TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUBAINISHA FURSA ZA KIUCHUMI ILI KUVUTIA WAWEKEZAJI HAPA NCHINI TANZANIA

Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa akifungua mkutano mkuu maalum wa UTPC, unaofanyika Jijini Dar es salaam 


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam 


SERIKALI imewataka waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri kwa kuandika habari zenye weledi zitakazovutia wawekezaji kuja nchini kuwekeza na kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi ikiwemo Waandishi wa habari. 


Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akifungua mkutano Mkuu Maalum wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Disemba 6,2022 jijini Dar es Salaam. 


"Najua vyombo vingi vya habari havilipi mishahara hivyo tunatakiwa sisi tujenge mazingira mazuri ambayo yatavutia wawekezaji kuja kuanzisha vyombo vikubwa vya habari na kuajiri wenzetu. Takwimu  zinaonesha kila mwaka kuna waandishi wa habari 1000 wanazalishwa nchini, hawa wote wanaenda wapi?," alihoji Msigwa

Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi UTPC wakiwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC jijini Dar es Salaam leo Disemba 6,2022

Amesema vijana waelezwe kuwa uandishi wa habari siyo rahisi ni taaluma inayohitaji mtu kukaa darasani na bila kufanya hivyo tutabakiwa na waandishi wajanja wajanja wasio na uwezo wa kutumia kalamu zao kubainisha fursa za kiuwekezaji katika mikoa yao. 


"Hii haiwezi kuwa kazi rahisi sana sababu tunapigania haki za watu, tunatetea wanyonge na tunatangaza maendeleo, kwa hiyo waelezeni hii ni kazi ngumu na hata kupata maslahi yake ni ngumu." amesisitiza Msigwa. 


Ameongeza kwa kusema kuwa "Moja ya changamoto tulizokuwa nazo ni hali ya uchumi, wadau wa maendeleo tunaomba mtusaidie kutukwamua tulipo ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri na  kufanya hivyo sio kuwa omba omba, tunataka tubadilike. "


Aidha Msigwa ametoa wito kwa Serikali za Mkoa kuchangia Klabu za waandishi wa habari kwa kuwa wamekuwa nguzo kubwa ya kuhamasisha maendeleo ya Mkoa husika kwa kuhabarisha umma kwenye karibu mambo yote yanayoendelea katika Mkoa husika.


Pia amewataka waandishi wa habari kufanya kazi zao bila woga wowote lakini kwa kufuata misingi na weledi bila kuvunja sheria za nchi yetu Tanzania. 


Hata hivyo Msigwa amevipongeza vyombo vya habari siku za karibuni kuanza kuandika habari kwa weledi bila kufuata taarifa  potofu ambazo zimekuwa zikiandikwa mitandaoni na  ambazo hazijafanyiwa uchunguzi.


Kuhusu sheria ambazo sio rafiki, Msigwa amesema tayari taratibu mbalimbali za kufanyia mabadiliko hayo zimefanyika na hivi karibuni sheria hiyo itafikishwa bungeni kwaajili ya kufanyiwa mabadiliko.

Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Keneth Simbaya akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC leo tarehe 6 Disemba, 2022.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo amesema Mkutano Mkuu maalum huo unalengo la kufanya mabadiliko katika mfumo mzima wa UTPC na kuitoa kutoka kuwa bora na kuwa bora zaidi (Moving UTPC from Good to Great) ikiwemo kuhamisha makao makuu yake kutoka Mwanza  kwenda Dodoma.

Akitoa salamu za mashirika ambayo ni marafiki wa UTPC, Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa, amewataka waandishi wa habari kuungana na kusema kuwa siku zote hakuna jambo la muhimu kama usalama wa mwandishi wa habari kwanza.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC wakiwa ukumbini wakiendelea na Mkutano Mkuu huo jijini Dar es Salaam leo Disemba 6, 2022. 

" Nawaomba ndugu zangu, tuungane ili kuhakikisha sheria iliyopo inabadilishwa kwaajili ya maslahi mapana ya waandishi wa habari, hakuna jambo muhimu zaidi ya usalama wa Mwandishi kwanza," amesema Ngurumwa. 


Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya amesema mabadiliko yanayoenda kufanyika yanahitaji utayari wa viongozi wote wa klabu za Waandishi wa habari nchini Tanzania, kwa kufanya hivyo wafadhili wataendelea kuipatia fedha UTPC na kuifanya kuwa imara zaidi.

Pichani waliokaa mbele ni Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi UTPC wakiwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC jijini Dar es Salaam leo Disemba 6,2022

Post a Comment

0 Comments