Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Mpango akipokea maoni ya wananchi alipokuwa ziarani Ukerewe. |
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza wameiomba serikali kushusha bei ya mahindi yanayotolewa kwa ajili ya msaada kutoka Sh 930 kwa kilo moja ya sasa angalau ifikie Sh 850 ili wananchi wengi waweze kumudu kununua kwani wanakabiliwa na upungufu wa chakula.
Pia wananchi wa Wilaya hiyo wameomba mahindi hayo yawe yanapatikana katika maeneo mbalimbali wilayani humo ili kurahisisha upatikanaji wake.
Wananchi hao walitoa maombi hayo leo Novemba 25, 2022 wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii katika viwanja vya Getrude Mongella vilivyopo Nansio Ukerewe Mkoani Mwanza baada ya kutoa malalamiko yao kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Philip Mpango alipokuwa akiwahutubia akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Mafuru John, Hawa Kuzenza na Nashon Masumbuko walisema bei hiyo ni kubwa kwani inakuwa haina tofauti sana na ile wanayouziwa sokoni ya shilingi 20,000 kwa debe moja lenye kilo 20 sawa na sh 1,000 kwa kilo moja hivyo tofauti ni Sh 700 tu.
“Tunajua nia ya serikali ni nzuri sana ya kutusaidia wananchi wake ili tuweze kumudu gharama za mahindi hasa ukizingatia kwamba wilaya yetu ilikumbwa na ukame wa muda mrefu uliosababishwa na kukosekana kwa mvua ambao umesababisha tuwe na upungufu wa chakula tunaomba watushushie bei ili tuweze kununua,” alisema John (mwananchi).
“Eneo tunalopata mahindi haya ni moja tu pale kwenye ghala la chakula sasa wanaotoka mbali unakuta gharama ya nauli inakuwa kubwa bora tu wanunue hukohuko waliko lakini kama tutawekewa maeneo tofauti tofauti itatusaidia sana kupunguza gharama za nauli,” alisema Masumbukuo (mwananchi).
“Mimi naishukuru sana serikali kwa kutuletea mahindi haya yenye bei nafuu ingawa si nafuu sana maana tofauti ya Sh 700 ukilinganisha na bei ya sokoni ni kubwa lakini hali ya maisha ni ngumu hasa sisi wananchi ambao tunategenea kilimo na mwaka jana mvua hazikunyesha nyingi kwa hiyo kipato chetu bado ni kidogo, naamini Rais Samia atatusaidia kushusha bei ili ifikie sh 800 au 850 tutashukuru zaidi,” alisema Hawa (mwananchi).
Hadi sasa kituo kikuu cha uuzwaji wa chakula hicho (ghala) kipo katika kituo cha walimu Nansio (TRC - NANSIO) yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo.
kutokana na jografia ya wilaya kuwa ngumu kwa wakazi wote kufika katika ghala hilo (TRC -NANSIO) kwa uwepo wa visiwa vilivyo umbali mrefu kutoka makao makuu ya wilaya, halmashauri imeweka utaratibu wa kuwapelekea chakula hicho katika maeneo yao ya visiwa hivyo lengo ni kuwafikishia chakula wakazi wa maeneo yote ya wilaya hiyo na hadi sasa wakazi wa kisiwa cha Ukara wamesogezewa huduma hiyo.
Awali akizungumza katika mkutano huo kwa ruhusa ya Makamu wa Rais Mhe.Dk. Philip Mpango, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Joseph Mkundi(CCM) alisema ili kuwanusuru wananchi wake na janga la njaa lililosababishwa na ukame hivyo wananchi wengi kuwa na upungufu wa chakula alishirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kuomba chakula kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Mhe. Mkundi alieleza kwamba Wizara ilikubali kuwapa tani 300 za mahindi na hadi sasa wamekwishapokea tani 100 kutoka NFRA kwa bei elekezi ya Sh 930 kwa kilo moja ambapo wananchi wenye kipato cha chini ndiyo wanaonufaika na mahindi hayo kama lilivyokuwa lengo la kuomba msaada huo na kudai kwamba bei hiyo ni kubwa hivyo anaiomba serikali iwapunguzie ili wananchi wengi waweze kumudu gharama za kununua kwani wengi wao wanaupungufu wa chakula.
Ikumbukwe kwamba suala la ugawaji wa chakula cha msaada kutoka serikalini husimamiwa na Wizara ya Kilimo kupitia NFRA hivyo Mhe. Makamu wa Rais Dk. Mpango aliwaomba wananchi wawe wavumilivu wakati anashughulikia maombi yao ili kuwatatulia changamoto hizo.
Mwisho.
0 Comments