Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi Zahara Michunzi. |
Na Urban Epimark, GEITA.
Malalamiko ya kuhusu umiliki wa ardhi katika mji wa Geita yanaelekea kuongezeka siku hadi siku hususani baada ya maendeleo ya jamii kuongezeka kwa kasi na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kulalamika au kulalamikiwa kutokana na kutokujua taratibu na sheria zinazo husu umiliki wa ardhi.
Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi Zahara Michunzi ametoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye malalamiko kuhusu kuonewa au kukandamizwa kutokana na eneo analo miliki na kushindwa cha kufanya, afike ofisini kwake ili apatiwe mwanasheria wa kumsaidia kutatua changamoto hiyo.
"Naomba kutoa rai kwa yeyote mwenye kuhisi kuonewa au kukandamizwa kuhusu eneo lake la ardhi afike ofisini kwangu ili nimpatie mwanasheria wa kumsaidia kutatua changamoto hiyo" ameeleza Mkurugenzi.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibolelo Mwabasabi, Kata ya Nyankumbu katika Halmashauri ya Mji wa Geita Bw Stephano Samson aliitisha kikao na wanahabari ofisini kwake kuelezea kuhusu mwananchi mmoja wa eneo hilo kwa jina Bw Daniel Mashiri kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa sasa wa CCM wa Mtaa huo kupora eneo la chanzo cha maji ambalo ni mali ya mtaa huo.
Mwenyekiti huyo alienda mbali zaidi kwa kueleza kwamba, eneo hilo ambalo ni chanzo cha maji ya asili au chemchemi ni mali ya mtaa wa Ibolelo na hivyo uongozi wa mtaa ulikusudia eneo hilo liuzwe ili kupatikane fedha za kununua eneo jingine la kujenga shule.
Baada ya kupatikana mteja wa kununua eneo hilo kwa gharama ambayo uongozi wa mtaa ulipanga kuuza eneo hilo, alijitokeza mwananchi mmoja ambae kwa jina ni Bw Daniel Mashiri na kudai eneo hilo ni lake na hivyo si halali wao Serikali ya Mtaa kutaka kuliuza.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa mtaa huo Bw Stephano Samson kwa kushirikiana na wajumbe wa mtaa huo, walitoa taarifa hiyo kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyankumbu Bw Charles Mpanduji pamoja na Diwani wa Kata hiyo Mhe John Lunyabha na kuamuru Bw Daniel Mashiri kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na Kamanda wa Sungusungu wa Mtaa huo na kumpeleka ofisi ya Kata na baadae kituo cha polisi ambapo alilala rumande hadi alipodhaminiwa kesho yake.
Kwa vile sheria ya umiliki wa ardhi katika eneo la Halmashauri ya Mji au Wilaya inampa mamlaka Mkurugenzi wa Mji au wilaya kuwa ndie mwenye dhamana ya kusemea mambo yote yahusuyo ardhi katika eneo hilo, lakini pia mipango yote ya maendeleo katika eneo la Halmashauri huanzia kwa ngazi ya chini kwenye mtaa kama mapendekezo kisha hufikishwa kwenye ofisi ya Mkurugenzi ambapo yeye hulifikisha mbele ya Baraza la Madiwani na kujadiliwa na kisha kuwekewa maazimio.
Je, Suala la ardhi inayo lalamikiwa kwamba ni mali ya Mtaa wa Ibolelo iliyokusudiwa kuuzwa ili zipatikane fedha za ununuzi wa kiwanja cha kujenga shule ambapo ni maendeleo ya jamii ya watu wa mtaa wa Ibolelo, lipo kwenye mkakati wa utekekezaji katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita ama lah?
Mwandishi wa habari hii ilimlazimu kumtafuta Bw Daniel Mashiri, anae lalamikiwa kupora ardhi ya mtaa ili kujua ukweli ni upi.
Bw Daniel Mashiri (56)anaeleza kwamba eneo lililosababisha hadi yeye kukamatwa na uongozi wa Mtaa wa Ibolelo na kuwekwa ndani, ni mali yake na nieneo analolimiliki kihalali kwa kipindi cha miaka 35 sasa na aliuziwa eneo hilo mnamo mwaka 1987 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkolani, kata ya Nyankumbu Mzee Nassor Said Muyugumbi, mkazi wa eneo la Shinde Mkolani kwa gharama ya shilingi elfu 20 pamoja na bomba ya kupulizia dawa ya wadudu aina ya Solo kutoka Ujerumani mwaka huo 1987.
Bwana Daniel Mashiri aliendelea kueleza kwamba, anayo hadi nakala ya barua ya mauziano ya eneo hilo na pia aliyemuuzia ambae ni Mzee Nassor Said Muyugumbi, bado angali hai na ni mzima wa afya tele na tena anafanya kazi zake pasipo tatizo lolote.
Ndipo mwandishi wa habari hii alipoamua kumtafuta Mzee Nassor Said Muyugumbi na kufanya nae mahojiano kuhusu ukweli wa umiliki wa eneo hili jinsi ulivyo.
Baada ya kufika nyumbani kwa Mzee Nassor Said Muyugumbi yeye alieleza kinagaubaga kuhusu eneo hilo linalogombaniwa na mtaa na akasema hivi,
"Eneo hilo la chanzo cha maji ya asili katika mtaa wa Ibolelo lilikuwa langu tangu mwaka 1974 wakati wa serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere alipoanzisha Siasa ya Ujamaa Vijijini ambapo ardhi iligawiwa kuwa chini ya umiliki wa vijiji vya ujamaa. Eneo hilo nililipata kwa vile mimi nilikuwa mmoja wapo wa wajumbe 8 katika kata Kalangalala wakati huo, tuliopewa dhamana ya kutenga na kugawa maeneo ya ardhi" alieleza Mzee Nassor.
Mzee Nassor aliendelea kufafanua zaidi kwamba, wakati huo mwaka 1974 alipopatiwa eneo hilo lenye sehemu ya bonde la maji ya chemchemi yanayo toka chini na kuendelea kulimiliki kwa kufanya kilimo cha nyanya kwa muda wote hadi mwaka 1987 alipo amua kumuuzia Bw Daniel Mashiri ambae walikuwa wakilima nae nyanya pamoja katika eneo hilo, alieleza hivyo.
"Baadhi ya viongozi wa sasa hawana uadilifu katika uongozi. Badala ya kuwatumikia watu na kulinda mali zao ili ziwe salama, wanatumia mamlaka yao kuwaonea watu wanyonge, huku akielekeza moja kwa moja malalamiko yake kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibolelo Bw Stephano Samson kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyankumbu pamoja na Diwani wake kwamba wanaonea wananchi kwa sababu zao wenyewe" ameongea Mzee Nassor.
Mzee Nassor Said Muyugumbi kwa asili ni mwenyeji wa mkoa wa Tabora ambae alikuwa Mwenyekiti Mstaafu wa kilichokuwa kijiji cha Mkolani, katika Kata ya Kalangalala hapo awali kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 1975 hadi miaka ya 80.
Anasema katika uongozi wake watu walimpenda na kumwamini kwa vile alikuwa mwadilifu na alikuwa katika uongozi kwa kutenda haki na kuwasaidia watu wapate mahitaji yao na si kuwaonea.
Ametoa wito kwa viongozi wa sasa wapatiwe mafunzo ya uongozi kama ilivyokuwa zikifanya serikali za awamu zilizopita ili viongozi wajifunze miiko na mipaka ya uongozi ili wasionee watu na mali zao, alisema.
Alimalizia kwa kusema kwamba, ardhi hiyo ilikuwa ni yake, na yeye ndie aliye muuzia Bw Daniel Mashiri na haijawahi kwa muda wote huo kuwa mali ya serikali ya mtaa wa Ibolelo, alimalizia Mzee Nassor Said Muyugumbi.
Baada ya kujiridhisha kwa maelezo yote haya mwandishi wa habari hii, ndipo alipo bisha hodi kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita pamoja na Ofisi ya Afisa Ardhi ili kupata ufafanuzi kuhusu ukweli wa umiliki wa eneo hilo na Mkurugezi alisema,
"Eneo hilo kama limemilikiwa na mwananchi anaetajwa kwa muda wa miaka 35, inawezaje leo kugeuka na kuwa mali ya serikali ya mtaa wa Ibolelo bila Ofisi yake kuwa na taarifa hizo?" Aliuliza Mkurugenzi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita alienda mbali zaidi kwa kusema, mipango yote inayohusu ardhi, ikiwemo uendelezaji wake kwa maana ya kujenga, lazima Ofisi yake ipate taarifa na kutoa idhini ya kiofisi kufanya jambo hilo, alisema.
Pia amefafanua kwamba, endapo Halmashauri ya Mji wa Geita itahitaji eneo kama hilo kutoka kwa mwananchi anae limiliki, Ofisi yake huhakikisha wanakaa pamoja na mwenye eneo hilo na kukubaliana apewe fidia au apewe eneo jingine lenye thamani kama hiyo na si kupora kwa nguvu kama ilivyo kwa eneo la Mtaa wa Ibolelo, alieleza.
Halikadhalika Mkurugenzi amewataka watendaji wote wanao onea wananchi kuhusu mali zao wakiwemo watendaji wa mitaa na kata ambao wapo chini ya ofisi yake, waache tabia hiyo mara moja vinginevyo wakibainika, atawachukulia hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kuwasimamisha kazi kwa uchunguzi.
Kuhusu Diwani wa Kata ya Nyankumbu kushiriki kumkandamiza mwananchi anae lalamikiwa kwamba amepora ardhi ya mtaa, Diwani anajua taratibu zote za utekelezaji mipango ya Halmashauri na akaongeza kwamba, Diwani anatakiwa awe mstari wa mbele kuwasemea na kuwatetea watu wake walio mchagua na si kushiriki kumkandamiza mtu yeyote.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi Zahara Michunzi alimalizia kwa kusema, hataki kuona mtu yeyote akionewa kwa mali anayo imiliki na hivyo kutoa wito kwa wote wenye malalamiko kama hayo, wafike ofisini kwake ili awapatie mwanasheria wa kuwasaidia kuondoa changamoto hizo, alimaliza hivyo.
Mwisho.
0 Comments