TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

"WARATIBU ZINGATIENI MAFUNZO YANAYOTOLEWA NA UTPC":NSOKOLO, RAIS WA UTPC

Deogratius Nsokolo rais wa UTPC wakati akifungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji waratibu wa klabu za waandishi wa habari (kushoto) na pembeni yake ni Kenneth Simbaya mkurugenzi mtendaji wa UTPC (alieketi) 

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam. 

Waratibu wa klabu za waandishi wa habari Tanzania wametakiwa kuzingatia na kutumia ujuzi wanaoupata katika mafunzo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa kiunganishi bora cha utendaji kati ya klabu hizo na  muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania( UTPC)na kufikia malengo ya  mkakati mpya wa UTPC wenye kauli mbiu ya "Moving UTPC from Good to Great".

Hayo yamesemwa na Rais wa muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa  waratibu wa klabu za waandishi wa habari Tanzania leo jijini Dar es salaam.

Rais wa muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Deogratius Nsokolo aliyesimama akitoa neno la ufunguzi kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa yote Tanzania. 

Nsokolo  amesema kuwa uimara wa klabu za  waandishi wa habari ndio utakao imarisha pia UTPC ambapo itaweza kutekeleza mpango kazi mpya wa miaka mitatu kwa mafanikio makubwa kuanzia 2023 hadi 2025.

"Waratibu ni wakurugenzi wa klabu za waandishi wa habari huko, kama ilivyo kwa mkurugenzi wa UTPC, hamkuajiriwa kwa bahati mbaya ni vyema kutumia vizuri nafasi na ujuzi ulionao ili kuleta mabadiliko chanya kwenye klabu huko kwa kuzingatia mambo yafuatayo ubunifu, uadilifu, nidhamu na kutunza siri za ofisi" amesema Deogratius Nsokolo. 

Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya akiwasisitiza waratibu kuzingatia mafunzo haya mara baada ya rais wa UTPC kutoa neno la ufunguzi leo april 18, 2023

Kwa upande wake mkurugenzi  mtendaji wa muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Kenneth  Simbaya amesema safari ya mabadiliko ya UTPC kutoka kwenye hali bora kuenda hali bora zaidi inahitaji ushirikiano wa hali ya juu.

"Naomba wote mshiriki mafunzo haya kwa manufaa, na kuhakikisha wote tunanufaika nayo kwa taasisi na kwa maisha binafsi, ni vema tuwe katika darasa na kusikiliza kwa umakini" amesema Simbaya. 

Amesema mafunzo hayo ni mwanzo wa mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa UTPC kutoka ilipokuwa  awali na kuifanya kuwa taasisi bora zaidi.

Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo (alieketi kushoto) na mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya (aliyeketi kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na waratibu wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Jamirex hotel Dar es Salaam leo 18 aprili 2023. 

Jumla ya waratibu 26 kati ya 28 sawa na mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani wanashiriki mafunzo hayo ambayo lengo lake kuu ni kuwajengea uwezo waratibu wa kiutendaji kwenye klabu zao, na hao waratibu 2 ambao hawakuhudhuria kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao watatafutiwa na UTPC namna flani kuhakikisha nao pia wamefundishwa.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments