TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

RC GEITA KUWA MGENI RASMI KATIKA UZINDUZI WA CHAMA CHA MICHEZO YA JADI MKOA WA GEITA

Dunia Mrisho (Mwenyekiti wa Chama Cha michezo ya jadi Mkoa wa Geita- CHAMIJATA).

 Na  Alphonce  Kabilondo,Geita.

 CHAMA  cha michezo ya jadi  Tanzania  (CHAMIJATA ) Mkoa wa Geita kinatarajia kufanya uzinduzi rasimi wa chama hicho  Mkoani hapa kwa kushirikisha washiriki wa  michezo  mbalimbali ya jadi kutoka wilaya tano za  mkoani hapa .

Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita Bw. Dunia Mrisho amesema kuwa uzinduzi rasimi wa chama hicho utafanyika  aprili15 mwaka huu ambapo mgeni rasmi ana tarajiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela .

Alisema kuwa  baada ya uzinduzi wa chama hicho yatafanyika mashindano ya michezo ya kijadi kutafuta mshindi mmoja kwa kila mchezo atakae kwenda kuuwakilisha mkoa wa Geita kwenye mashindano ya kitaifa ya michezo ya kijadi yanayotarajiwa kufanyika kitaifa jijini Dodoma  mwezi oktoba mwaka huu 2023.

Bw.Mrisho alisema kuwa  uzinduzi huo  utapambwa  na michezo mbalimbali ya kijadi pamoja  na mbio za baiskeli zitakazo anzia mjini Geita  kuelekea kijiji cha Igaga kinachotenganisha  wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza na wilaya ya   Geita mkoani hapa , washiriki wa mbio za baiskeli zaidi ya 10  wameshathibitisha kushiriki mbio hizo.

 Akizungumzia zawadi kwa washiriki wa mbio hizo alisema kuwa mshindi wa kwanza  atajinyakulia kitita cha shilingi elfu sabini  (Tsh 70,000/= ) mshindi wa pili kitita cha  elfu shilingi hamsini  (Tsh 50,000/=)  na  mshindi wa tatu ataibuka na kitita cha shilingi elfu thelathini (Tsh 30,000/=) .

Aidha alisema  kuwa  maandalizi  ya  uzinduzi wa chama hicho  yamekamilika ,pia  mbali na mashindano ya mbio za baiskeli  kutakuwa na michezo mingine mingi ya jadi zikiwemo ngoma za  asili za makabila mbalimbali, karata, kufukuza kuku , kuvuta kamba  pamoja na kurusha mkuki, kukimbia kwenye gunia,  dama ,mpira wa aina yake utakao chezwa kwa kutumia vijwa pekee .

“Chama hiki kina mwaka mmoja toka tumekipokea mkoa wa Geita lakini kimesajiliwa hapa nchini tangu mwaka 1976  kilikuwa kimefifia  lakini Mhe. Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan  amekifufua  baada ya kukutana na viongozi wa jadi (Machifu) wa mikoa baadhi ya Tanzania  lengo kuu  likiwa ni kudumisha tamaduni chanya   pamoja na  kuachana na tamaduni za kigeni", alisema Mrisho .

Omary Shaban (Katibu wa chama cha michezo ya jadi Mkoa wa Geita -CHAMIJATA).

Katibu mkuu wa chama hicho mkoa wa Geita Bw. Omary Shaban alifafanua kuwa hafla ya uzinduzi wa chama hicho utafanyika eneo la uwanja wa wazi  maarufu  Lukirini mtaa wa mkoani mjini Geita aprili 15, 2023.

Shaban  alisema kuwa hayati  mwalimu Julius  Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa akiipenda michezo ya kijadi hivyo  jamii haina budi kumuenzi kwa kuibua michezo  hiyo .

 Katibu  huyo aliongeza kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kuna michezo ya jadi zaidi ya 17, pia   chama  hicho (CHAMIJATA) kinakusudia  kuwarejesha  vijana wa  kitanzania kutoka kwenye  tamaduni za kigeni huku akitumia fursa hiyo kuwataka wapenzi na mashabiki wa michezo ya jadi kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo ya uzinduzi rasmi wa Chama cha michezo ya jadi Tanzania kwa mkoa wa Geita. 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments