TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MKUU MPYA WA WILAYA YA CHATO KUANZISHA MPANGO WA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Mkuu Mpya wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale. 

Salum Maige,Chato. 

Mkuu mpya wa wilaya ya Chato mkoani Geita Deusdedith Katwale ametaja mikakati yake ya kukuza uchumi wa wananchi wa Chato utakaochochea kuongezeka  ajira kwa vijana kwa kutumia rasilimali zinazopatikana wilayani humo.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia rasilimali ya Ziwa Victoria na Ardhi iliyopo yenye rutuba kwa kulima mazao ya biashara na chakula kama vile mpunga,mahindi,pamba na mboga mboga ambayo yatauzwa ndani na nje ya nchi. 

Katwale ametaja mikakati hiyo alipokutana na wazee wa wilaya ya Chato baada ya kumkaribisha wilayani humo sambamba na kutoa pongezi kwa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu  Hassan kumteua Katwale ambaye ni Mzaliwa wa Chato.

Akizungumza na wazee hao mjini Chato Katwale leo February 2,2023 amesema Chato itakuwa wilaya ya Mfano kwa uzalishaji wa Chakula nchini ambapo badala ya wananchi kutegemea mvua kuendesha kilimo watalima kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria.

Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale akisalimia na Mwenyekiti wa baraza la wazee wilaya ya Chato Mzee Elias Makoli alipowasili katika ukumbi wa Mshikamano mjini Chato kuzungumza na wazee wa wilaya hiyo.

"Sitarajii kuona wilaya ya Chato tunaomba chakula,tutalima mazao kwa wingi na kutumia uwanja wa ndege wa Chato na Stendi ya mabasi na barabara zetu kusafirisha mazao haya ndani na nje ya nchi,tutatumia mabonde tuliyonayo kulima mpunga,mboga mboga,hii itasaidia kuchochea uchumi wa Chato"alisema Katwale.

Aidha,aliwaomba wazee hao kumsaidia kutunza amani katika wilaya hiyo ili aweze kupata muda wa kukimbia sehemu mbalimbali kuhakikisha mipango hiyo ya kilimo cha kisasa inakamilika huku akiwaonya watumishi wenye nia ya kumkwamisha.

"Mimi kama mtumishi wenu,ndugu yenu wazee wangu tukifanikiwa hili tutapunguza tatizo la ajira  kwa vijana wetu na sekta hii itatioa ajira nyingi kwa kundi hili na Chato itakuwa ya mfano,hivyo wazee wangu naomebni sana ushirikiano wenu ili tuweze kufanikisha mpango huu."alisema DC Katwale.

Wazee wa wilaya ya Chato wakiwa katika Ukumbi wa Mshikamano mjini Chato wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Deusdedith Katwale alipokuna nao kuzungumzia mustakabali wa maendeleo ya Chato siku chache baada ya kuapishwa na mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela

Katwale ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Katende umbali wa kilomita tano kufika mjini Chato amehitimu elimu ya msingi kijijini hapo kabla ya mwaka 1995 alipojiunga na shule ya sekondari Kaholoro,na mwaka 2008 amewahi kuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana mkoa wa Kagera wakati huo huo Chato ikiwa wilaya ya mkoa huo.

Alisema kabla ya kuteuliwa na Rais  kuwa mkuu wa wilaya hiyo alikuwa mtumishi wa serikali kwenye ofisi ya Makamu wa Rais kama mhandisi na hivyo kuteuliwa kwake  kuongoza Chato si kwa kubahatisha kwa sababu anaijua Chato.

Awali Mwenyekiti wa baraza la Wazee wilaya ya Chato Elias Makoli alisema Rais hajakosea kumteua kwenda Chato kutokana na Uzoefu aliona wa Kazi.

"Leo Mheshimiwa mkuu wilaya tunampongeza sana Rais kukuteua kuja wilayani Kwetu,tunakukaribisha sana nyumbani wewe ni kijana wetu Chato unaifahamu utaiendeleza ,leo ilikuwa siku ya kukukaribisha tu,kuna siku tutakutana kukueleza changamoto zetu zikiwemo za Afya."

Wazee wa wilaya ya Chato wakiwa katika Ukumbi wa Mshikamano mjini Chato wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Deusdedith Katwale alipokuna nao kuzungumzia mustakabali wa maendeleo ya Chato siku chache baada ya kuapishwa na mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela. 

 Diwani wa Kata ya Chato Mange Ludomya alisema hana wasiwasi na uongozi wa mkuu huyo wa wilaya na  kuteuliwa kwake ni mwarobaini wa Chato kusongambele kupitia miradi ya maendeleo kutokana na kwamba Katwale ni mwenyeji wa wilaya hiyo.

Alisema hakuna mradi uliosimama hadi sasa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato,stendi ya Magufuli Chato na uwanja wa ndege na kwamba safari za ndege katika uwanja huo zinatarajiwa kuongezeka kutoka mbili kwa wiki hadi tatu.

mwisho.

Post a Comment

0 Comments