TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WAKATOLIKI GEITA WAANZA KAMPENI YA KUPANDA MITI

Paroko wa Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Jimbo Katoliki la Geita Padre Gerald Singu akipanda mche wa mti wa matunda katika kuzindua kampeni ya kila familia kupanda miti miwili, leo November 13, 2022

Na Urban Epimark, GEITA. 

Waraka wa kichungaji wa "Laudato Si" wenye maana ya "Sifa Iwe Kwako" ulio tolewa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis umeanza kutekelezwa kwa vitendo katika Jimbo Katoliki la Geita.

Waraka huo unao himiza utunzaji wa mazingira kwa lengo la kuhifadhi uumbaji wa Mungu kwa dunia nzima na vyote vilivyomo, umeanza Jimboni Geita kwa uzinduzi wa kampeni ya kila familia au kaya kupanda miti miwili ya matunda au mbao nyumbani kwake na kuitunza ili kurejesha uoto wa asili ulio potea na kusaidia mvua ziwe zikinyesha kwa msimu wake.

Leo Jumapili asubuhi November 13, 2022 baada ya Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu, Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Jimbo Katoliki la Geita, Paroko wake Padre Gerald Singu alizindua kampeni hiyo kwa kubariki na kupanda mche wa mti wa matunda katika eneo la Shule ya Awali ya Mt Alois iliyopo jirani mwa parokia hiyo.

"Nendeni nanyi mkafanye hivyo kwenye familia zenu na kaya zenu. Hakikisheni jambo hili kila mmoja analifanya kwa uaminifu kwani tumeharibu uoto wa asili na mvua sasa hainyeshi tena kwa wakati wake. Endapo tukifanya hivyo kwa miaka 10 ijayo, lazima hali ya mazingira yetu itarejea na tutaweza tena kupata mvua za msimu ilivyo kawaida" alisema Padre Singu.


Paroko, Padre Gerald Singu akianda mche wa mti wa matunda tayari kwa kuupanda leo November 13, 2022

Padre Singu aliendelea kufafanua zaidi kwamba, duniani kwa sasa joto limezidi na kuongezeka kuliko kawaida sababu ya kuongezeka zaidi hewa ya ukaa katika utando wa anga na kusababisha  jua la asubuhi saa 5 kuwa kali zaidi tena lenye joto ambalo si kama Mungu alivyo kusudia, aliongeza hivyo.

Akitoa tangazo la kuzindua kampeni hizo ambazo zitafanyika kila baada ya Misa Takatifu parokiani hapo, Katibu wa Parokia Bw Emanuel Mehendeka aliwatangazia wakristo kwamba, 

"Kila familia itawajibika kupanda miti miwili ya matunda, mbao au kivuli na kuitunza vyema hadi ikue. Na watoto katika familia watawajibika kuimwagilia maji kila asubuhi na jioni, na pia viongozi wote wa mitaa na jumuiya zote ndogo ndogo wanatakiwa kuandaa taarifa ya zoezi la upandaji miti mitaani kwao na kuileta parokiani kwa uongozi ili baadae ukaguzi wa kanisa uweze kufanyika ili kujiridhisha" alieleza Bw Mahendeka.


Wanakwaya wakiimba wakati wa zoezi la uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti miwili katika kila familia katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Jimbo Katoliki la Geita leo November 13, 2022

Baada ya kumalizika mkutano wa 20 wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yaani AMECEA, uliofanyika jijini Dar es Salaam mwenzi July mwaka huu, ulitoka na maazimio ya kutekeleza waraka wa "Laudato Si" kwa vitendo katika kila Jimbo Katoliki.

Halikadhalika Jimbo Katoliki la Geita, chini ya Mchungaji wao Askofu Flovian Kassala pamoja na mapdre wote Jimboni humo na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Walei kutoka kila Parokia, walikutana katika ukumbi wa Shule ya Mt Alois, iliyopo mjini Geita na kujadili jinsi ya kutekeleza waraka huo.


Paroko, Padre Gerald Singu akiuombea mti huo baada ya kuupanda ili ustawi na kukuwa. Yeye mwenyewe ameahidi kuutunza kwa kuumwagilia maji kila siku, na endapo akisahau ameomba akumbushwe kufanya hivyo.


Paroko, Padre Gerald Singu akiwabariki wakristo baada ya kuzindua zoezi la upandaji miti katika kila familia, uliofanyika eneo la Shule ya Awali ya Mt Alois iliyopo mjini Geita leo November 13, 2022


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments