Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kardinali Pengo akipokelewa uwanja wa ndege. |
Na Mwandishi wetu, Geita.
Jimbo Katoliki la Geita, kesho jumamosi March 18, 2023 linategemea kulitabaruku upya kanisa kuu la jimbo la Geita ambalo lilifanyiwa kufuru na kunajisiwa mwezi uliopita, wageni mbalimbali tayari wameanza kuwasili mjini humo huku Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kardinali Pengo ambae ndie ataongoza Ibada ya tukio hilo akishirikiana na Rais wa TEC Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga na maaskofu wengine tayari amewasili mjini humo jana jioni.
Ratiba iliyotolewa mapema jana na ofisi ya Askofu wa Jimbo la Geita, inaonesha baadhi ya wageni watakaoshiriki kwenye tukio hilo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ambae ataiwakilisha serikali katika tukio hilo akiambatana na kamati ya haki na amani ya mkoa wa Geita.
Wakati huo huo Rais wa TEC ambae pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga ataongoza adhimisho la misa takatifu, parokia ya Bikira Maria wa Fatima Geita siku ya Jumapili March 19, 2023 kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 12 tangu ateuliwe kuwa Askofu mwaka 2011.
Taarifa iliyotolewa na Padre Gerald Singu, ambae ndie Paroko wa Kanisa la Bikira Maria wa Fatuma jimboni Geita imesema, katika adhimisho hilo Askofu Mkuu Nyaisonga ataongoza Harambee ya kuchangia ujenzi wa Kigango cha Nyamalembo kilichopo chini ya parokia hiyo.
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwa tayari kulitabaruku upya kanisa kuu la jimbo la Geita kesho 18 Machi 2023. |
Mwisho.
0 Comments