TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

HATIMA YA WANANCHI WA GEITA WANAOISHI NDANI YA VIGINGI KWENYE LESENI YA MGODI WA GGML KUJULIKANA JANUARY 09,2023

Waziri wa Madini Mhe Dkt Doto Biteko akiongea na wanahabari mjini Geita mara baada ya kumalizika kikao hicho.

Na Urban Epimark, GEITA. 

Serikali imekataa na kutupilia mbali taarifa ya Kampuni ya Uchimbaji madini nchini ya AngloGold Ashanti ya mjini Geita (GGML) kuhusu ulipaji fidia za ardhi katika maeneo ya mgodi huo mkoani Geita na kutoa siku 14, hadi January 09, 2023 iwasilishe taarifa inayo takiwa.

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameikataa taarifa ya Mgodi wa Geita Gold Mine Limited (GGML) ambayo haijabainisha mahitaji ya ardhi katika leseni yake na hatma ya watu wanaoishi ndani ya vigingi katika leseni ya mgodi huo.

Dkt.  Biteko ameikataa taarifa hiyo iliyowasilishwa na Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashant inayomiliki mgodi huo Simon Shayo katika kikao kilichofanyika mkoani Geita ili ichakatwe upya kwa lengo la kujibu changamoto za wananchi wa Geita.

Kampuni ya AngloGold Ashant iliahidi kuwasilisha taarifa itakayotoa suluhisho la kudumu la changamoto ya kulipa fidia kwa wananchi wa Geita ili kupisha maeneo ya uwekezaji katika mgodi huo au kuendelea kuishi katika maeneo yao na kuyaendeleza ambapo taarifa hiyo haijaeleza masuala hayo.

Baadhi ya washiriki katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Geita wakiwemo wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ya mkoa huo.

Amesema malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Geita wanaoishi ndani ya vigingi kwenye leseni ya mgodi wa GGML ambao wananchi wanatakiwa kulipwa fidia ya maeneo yao ili kupishe uwekezaji au kuendelea kuishi na kuyaendeleza maeneo yao inapaswa kufika mwisho na kujulikana hatma ya changamoto hiyo.

"Katika taarifa ya GGML nilitarajia kusikia changamoto ya watu wanaoishi ndani ya vigingi vya leseni ya mgodi wanalipwa fidia au wanaachiwa maeneo yao lakini taarifa hii haijazungumzia hilo," amesema Dkt. Biteko.

Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Biteko amesema hadi kufikia Januari 09, 2023 mgodi huo uwe umewasilisha taarifa inayojibu changamoto zinazotakiwa kupatiwa majibu na hatma ya watu wanaoishi ndani ya vigingi vya mgodi huo ijulikane.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolfu Ndunguru (kulia) akiwa na Katibu Tawala (RAS) wa mkoa wa Geita Prof Godius Kahyarara (kushoto) wakiwa katika kikao hicho mjini Geita.

"Watu wanaoishi ndani ya vigingi vya mgodi wa GGML wameambiwa wasiendeleze maeneo yao, sasa wanalipwa fidia au wanaachiwa maeneo yao ili waendelee na maisha yao ikiwemo kuyaendeleza maeneo yao," amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ameutaka mgodi wa GGML kuichakata upya taarifa hiyo ili iweze kuwa na majibu ya hatma ya watu wa Geita ambao wameteseka kwa muda mrefu ili Wizara itoe muelekeo maalumu juu ya hatma ya jambo hilo.

Awali, Dkt. Biteko alikutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ambapo amewataka kuepuka vitendo vya udanganyifu katika biashara ya madini na badala yake kuwa waadilifu katika utendaji wa shughuli zao.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mhe Costantine Kanyasu (mwenye miwani) akifafanua jambo katika mkutano huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella amempongeza Dkt. Biteko kwa dhamira njema anayoionesha ili kumaliza tatizo lililodumu kwa muda mrefu la wananchi wanaomiliki ardhi kulipwa fidia katika maeneo yao ili kupisha eneo la leseni ya GGML au kuachiwa kuendeleza maeneo yao.

Naye, Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashant Simon Shayo  amesema, GGML imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Dkt. Biteko na kuahidi kuyafanyia kazi ili kupatina haki kwa pande zote.

Kikao hicho, kimehusisha Kampuni ya GGML, Serikali ya Mkoa wa Geita, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Geita mjini na Wataalamu kutoka Wizara ya Madini.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashanti Bw Simon Shayo (aliyesimama mbele kushoto) akiwasilisha hoja ya GGML kwenye mkutano huo ambapo Serikali imekataa kupokea ripoti hiyo.

Ni muda mrefu sasa tangu mpango huo wa kuwalipa fidia wananchi wa mkoa wa Geita hususani katika wilaya ya Geita ambapo tangu mwaka 2000 kampuni hiyo ya AngloGold Ashanti ilipoanza uwekezaji wake hapa nchini, wamekuwa wakizubiri kulipwa stahiki zao lakini hadi sasa bado hatma yao ya kulipwa ipo mashakani.

Naibu Waziri wa Madini Dr Steven Kiruswa (MP) akiwa na baadhi ya viongozi wa CCM katika mkoa wa Geita alipotembelea na kujioni baadhi ya shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) hivi karibuni.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments