TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MAISHA YA WANAFUNZI ZAIDI YA ELFU 6 YAKO HATARINI KWA AJALI ZA BARABARANI MJI WA KATORO GEITA

Watoto wa wanaoishi kitongoji cha Afya kata ya Ludete mji mdogo wa Katoro wakifurahia jambo wakati wazazi wao walipokutana kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya msingi ya Afya kufanya changizo la ujenzi huo watoto ni miongoni mwa wanafunzi wa shule ambazo wanafunzi wake wanakabiliwa na ajali wakienda shule (Picha na Salum Maige)

Salum Maige, Geita.

Maisha ya wanafunzi 6,973 wanaoishi katika kitongoji cha Afya kata ya Ludete mamlaka ya mji mdogo wa Katoro halmashauri ya wilaya ya Geita yako shakani kutoka kukabiliwa na ajali za barabarani mara kwa mara wakati wakivuka kwenda na kutoka shuleni.

Ajali hizo hutokea wakati wanafunzi hao wakivuka barabara inayotoka Katoro kwenda Lwamgasa wakielekea kwenye shule za msingi Ibozyamagigo, Katoro,Uhuru, Mtoni na Simbachawene, shule ambazo zipo kata jirani ya Katoro.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kitongoji cha Afya Jonathan Kazungu amesema ,katika kipindi cha kuanzia januari 2021 hadi aprili mwaka huu wa 2023 tayari wanafunzi saba wameshapatwa na majanga ya ajali za barabarani kwa kugongwa na pikipiki na gari zinazotumia barabara hiyo.

Kazungu amesema, kati ya wanafunzi hao waliopatwa na ajali mwanafunzi mmoja alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na pikipiki wakati akivuka barabara hiyo kwenda shule ya msingi Ibozyamagigo alikokuwa akisoma huku wengine sita wakijeruhiwa na kupata ulemavu.

Wanafunzi ambao wako hatarini zaidi kukumbwa na ajali hizo ni wale wanaosoma darasa la awali la kwanza na pili ambao umri wao ni katika ya miaka 4 hadi 8 ambao hawana uwezo wa kuchukua tahadhari wanapovuka barabara hiyo ambayo inamwingiliano mkubwa wa gari na pikipiki zinazoingia na kutoka katika mji wa Katoro.

Hata hivo,mwenyekiti huyo amesema kuwa, katika kukabiliana na tatizo hilo wananchi wameanzisha ujenzi wa shule mpya ya msingi ili kuwanusuru watoto wao na ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara na kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Ni watoto wa kitongoji cha Afya mji mdogo wa Katoro wakiwasikiliza wazazi hawako pichani wakati walipokutana kwa ajili kufanya harambee ya ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Afya ,watoto ni miongoni mwa wanafunzi wa shule ambazo wanafunzi wake wanakabiliwa na ajali wakienda shule.Picha na Salum Maige

“Mimi kama mwenyekiti wa kitongoji hiki ambaye ni kiongozi wa ulinzia na usalama nilianzisha mkakati wa kupata eneo la kujenga shule baada ya kupata malalamiko ya wananchi wangu kwamba watoto wao kila wakati wanapata ajali ,tulianza kulipa fidia wananchi na tukaanza ujenzi hadi sasa tumeshakamilisha maboma ya madarasa sita na matundu ya vyoo manane”anasema mwenyekiti huyo.

Ameongeza kuwa,matarajio ya wananchi ni kukamilisha ujenzi wa shule hiyo mpya ifikapo julai mwaka huu ili ianze kutumika hasa kwa wanafunzi wa awali,darasa la kwanza na la pili ambao licha ya kukabiliwa na ajali hutembea umbali mrefu kwenda shule ikilinganisha na umri wao.

Akizungumza na mwanadishi wa habari hizi mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Ibozyamagigo Lackseda Joshua wa darasa la saba amesema kuwa,amewahi kushuhudia ajali ya mwanafunzi mmoja akigongwa na pikipiki kitendo kilichoumiza moyo wake.

Ameomba wazazi wajitahidi kutoa michango ya ujenzi wa shule hiyo ili ikamilike kwa wakati kusaidia wanafunzi wadogo waweze kusoma karibu makazi yao.

“Sisi tunapokuwa tunaelekea shuleni huwa tunawavusha wale wanafunzi wa awali,la kwanza na la pili ambao ni wadogo ,huwa tunasimama tunasubiri pikipiki na gari zinapita ,baadae tunavuka,nawashukuru sana wazazi kuanzisha huu ujenzi ili kutusaidia tuje tuanze kusomea karibu”amesema Lacksadi.

Baadhi ya wazazi na walezi wa kitongoji hicho Matonange Alphonce,Neema Benedicto na Mariam Julias wamepongea hatua zilizoanza kuchukuliwa za ujenzi wa shule hiyo baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wazazi kuhusu matukio ya watoto wao kupata ajali wanapokuwa wanavuka barabara.

“Yaani huwa hatuna amani moyoni kabisa, mtoto anapokuwa ameenda shule,unakaa unawaza na kufikiria kama mtoto atarudi salama wakati mwingine hata chakula hakiliki vizuri hadi unapomuona mtoto amerejea salama nyumba ndipo moyo unatulia,tunashukuru sana hatua hii na tunaiomba serikali itushike mkono tukamilishe shule yetu”anasema Neema.

Ujenzi wa shule hiyo unaotarajia kukamilika mwaka huu na matarajio ya uongozi wa serikali na wananchi wa kitongoji cha Afya shule hiyo itaanza kutumika januari mwakani kwa kuwahamisha baadhi ya wanafunzi wa awali,la kwanza na la pili ili waanze kusoma karibu na makazi yao.

Jumla ya shilingi milioni 41.3 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo ili kuwa na watoto salama kwa kupata elimu bora na kuondokana na ajali za mara kwa mara kwa watoto waendao shuleni.

Diwani wa kata ya Ludete Sebastian Benedicto amepongeza nguvu za wananchi kukamilisha ujenzi wa maboma sita na kwama kwa nafasi yake atahakikisha sehemu ya mapato yatokanayo na huduma ya uwajibikaji kwa jamii kutoka mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) zinatumika katika kukamilisha ujenzi huo.

Aidha,mkurugenzi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro Damian Aloyce amekiri kuwepo kwa changamoto ya ajali kwa wanafunzi pamoja na ombi la wazazi la kusaidiwa kukamilisha ujenzi huo ambapo tayari halmashauri ya wilaya ya Geita imetenga shilingi milioni 100 kuunga mkono juhudi hizo za wananchi.

Kitongoji cha Afya kina idadi ya kaya 4,880 na kaya hizo zina jumla ya wanafunzi 6,973 kati yao wavulana 3,132 na wasichana 3,841 wote hao wanasoma kwenye shule zilizo ng’ambo ya barabara ya Lwamgasa ambapo wanakabiliwa na changamoto ya ajali wanapovuka barabara hiyo kwenda kutafuta elimu.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments