Na Urban Epimark, GEITA.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi-CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolaus Kasendamila ametoa wito kwa muwekezaji wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) kusaidia kuubadilisha mkoa wa Geita kimaendeleo ili uwe tofauti na mikoa mingine kutokana na matokeo ya utajiri wa madini ya dhahabu yaliyopo mkoani humo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolaus Kasendamila akitoa nasaha zake wakati wa mkutano wa utiaji saini pesa za CSR mjini Geita mapema leo 21 Machi 2023. |
GGML ni kampuni tanzu ya Anglo Gold Ashanti iliyowekeza nchini tangu mwaka 2000 inayo miliki mgodi wa dhahabu wa Geita, inachangia takribani asilimia 40% ya pato la taifa litokanalo na sekta ya madini nchini, pia GGML imeajiri watumishi zaidi ya elfu 6 ambapo asilimia 90% ya watumishi hao ni watanzania.
Leo Machi 21, 2023 mjini Geita muwekezaji huyo amesaini makubaliano na serikali ya mkoa wa Geita ya utekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamiii yaani "Corporate Social Responsibility- CSR" ambapo halmashauri tano za mkoa huo zitanufaika na fedha hizo ili kuwezesha kuboresha miundo mbinu mbalimbali ya kijamii mkoani humo.
"Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunampongeza sana muwekezaji wetu ambae ni GGML. Ukweli sisi sote tunaona mchango wake katika ulipaji kodi serikalini na pia katika kuusaidia mkoa wetu wa Geita ili ubadilike kimaendeleo na kujitofautisha na mikoa mingine isiyo kuwa na utajiri wa dhahabu kama wetu" alisema Mwenyekiti huyo.
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela (katikati) akishuhudia utiaji saini makubaliano ya pesa za CSR kutoka GGML kiasi cha shilingi bil.19 mjini Geita leo Machi 21, 2023 |
Nae mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela amezitaka mamlaka za utekelezaji katika mkoa wa Geita ambazo ni halmashauri ya mji wa Geita, Geita DC, Mbogwe, Chato na Bukombe kuzitumia vizuri pesa hizo za CSR zitakazo tolewa na muwekezaji huyo.
Halikadhalika Mhe Shigela ameagiza mamlaka hizo kuhakikisha wakandarasi wa kumalizia na wale wa kuanza miradi mipya kwenye Halmashauri hizo, waandaliwe mapema hadi kufikia mwishoni mwezi aprili wote wawe kwenye maeneo yao ya miradi na mwezi mei mwaka huu atafanya ziara ya kukagua miradi hiyo na maendeleo yake, alisisitiza.
Awali makamu wa rais wa kampuni hiyo ya Anglo Gold Ashanti inayo miliki mgodi wa GGML Bw. Simon Shayo katika taarifa yake alisema,
"GGML imedhamiria uwepo wake hapa nchini na hususan katika mkoa wa Geita, utafsiriwe katika maendeleo ya watu kutokana na mrejesho wa pato linalo patikana kutoka katika mgodi huo" alisema.
Katika makubaliano hayo ya pesa za CSR kiasi cha shilingi bilioni 19 zimetolewa kwa miaka miwili, halmashauri ya mji wa Geita itapata bilioni 9.8, Geita DC bilioni 8.6, Chato milioni 200, Mbogwe milioni 200 na Busada milioni 200/=.
Mwisho.
0 Comments