Moja ya aina za Groto ya Mama Bikira Maria inayo tumika kwa sasa na Kanisa Katoliki kwenye vituo vya sala au mahali pa kuabudia. |
Na Urban Epimark, GEITA.
Mwaka 2022 unafikia ukingoni kwa mafanikio makubwa kwa kalenda ya matukio ya mpango kazi wa kanisa katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Jimbo Katoliki la Geita na sasa imeweka hadharani mipango mipya ya utekelezaji kwa mwaka mpya wa 2023 ukijumuisha ujenzi wa "Groto ya Kuabudia ya Mama Bikira Maria" parokiani hapo pamoja na mengine mengi.
Mwaka huu 2022, parokia hiyo chini ya uongozi wa Paroko wao ambae pia ni Dekano wa Dekania ya Geita Padre Gerald Singu kwa ushirikiano mkubwa na uongozi wa Halmashauri ya Walei parokia ulikamilisha ujenzi wa kanisa jipya na la kisasa kwa gharama ya takribani BIL 2.0/= kupitia michango ya wanaparokia wenyewe kwa kipindi kifupi cha miaka miwili tuu pamoja na ujenzi wa nyumba ya mapdre na ofisi ya parokia na hivyo Askofu wa Jimbo la Geita Mhashamu Flavian Kassala kulitabaruku kanisa hilo rasmi March 19, 2022.
Haya ni mafanikio ya juu sana yaliyo jengeka katika msingi wa ukuaji imani kiroho baina ya wanakanisa wa eneo hilo na sasa wamepanga kujenga Groto ya kuabudia ikiwa ni mojawapo wa mipango mipya ya utekelezaji kwa mwaka 2023.
Akieleza baadhi ya maazimio ya mkutano mkuu wa kwanza katika kipindi kipya cha uongozi wa Halmashauri ya Walei Parokia uliofanyika jana December 10, 2022 na pia kutangaza maazimio hayo kwenye misa za jumapili leo December 11, 2022, Paroko Padre Gerald Singu amesema,
"......nina washukuru sana kwa kazi nzuri mliyoifanya ya ujenzi wa kanisa na hadi kutabarukiwa mapema mwaka huu na Baba Askofu Flavian Kassala, kupitia michango yenu na majitoleo yenu na hivyo sasa niwaombe tena moyo huo huo tuuelekeze katika ujenzi wa Groto ya kuabudia ya Mama Bikira Maria pamoja na ujenzi wa vyoo vipya na vya kisasa katika parokia yetu kwa mwaka mpya wa 2023" alisema Padre Singu.
Aliendelea kufafanua zaidi Paroko huyo kwa kuwasihii wakristo kuendelea kujitoa na kumtolea Mungu sadaka zao na ukarimu mwingine ambapo amewatia moyo kuongeza kidogo kiwango cha utoaji sadaka kanisani wakati wa misa za jumapili na siku nyingine ili parokia iweze kupata fedha za kutosha kugharamia mipango iliyopo mbele yake ikiwemo kuwategemeza watumishi wa kanisa ambao ni mapadre, masista na makatekista.
Katika hatua nyingi, Paroko Padre Gerald Singu ametangaza muundo mpya wa Jumuiya ndogo ndogo za kikristo (JNNK) parokiani hapo na kusema Jimbo Katoliki la Geita linategemea kutoa waraka mpya wa kila jumuiya iwe inaundwa na familia kati ya 7 na 15 na pale zitakapo ongezeka, jumuiya hiyo itabidi igawanyike ifanye jumuiya mbili.
Ufafanuzi alio utoa leo parokiani Paroko amesema, waamini wasiogope kuzigawa jumuiya zao zenye familia zaidi ya 15, kwani hakulengi ukusanyaji wa michango ya pesa bali kutaimarisha zaidi utoaji huduma za kiroho baina ya jumuiya husika na pia kuansha mwamko mpya kwa wale wavivu wa kuhudhuria sala za jumuiya na hivyo kuongeza ukuaji imani, ushirikiano na upendo baina ya wakristo wenyewe.
Muda wa kukamilisha mpango huo ikiwemo ujazaji wa nafasi za viongozi katika jumuiya zitakazo gawanyika ni February 04, 2023.
Mipango mingine ya kutekelezwa kwa mwaka 2023 ni pamoja na uwekaji mageti mawili ya kisasa ya kuingia kanisani hapo, uwekaji wa vigae eneo la nje ya kanisa (pavement blocks) pamoja na mingine mingi.
Mwisho.
0 Comments