Na Urban Epimark - MOROGORO
Maafisa Mipango wa Halmashauri pamoja na Sekretarieti za Mikoa Nchini wametakiwa kuandaa mazingira mazuri na wezeshi ya uwekezaji katika Mamlaka zao za Serikali za Mitaa Nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi Februari 02, 2023 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Grace Magembe kwaniaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Bi. Angellah Kairuki katika hafla ya kufunga Mafunzo juu ya Uandishi wa Maandiko ya Miradi ya kibiashara ambayo yataziwezesha Halmashauri hapa nchini kufungua Makampuni ya kiuwekezaji kibiashara iliyofanyika kwa siku kumi katika Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Magembe amewatata washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema ujuzi walioupata kwenye mafunzo hayo kuandaa mazingira mazuri na wezeshi yatakayo vutia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza katika Halmashauri zetu na kusema,
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa za kuifungua nchi yetu kiuwekezaji kwa kujenga mazingira mazuri yanayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu , hivyo ndugu zangu Maafisa Mipango kupitia ujuzi mlioupata nendeni mkaweke mazingira wezeshi katika Halmashauri zetu kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika Halmashauri zenu kwa kufungua Makampuni” alisema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe amekipongeza Chuo cha Mipango pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuandaa mafunzo hayo yenye tija kwani yamejumuisha nadharia na vitendo kitu kilichowezesha washiriki kuibuka na maandiko chanya ya kibiashara.
“Naomba niwapongeze na kuwashukuru sana Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuandaa na kuendesha vyema mafunzo haya yenye tija ” aliongeza Dkt. Magembe.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya amesema mafunzo hayo elekezi yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yametoa jumla ya maandiko kumi na tatu (13) ya kibiashara ambayo yataziwezesha Halmashauri kuyawasilisha kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata Mikopo ya kuanzisha Makampuni (SPV).
Nae Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Emmanuel Nnko akizungumza kwa njia ya mtandao amekishukuru Chuo cha Mipango kwa utafiti ambao ulibainisha changamoto ya ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya mapato katika Halmashauri nchini na hivyo kuandaa mafunzo haya.
Vile vile ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ushirikiano inaotoa kwa taasisi hizi mbili na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutatua changamoto za maendeleo ikiwemo kusaidia upatikanaji wa vyanzo vya mapato katika Halmashauri Nchini.
Aidha; aimeiomba Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuipa kipaombele miongozo ya uwekezaji iliyopo katika kila Mkoa.
Mwisho.
0 Comments