafunzi kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Wanafunzi wengine wa kigeni ni kutoka mataifa ya Ghana, Malawi, Zambia, Congo, Namibia na Ethiopia ambapo nao wametunukiwa Shahada katika mahafali hayo yaliyofanyika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Mwisho.
0 Comments