Na Alphonce Kabilondo,Geita
KANISA huru la kipentekoste Tanzania (FPCT) jimbo la Geita Mkoani hapa limetoa msaada wa sabuni , sukari ,mafuta ya kupikia ,mchele pamoja na Ng’ombe mmoja kwa wafungwa wa gereza la Wilaya ya Geita kwaajili ya kuwawezesha kusherekea Sikukuu ya Kristmas na mwaka mpya 2023.
Askofu wa kanisa hilo Mch. David Nzumbi akikabidhi msaada huo amesema kuwa msaada huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni moja lengo likiwa ni kuwawezesha wafungwa kusherekea Sikukuu hizo kwa kuwa nao ni sehemu ya jamii .
Askofu huyo alisema kuwa msaada huo umetokana na michango ya waumini wa kanisa kufuatia utaratibu wa kanisa hilo wa kila mwaka kuwa tembelea wafungwa waliopo gerezani na kufanya nao ibada, kuwajulia hali na kuwatia moyo na kuwasaidia mahitaji mbalimbali .
“Tumekuja kufanya ibada na wafungwa leo na kuwasaidia mahitaji mbalimbali mafuta,sukari,sabuni, mchele , na kitoweo cha Ng’ombe kwaajili ya Sikukuu ya Kristmas, tumetimiza maandiko matakatifu tunaamini kuwa nao ni sehemu ya jamii wamo ndani yao watumishi wanamtumikia Mungu" alisema Askofu Nzumbi.
Justina John katibu wa wanawake wa kanisa la FPCT jimbo la Geita alisema kuwa katika kusherekea Sikukuu ya Kristmas tumeungana na waumuni wenzetu kuja kuwajulia hali wafungwa na kuwapatia mahitaji mbalimbali .
Aidha Mkuu wa gereza la Wilaya ya Geita mrakibu mwandamizi wa jeshi la magereza SSP Jovin Bujwina amelipongeza kanisa la FPCT Jimbo la Geita kwa msaada huo na ambapo ameshauri madhebu mbalimbali ya dini kuiga mfano wa kanisa hilo la FPCT Geita .
Mkuu huyo aliongeza kuwa waumini wa kanisa hilo wamefanya jambo jema la kuwasadia wafungwa hao na kwamba hawastahili kunyanyaswa wala kutengwa kwa kuwa nao bado ni sehemu ya jamii.
MWISHO
0 Comments