Na Alphonce Kabilondo,Geita.
KAMPUNI ya uuzaji wa vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini, mitambo na magari makubwa GF Trucks & Equipment imewashauri wachimbaji madini wadogo na wakati mkoani Geita pamoja na mikoa jirani ya kanda ya ziwa kuunda vikundi ili waweze kukopeshwa vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini na mitambo.
Mkurugenzi wa biashara na masoko wa kampuni hiyo Salman Karmali ametoa ushauri huo jana mjini hapa kwenye hafla ya ufunguzi wa ofisi mpya ya kampuni hiyo iliyofunguliwa soko kuu la dhahabu mkoani hapa.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa kampuni hiyo imeamua kuingia ubia na taasisi za kifedha ili kuwasaidia mikopo ya vifaa vya kisasa na mitambo ya uchimbji madini kwa wachimbaji wadogo na wakati hivyo wachimbaji wadogo na wakati hawana budi kuunda vikundi vya uchimbaji ili waweze kukopesheka.
Alisema kuwa lengo la kampuni hiyo kufungua ofisi mkoani Geita ni kusogeza huduma kwa wachimbaji wadogo hasa wa mkoa huu wa Geita pamoja na mikoa jirani ya kanda ya ziwa huku akiipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwenye sekta ya madini.
Aidha alisema kuwa mbali na kampuni hiyo kuwakopesha vifaa na mitambo wachimbaji wadogo kadhalika wanakodisha vifaa na mitambo kwa wachimbaji lengo likiwa ni kuwainua wa chimbaji wadogo wa madini .
Mkurugenzi wa biashara GF TRUCKS kanda ya ziwa aliyevaa T-shirt nyeupe kwenye hafla ya ufunguzi Ofisi ya kampuni hiyo mkoani Geita. |
“Tutawafikia wachimbaji wadogo wote kwenye maeneo yao ya uchimbaji na kuwapatia elimu ya matumizi ya vifaa vya kisasa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani ya kanda ya ziwa" alisema Karmali .
Awali katibu wa chama cha wachimbaji wadogo mkoa wa Geita (GEREMA) Golden Hainga akitoa kilio cha wachimbaji wadogo alisema kuwa wachimbaji wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini pamoja na mitaji na kutoaminiwa na taasisi za kifedha .
Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Geita Gold wakiwa katika furaha mdamini wao GF TRUCKS & EQUIPMENTS kufungua Ofisi mkoani Geita. |
Alisema kuwa uchimbaji madini kwa kutumia dhana duni unachangia wachimbaji wengi kupata uzalishaji mdogo wa madini angali wakitumia gharama kubwa kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini.
Katibu huyo aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuja na suluhisho kwa wachimbaji wadogo ambapo alitoa wito kwa wachimbaji wadogo mkoani humo kuchangamkia fursa ya mikopo ya vifaa na mitambo ya kisasa.
“Wachimbaji wengi mkoani Geita bado wafanya uchimbaji madini kwa kutumia dhana duni kampuni hii imekuja muda mwafaka kwa wachimbaji hususani wa mkoa wa Geita" alisema Hainga.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoani hapa GEWOMA Husina Mwasimba alisema kilio kikubwa cha wachimbaji wadogo ni ukosefu wa mitaji, vifaa vya kisasa vya uchimbaji wa madini na hivyo kuiomba kampuni hiyo kuwakopesha vifaa kwa mikopo ya masharti nafuu.
Mwisho.
0 Comments