Na Urban Epimark, GEITA.
Mamlaka zinazo wasimamia na kuwalipa haki zao waalimu wa makundi yote katika wilaya ya Geita wametakiwa kuwalipa waalimu stahiki zao zilivyo pangwa na serikali kwa wakati ili waweze kuendelea kufundisha kwa moyo.
Mamlaka hizo ni pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Geita pamoja na Chama cha Waalimu (CWT) na zinginezo zinazo simamia waalimu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo kwenye kilele cha kuhitimisha Wiki ya Elimu ya Watu Wazima iliyofanyika Uwanja wa CCM Kalangalala leo November 10, 2022.
"Natoa pongezi nyingi kwa wadau wa elimu katika wilaya yetu ya Geita kuendelea kuthamini mchango wa Wiki ya Elimu ya Watu Wazima lakini pia nitoe rai kwamba, kile kilichopangwa na serikali kwa ajili ya kuwalipa waalimu mamlaka zifanye hivyo kwa wakati ili waweze kuendelea kufundisha kwa moyo" alisema.
Mkuu wa Wilaya aliendelea kueleza zaidi kwamba, jamii ishirikiane kikamilifu kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi shuleni kwa makundi yote lakini pia viongozi, wasimamizi na wadau wote wa elimu waendelee kujitoa kuiboresha sekta ya elimu ili iweze kuleta tija zaidi kwa Taifa.
Halikadhalika Mkuu wa Wilaya Mhe Wilson Shimo ametoa rai kwa jamii kutumia fursa ya Elimu ya Masafa kujiendeleza kielimu ili kujipatia maarifa mapya ya kukabiliana na changamoto za kimaisha,
"Ni zamu yetu sisi wananchi bila kujali rika kutumia mpango huu wa elimu ya masafa na mambo mengine yeyote yanayosaidia upatikanaji wa Elimu ambapo hata kama upo njema ya mfumo, itumieni itasaidia" amesisitiza DC Shimo.
Ameshauri pia kwamba, jamii iendelee kuwafichua wanao waficha walemavu ili wasikose fursa ya kupata elimu kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imetoa fursa nyingi za kusoma, hata mtu akiwa mtu mzima.
Kuhusu uboreshaji wa mazingira ya kufundishia Mkuu wa Wilaya amesema, mipango ifanyike kuongeza madarasa yanayotumiwa na wanafunzi wa mfumo wa MUKEJA kwani bado lipo tatizo kwa jamii kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Jambo jingine aliloshauri ni kuwezeshwa mifumo ya madarasa ya kufundishia pamoja na waalimu wa Mpango wa Uwiano kati ya Elimu na Jamii, kwa kifupi MUKEJA.
Nae Afisa Elimu ya Watu Wazima katika Halmashauri ya Mji wa Geita Bi Recho Mwera wakati akisoma taarifa ya utekelezaji ya Elimu ya Watu Wazima alisema,
"Hali ya utoaji elimu kwa makundi maalum sio ya kuridhisha sana kwa sababu ya kutokuwezeshwa vyema kwa waalimu na pia baadhi ya wazazi kuendelea kuficha walemavu" alisema Afisa Elimu Watu Wazima.
Pia alitaja sababu zingine ni pamoja na jamii kuzongwa zaidi na shughuli za kijamii au kimaisha na wengine kukosa uelewa wa elimu ya watu wazima na manufaa yake.
Wiki ya Elimu ya Watu Wazima hufanyika kila mwaka kote nchini ikiwa lengo lake ni kutoa fursa kwa watu wazima kukutana na kutathmini jinsi ya kuendeleza jamii na kuhamasishana juu ya kuandikasha watoto shule katika umri sahihi.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni kuboresha mazingira ya kujifunzia kusoma, kuandika na kuhesabu yatakayozingatia ubora, usawa na utumishi wa makundi yote.
Wazazi, Walezi, Wanafunzi na washiriki mbalimbali waliohudhuria kilele cha kuhitimisha Wiki ya Elimu ya Watu Wazima iliyofanyika Uwanja wa CCM Kalangalala leo November 10, 2022 |
Mwisho.
0 Comments