TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

GPC YAOMBA MGAWANYIKO WA WAANDISHI GEITA UTATULIWE.

Mwandishi wa Habari wa Uhuru Digital Bi Rose Mweko akitoa ombi kwa viongozi wa serikali katika mkoa wa Geita kuingilia kati kusaidia kutatua tatizo la mgawanyiko ndani ya waandishi wa habari wa mkoa huo wakati alipopatiwa nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo (hayupo pichani) kwenye Mkutano mkuu maalum wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita (Geita Press Club) uliofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi leo December 22, 2022.

Na Urban Epimark, GEITA

Ombi limetolewa kwa viongozi wa serikali mkoani Geita kuingilia kati kusaidia kutatua tatizo la mgawanyiko uliopo ndani ya waandishi wa habari wa mkoa wa Geita ambao umedumu kwa muda sasa, kwani unachangia kudhoofisha jitihada za ufanisi wa utendaji wao wa kazi wasipokuwa na umoja katika mkoa huo.

Ombi hilo limetolewa na Mjumbe wa mkutano mkuu maalum wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita (Geita Press Club) uliofanyika leo December 22, 2022 katika ukumbi wa Bwalo la Polisi, ambae pia ni mwandishi wa habari wa chombo cha habari kinachomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) cha Uhuru Digital Bi Rose Mweko kwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo. 

"Ndugu Mgeni wetu Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Geita, tunakushukuru kwa kukubali kuja kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano wetu maalum wa leo. Pia tunashukuru sana kwa nasaha zako kwetu waandishi. Tuna waomba viongozi wa serikali katika mkoa wa Geita mtusaidie kumaliza tatizo la mgawanyiko ndani yetu waandishi hapa mkoani Geita kwani jambo hili linatukwamisha tusiweze kusonga mbele kwa umoja wetu. 

Mgeni Rasmi katika Mkutano mkuu maalum wa klabu ya waandishi wa habari  mkoa wa Geita (Geita Press Club) ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo (kushoto) akinong'onezwa jambo na Mwenyekiti wa klabu hiyo Bw Renatus Masuguliko (kulia shati jeupe) wakati wa Mkutano mkuu maalum wa GPC uliofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi mjini Geita leo December 22, 2022.

Pengine tunakiri yapo mapungufu tuliyo nayo lakini   ni vizuri ninyi viongozi wetu mkasaidia kutatua. Ninyi kwetu ni kama baba wa familia. Baba asipo simamia vyema familia yake, familia itagongana na kufarakana hivyo kwa niaba ya wenzangu niwaombe sana viongozi wetu msaidie jambo hili" alisema Bi Rose Mweko.

Bi Rose Mweko alikuwa akitoa neno la shukrani mbele ya Mgeni rasmi kwa niaba ya wanachama wa klabu ya waandishi wa habari  mkoa wa Geita kwa kumshukuru Mkuu wa Wilaya  Geita Mhe Wilson Shimo ambae katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, aliwapongeza waandishi wa habari mkoani Geita kwa kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa katika kuhabarisha jamii kwa usahihi mambo mbalimbali yanayoleta maendeleo ya watu na kuibua pia kero za jamii ili zishughulikiwe na viongozi.

Mkuu wa wilaya aliwapongeza wanahabari wa mkoa wa Geita kwa kujitoa kwao kikamilifu na kwa usahihi katika kuhabarisha jamii kwa wakati japo zipo changamoto Waandishi wanazo kabiliana nazo lakini hawakuvunjika moyo.

Baadhi ya wanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Geita (Geita Press Club) wakiwa ukumbini wakifuatilia kwa makini sana mijadala iliyokuwa ikiendelea kwenye mkutano mkuu maalum wa GPC uliofanyika ukumbi wa Bwalo la Polisi mjini Geita leo December 22, 2022.

Nae Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita (Geita Press Club-GPC) Bw Renatus Masuguliko kwenye neno lake la kumkaribisha Mgeni Rasmi katika mkutano Mkuu Maalum huo alisema,

"Dhamira ya GPC ni kujenga umoja ndani ya waandishi wa habari wa vyombo vyote vinavyo fanya kazi zao mkoani Geita na kwingineko na pia kujenga mahusiano mazuri baina ya Waandishi na viongozi wa ngazi zote hapa mkoani Geita ili vyombo vya habari viweze kusaidia kuleta maendeleo ya watu kwa kuhabarisha vyema" alisema hivyo Bw Masuguliko. 

Wakati huo huo wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa GPC wamempongeza Mwenyekiti wa Klabu hiyo ya GPC Bw Renatus Masuguliko kwa mtizamo na mawazo mapana ya kuwezesha Klabu hiyo kusonga mbele.

Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo (wa tatu toka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari  Mkoa wa Geita (Geita Press Club-GPC) mara baada ya kumalizika mkutano mkuu maalum wa GPC. Wengine ni Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Geita Bw Said Lipunjaje (mwanzo kulia) na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Thomas Joseph (wa tatu kutoka kushoto) ambae alimwakilisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita (RPC) katika mkutano huo.

Mjumbe mwingine wa mkutano huo Bw Gharos Riwa Kwath ambae anafanya uandishi wake wa habari katika kituo cha redio Rubondo FM ya mjini Geita alimpongeza Mwenyekiti wa GPC Bw Renatus Masuguliko na kusema wazi kuwa mwanzoni wakati anashika nafasi hiyo ya kuwa Mwenyekiti wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita alikuwa hamwelewi vizuri lakini kadiri siku zinavyo songa mbele anazidi kumwelewa vizuri zaidi katika utendaji wake ulio mahiri.

Mkutano huo uliidhinisha kupatiwa uanachama waandishi wawili wapya ambao ni Mathayo Marco Kanani (GPC Blog) na Bw Adeltus Lunyali(Geita Cable TV) na pia uliazimia mambo mbalimbali yatakayo anza kutekelezwa kwa mwaka mpya wa 2023. 

Mkutano mwingine Mkuu wa GPC wa kawaida wa kila mwaka kwa mujibu wa  katiba  umepangwa kufanyika mwezi February 2023.



Mwisho.

Post a Comment

0 Comments