TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WANAWAKE WATAKIWA KUWANIA UENYEKITI SERIKALI ZA MITAA NA VIJIJI 2024

Pichani katikati ni Hellen Mbogohe (
Mjumbe wa baraza kuu umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT taifa) akikata utepe ishara ya kufungua nyumba ya Katibu wa umoja wa wanawake UWT wilaya ya Geita, kushoto kwake ni Mary Mazura (Mjumbe wa Mkutano mkuu CCM taifa) akifuatiwa na Pauline Alex (Mwenyekiti wa UWT CCM Wilaya ya Geita) wakishuhudia zoezi hilo. 

Na Alphonce Kabilondo,Geita

 Mjumbe wa baraza kuu umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi CCM (UWT) Taifa Helen Mbogohe amewataka wanawake kujiandaa kugombea nafasi za uongozi wa uenyekiti wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unaotarajiwa kufanyika Nchini mwaka 2024 .

Mbogohe ametoa kauli hiyo jana kwenye hafla ya ufunguzi wa nyumba ya katibu wa umoja wa wanawake chama cha mapinduzi CCM (UWT) Wilayani Geita Mkoani hapa iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 20.

Alisema kuwa wana CCM hawanabudi kuanza kuangalia viongozi waadilifu watakao chaguliwa kuongoza nafasi hizo ili uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 chama kisiwe na kazi kubwa.

Pia aliwataka wanawake wa umoja huo Nchini kuhakikisha mgombea Urais wa chama hicho Dkt Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 anashinda kwa kishindo kwa kuwa ndiye mgombea pekee wa chama hicho .

 “Nimekuja leo hapa Geita kwa kazi ya kufungua nyumba ya katibu wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Geita lakini lazima niseme ukweli 2025 CCM hatuna mgombea Urais tofauti na Dkt Samia, wana CCM tuanze kuangalia wanachama wenye uwezo wa kuongoza serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kwakuwa ngazi hiyo ndiyo msingi" alisema Mbogohe .

Akizungumzia mmomonyoko wa maadili nchini alisema kuwa wanawake wanapaswa kuwa wakali na kukemea watoto kujihusisha na vitendo viovu sambamba na kutimiza jukumu la kukaa na watoto badala ya jukumu hilo kuwaachiwa dada wa kazi.

Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Geita Komredi Manjale Magambo akitoa salamu za vijana kwenye hafla ya ufunguzi nyumba ya Katibu wa UWT wilaya ya Geita iliyojengwa kwa michango ya wanachama na wadau wa CCM. 

Aidha kufuatia uwepo wa wimbi la matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani hapa mwenyekiti wa umoja wa vijana (UVCCM) Mkoa wa Geita Komredi Manjale Magambo akitoa salaam za vijana wa mkoa huo alionyesha kusikitishwa na matukio ya vitendo vya ukatili na hivyo kuwaomba wanawake kurudi kwenye misingi ya malezi kwa watoto.

Manjale alisema kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakitokea kila kukicha dhidi ya wanawake na watoto , wanawake kuuawa kikatili na watoto kupigwa na kuchomwa na vitu vyenye ncha kali.

“Akina mama ninyi ndiyo walezi wetu mnaweza kutusaidia kunusuru hali hii,  vijana tunaweza kukengeuka tukajikuta tunaingia kwenye wimbi hili la ukatili lakini ninyi ndio mnaweza kutunusuru kutoka kwenye hali hii.
Geita sasa nitishio matukio 6 ya ukatili kwa kipindi hiki tu cha robo ya kwanza ya mwaka" alisema komredi Manjale.

Pichani katikati ni Hellen Mbogohe (
Mjumbe wa baraza kuu umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT taifa) akimkabidhi hati ya pongezi Titus Kabua mjumbe wa kamati ya siasa CCM Wilaya ya Geita kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha ujenzi wa nyumba hiyo. 


Titus Kabua mjumbe wa kamati ya siasa Wilaya ya Geita alisema kuwa wazazi na walezi wanalo jukumu kubwa la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili hasa kwa watoto.

“Mmomonyoko huu wa maadili pia unachangiwa na sisi wazazi na walezi kutotimiza wajibu wetu na kutowakemea watoto wetu kufanya matendo maovu hivyo kuna kila sababu ya kuwajengea watoto kuwa na hofu ya Mungu" alisema Kabua .

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Geita Paulina Alex alitumia fursa hiyo kuliomba jeshi la polisi Mkoani hapa kufanya uchunguzi wa kina na kuwabaini wanaofanya matukio hayo ya kikatili na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kwani kila kukicha wanawake na watoto wanafanyiwa ukatili" alisema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Geita Paulina Alex (mwenye kipaza sauti) akitoa neno kwenye hafla hiyo ya kufungua nyumba. 

Hata hivyo hivi karibuni kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita ACP Safia Jongo akizungumza na waandishi Mkoani hapa wakati akitolea ufafanuzi wa matukio ya ukatili alisema kuwa matukio hayo yana changiwa na wivu wa kimapenzi pamoja na wazazi na walezi kutotimiza wajibu wao wa kukaa na kuwafunda watoto wao hali inayochangia mmomonyoko wa maadili hivyo kunahaja ya kushirikiana na viongozi wa madhehebu ya dini kuwa elimisha waumini wao pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kupinga ukatili huo .

Kamnda wa jeshi la polisi Mkoa wa Geita ACP  Safia Jongo


 Mwisho.  

Post a Comment

0 Comments