Mwalimu wa darasa la awali na la kwanza akiwaongoza Wanafunzi kunawa mikono. |
Na Salum Maige, Geita.
Ikiwa ni mwezi wa pili sasa tangu Muhula wa kwanza wa Masomo uanze wa mwaka 2023 Mkoa wa Geita umefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali baada ya serikali kuongeza muda wa zoezi la uandikishaji hadi Machi 31,mwaka huu.
Hadi siku ya pili ya muhula wa masomo kuanza mwaka huu mkoa wa Geita ulikuwa haujafikia lengo la kuandikisha wanafunzi 168,480 baada ya kuwa umeandikisha wanafunzi 137,371 sawa na asilimia 82.75%.
Katika idadi hiyo wanafunzi wa awali waliokuwa wameandikishwa hadi kufikia Disemba 31,mwaka jana 2022 ili kuanza masomo mwaka huu wa 2023 ni wanafunzi 55,875 wa darasa la awali huku wa darasa la kwanza waliokuwa wameandikishwa ni wanafunzi 83,514.
Kwa mujibu wa Afisa elimu mkoa wa Geita Antony Mtweve ni kwamba mkoa wa Geita umevuka lengo la kuandikisha wanafunzi 168,480 ambapo hadi kufika Februari 28,mwaka huu mkoa huo umefanikiwa kuandikisha wanafunzi 189,966.
Walimu wa awali na la kwanza wakifurahia na wanafunzi wao. |
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, Mtweve amesema katika uandikishaji huo wanafunzi wa darasa la awali lengo ilikuwa ni kuandikisha wanafunzi 66,205 lakini hadi kufikia Februari 28 walioandikishwa ni watoto 75,053 sawa na asilimia 113.36.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na zoezi la uandikishaji kuanza mapema Disemba mwaka jana uwepo wa uhamasishaji kuanzia ngazi ya jamii ,viongozi wa vijiji, mitaa, kata na wilaya, elimu bila ada na kuanzishwa kwa shule mpya.
“Mafanikio haya yametokana na uhamasishaji..kuanza kwa zoezi mapema ,hata hivyo tunatarajia kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa madarasa hayo kutokana na zoezi la kuwaandikisha kuongezwa hadi machi 31,mwaka huu”anasema Mtweve.
Miongoni mwawanafunzi hao wenye mahitaji maalumu walioandikishwa kuanza darasa la kwaza mwaka huu ni watoto 353 wavulana ni 205 na wasichana ni 148,huku wanafunzi wa awali wakiwa wameandikishwa 200 wavulana 114 na waschana 86.
Wanafunzi wa darasa la Kwanza wakiwa ndani ya darasa. |
Wakati mkoa huo ukifanikisha kuvuka lengo la uandikishaji ,wanafunzi wa madarasa ya awali na la kwanza unakabiliwa na uhaba wa walimu wenye taaluma ya kufundisha wanafunzi wa darasa la awali na badala yake imekuwa ikiwatumia walimu waliopo kufundisha kwenye madarasa hayo baada ya kuwapatia mafunzo maalum.
Akizungumzia walimu wa awali,Bila kutaja idadi ya walimu waliopo asliema serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu walipo kwa ajili kufundisha awali,na kwamba serikali imekuwa ikitoa mafunzo ili kuwa mahili na uwezo wa kufundisha watoto hao.
Akizungumzia kuhusu miundombinu Mtweve anasema,miundombinu iliyopo haiendani na idadi ya wanafunzi ingawa amewatoa wasiwasi wazazi kuwa serikali inakusudia kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Msingi Kukuluma Lusori Manyama amesema katika shule yake wanafunzi walioandikishwa ni 163 wa darasa la kwanza na Awali hadi kufikia Februari 28,mwaka huu.
Amefafanua kuwa, wanafunzi wa darasa la kwanza ni 112 wavulana wakiwa 51 na waschana 61 huku wale wa darasa la awali ni 51 wavulana 31 na wasichana 20.
Manyama amefafanua kuwa kuna changamoto ya walimu wa Awali na la kwanza shuleni kwake na kwamba mwalimu wa darasa la awali analazimika kuingia darasa la kwanza kufundisha masomo yote kwa kufuata KKK(kusoma,Kuandika na Kuhesabu).
“Hivyo basi tunaiomba serikali kuajili walimu wa madarasa hayo ili kuwa na msingi imara wa elimu nchini ili kuongeza kiwango cha elimu nchini ,kwani serikali imekuwa ikitumia nguvu kubwa kwa madarasa ya juu na kusahau kwenye msingi wa elimu”anasema Manyama.
Katika Kongamano la Kujadili elimu lililofanyika kwenye shule ya waschana Nyankumbu,Afisa elimu Taaluma mkoa wa Geita Mustapha Mujibu amesema mkoa wa Geita una jumla ya shule za msingi 763 katio yake za binafsi zikiwa shule 693.
Aidha amefafanua kuwa mkoa huo una walimu 9,105 upungufu ukiwa walimu 8,511 na kwamba kutokana na upungufu huo uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 86 uwioano ambo umepungua kutoka uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 89.
“Hii inatokana na ajila za walimu zilizotolewa na serikali mwaka jana hali hii imetufanya mkoa sasa kuwa na uwioano huo ambapo walau umepunguza kiasi”anasema Mujibu.
Kwa mujibu wa Programu ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto(PJT-MMMAM) ni kwamba katika mwaka 2018 Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia iliripoti upungufu wa asilimia 31.7 ya walimu wa aelimu ya awali wenye vigezo vya kufundisha wanafunzi wa awali.
Katika taarifa hiyo ni kwamba kwa mwaka 2017 walimu wa awali walikuwa 5,367 na hadi kufika mwaka 2018 idadi iliongezeka na kufika walimu 7,86.
Wanafunzi wa Darasa la Awali na la kwanza wakiwa pamoja. |
Aidha,idadi hiyo inasababisha kuwa na uwiano wa wanafunzi na walimu katika mkondo wa elimu ya awali ya shule za serikali iliripotiwa kuwa ni mwalimu mmoja kfundisha wanafunzi 249 kinyume na mwongozo wa wa kisera wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 25.
Mwisho.
0 Comments