TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SERIKALI YAKOSHWA UTENDAJI CHUO CHA MIPANGO.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo akisogeza kitambaa kuashiria uwekaji jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la Maktaba ya Chuo cha Mipango, tawi la Mwanza December 16, 2022. Pembeni yake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho Prof Martha Qorro (mwenye nywele fupi nyeupe).

Na Urban Epimark, MWANZA

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeupongeza uongozi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) kwa jinsi inavyowaandaa vyema vijana kushiriki katika kuwaletea maendeleo wananchi na usimamizi wa miradi mikubwa inayojengwa na serikali kwenye jamii.

Pia imekoshwa na usimamizi mzuri wa fedha za bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya majengo katika chuo hicho yakiwemo majengo ya utawala na madarasa katika kituo cha mafunzo cha kanda ya Ziwa Mwanza na kuahidi kuwapa majukumu zaidi ya kiutendaji wataalam hao wa chuo cha Mipango ili waisaidie zaidi serikali kupanga na kusimamia miradi maeneo mengine.

Pongezi hizi zimetolewa kwa nyakati tofauti na watendaji wa ngazi ya juu wa Wizara ya Fedha na Mipango akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi Jenifa Omolo na Mchumi Mkuu wa Wizara Bw Moses Dulle kwenye sherehe za mahafali ya 36 ya chuo hicho jijini Mwanza.

"Hakuna taasisi au ofisi yeyote hapa nchini isiyohitaji  kufanya mipango mizuri ya maendeleo katika kujiendeleza lakini pia upande wa tawala za mikoa na serikali za mitaa kunahitaji sana wataalam wa mipango wanao andaliwa na Chuo cha Mipango ili kusimamia miradi inayo anzishwa mikoani, hivyo wizara inapongeza juhudi kubwa inayofanywa na uongozi wa chuo cha Mipango" alisema Naibu Katibu Mkuu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo (wa pili kutoka kushoto) akielezwa jambo na Mkurugenzi wa Mipango wa wizara hiyo Bw Moses Dulle (mwenye kaunda suti katikati) wakati wa kuelekea kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Maktaba ya Chuo cha Mipango, tawi la Mwanza December 16, 2022. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza Prof Juvenal Nkonoki (kulia shati la draft) na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho Prof Martha Qorro (kushoto). Nyuma kidogo mwenye suti ya kijivu ni Mkuu wa Chuo hicho Prof Hozen Mayaya.

Naibu Katibu Mkuu Bi Jenifa Omolo alifurahishwa zaidi jinsi Chuo cha Mipango kinavyoshirikiana vizuri na Wizara katika kuboresha miundombinu ya chuo hicho katika kituo cha mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza  na hata kuweza kumwalika kuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kisasa la Maktaba ya chuo hicho pamoja na majengo ya kumbi za kufundishia (Lecturers Theater) na kusema serikali inajivunia sana watendaji katika chuo hicho.

Nae Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambae pia ndie Mkurugenzi wa Mipango wa wizara hiyo Bw Moses Dulle amewaeleza watumishi wa chuo hicho akiwemo Mkuu wa chuo Prof Hozen Mayaya na pia wakiwemo wajumbe wa Baraza la Uongozi wa chuo na watumishi wote wakati wa sherehe ya mahafali hayo kwamba, 

"Wizara ya Fedha na Mipango imeona kinachofanyika katika chuo hiki na hivyo wizara ina ahidi  itawatumia wataalam wa chuo hiki kuisaidia serikali katika kubuni na kusimamia mipango ya miradi mingine inayofanywa na serikali kupitia wizara yetu kwani mmeonesha umahiri mkubwa katika utendaji" alisema hivyo Mchumi huyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo (katikati) akiandamana na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Prof Martha Qorro (kulia) na Mkuu wa Chuo hicho Prof Hozen Mayaya (kushoto) katika kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Maktaba ya chuo hicho tawi la Mwanza December 16,2022.

Hivyo Mchumi huyo aliahidi kufanya ziara ya kikazi na kuonana na uongozi wa chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwenye Makao Makuu yake  yaliyopo jijini Dodoma mapema juma hili ili kujadili na kupanga jinsi ya kutekeleza jambo hilo.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, Prof Juvenal Nkonoki ameupongeza uongozi Kanisa la African Inland Church (AIC Tanzania) kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa chuo hicho hadi kukiwezesha kupata eneo la ujenzi wa kituo hicho, kilichopo mtaa wa Kisesa jijini Mwanza.

Halikadhalika ametoa pongezi kwa wazee wa kata ya Kisesa pamoja na uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Kata hiyo ya Kisesa katika mkoa wa Mwanza na kusema kama sio ushirikiano wao mzuri,  kamwe chuo hicho kisingeweza kufikia hapo kilipo sasa.

Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini duru ya pili, tawi la Mwanza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo akimpongeza mmoja wa waadhiri wa chuo hicho wakati wa mahafali hayo jijini Mwaza December 16, 2022.

Diwani wa Kata hiyo ya Kisesa Mhe Marko Kabadi alikosa cha kusema mbele ya Wawakilishi wa Wizara ya Fedha, Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Mkuu wa chuo hicho Prof Hozen Mayaya na watumishi wote wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini wakati alipopatiwa nafasi ya kuongea kwenye tafriji fupi ya kujipongeza iliyofanyika  katika ukumbi wa chuo hicho kwenye majengo ya zamani eneo la Bwiru Press na kusema, 

"Kata ya Kisesa inajivunia sana uwepo wa chuo hicho katika kata hiyo hivyo, tupo tayari kwa kutoa msaada wowote unaotakiwa na chuo hicho ikiwemo eneo la nyongeza la upanuzi wa chuo hicho katika Kata ya Kisesa" alimalizia hivyo Diwani huyo.

Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, kituo cha mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, mwaka huu kimefanya mahafali ya kumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 kwenye eneo dogo la Mtaa wa Bwiru Press, jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Prof Martha Qorro (aliye simama) akimweleza kwa ufupi Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo hatua ya maendelea ya miradi inayofanyika katika kituo cha mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, kabla ya kuweka jiwe la msingi la Maktaba ya chuo hicho. Kushoto anaesikiliza ni Mkurugenzi wa Mipango wa wizara ya Fedha Bw Moses Dulle jijini Mwanza December 16, 2022

Baadae mwaka 2019 chuo hicho kilipata eneo jipya na la kutosha la ujenzi wa majengo mapya ya chuo hicho katika Kata ya Kisesa na serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ikatenga bajeti ya kutosha ya ujenzi wa miundombinu.

Hadi sasa tayari pamejengwa jengo la kisasa la Utawala, kumbi za kufundishia, madarasa, mabweni na hivyo sasa  jengo kubwa la maktaba ya chuo linaendelea kujengwa ambapo Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango  Bi Jenifa Omolo tayari ameliwekea jiwe la msingi.

Inategemewa baada ya miaka mingine kumi ijayo, Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, tawi la Mwanza kitakuwa kituo kikubwa cha kitaaluma cha maendeleo ya mikoa katika kanda nzima ya Ziwa Mwanza na pia nchi za jirani.

Mkurugenzi wa kituo cha mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza Prof Juvenal Nkonoki akitoa maelezo mafupi wakati wa kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo (hayupo pichani) kituoni hapo December 16, 2022 wakati alipokuwa Mgeni Rasmi siku ya mahafali. Wengine jirani yake ni Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Fedha Bw Moses Dulle (kulia) na Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango upande wa Taaluma, Utafiti na Uelekezi Prof Provident Dimoso(Kushoto mwenye miwani).

Mkuu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Prof Hozen Mayaya (mwenye suti ya kijivu) akiwaongoza wageni kuelekea jengo la Utawala mara baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Maktaba katika kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza kilichopo Kata ya Kisesa December 16, 2022.



Mwisho.

Post a Comment

0 Comments