TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

M/K WA BARAZA LA NEEC AISHAURI GS1-TANZANIA.

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Prof. Aurelia Kamuzora (kulia) akiwa kwenye banda la maonesho la kampuni zilizo pata uwezeshaji kupitia mpango wa kusaidia viwanda wa SANVN VIWANDA SCHEME unao ratibiwa na NEEC pamoja na taasisi zingine nne za SIDO, VETA, NSSF na benki ya Azania, ambapo alipewa maelezo ya mafanikio. Kushoto ni Mkurugenzi na Mmiliki wa kiwanda cha kuzalisha vijiti vya meno (toothpicks) na vibanio vya kuchoma nyama au sticks za kuchomea mishikaki cha Bongo Toothpicks Industry cha Kisarawe, mkoani Pwani Bi Violet Oscar (kushoto mwenye kitenge). Aliipongeza kampuni hiyo ya kitanzania iliyo asisiwa na Mwanamke wa kitanzania ambapo ni kiwanda pekee kinachozalisha vijiti vya meno nchini na kuwezesha bidhaa hiyo kupatikana nchini badala ya kuagiza vijiti hivyo nchini China. Pia amekipongeza kiwanda hicho kwa kuwekea bidhaa hizo Barcode ya namba ya Tanzania kutoka GS1-Tanzania, wakati alipotembelea maonesho hayo mjini Kigoma jana Mei 26, 2023.

Na Mwandishi wetu, KIGOMA

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Prof. Aurelia Kamuzora ametoa ushauri kwa taasisi za urasimishaji shughuli za biashara nchini ikiwemo GS1-Tanzania, menejimenti zao zisaini mkataba wa mahusiano kiutendaji kazi kwa kushirikiana na Shirika la Viwango nchini TBS ili kuongeza uwajibikaji zaidi na kuimarisha ubora na thamani ya  bidhaa zinazo zalishwa nchini.

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo jana Mei 26, 2023 mjini Kigoma alipotembelea maonesho ya Sita ya Mifuko ya Program za Uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayo endelea katika viwanja vya Mwanga Community Centre na kufika kwenye meza ya  GS1-Tanzania kwenye maonesho hayo.

"Nashauri GS1-Tanzania pamoja na taasisi zingine muhimu zinazo husika moja kwa moja na kuongeza thamani kwenye bidhaa za Tanzania, menejimenti zenu  ziangalie uwezekano wa kuwa na mkataba wa kiutendaji wa kushirikiana (MoU) na TBS ili kusaidia kuongeza chachu na msisitizo wa ubora wa bidhaa zinazo zalishwa na wenye viwanda nchini wakiwemo wajasiriamali" alishauri Prof. Kamuzora . 

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Prof. Aurelia Kamuzora akisaini kitabu cha Wageni kwenye banda la Benki ya Azania lililopo kwenye viwanja vya maonesho vya Mwanga Community Centre mjini Kigoma hapo jana Mei 26, 2023 alipo tembelea maonesho ya mifuko ya Uwezeshaji yaliyo andaliwa na NEEC. Jirani kidogo kulia ni Meneja wa Benki ya Azania katika mkoa wa Geita Bi Rhoda Baluya (mwenye nywele fupi) na kushoto kidogo kwa Mwenyekiti  ni Afisa Mahusiano na Huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati wa Benki ya Azania Bw Peter Maganga.

Pia katika kutembelea shughuli za maonesho hayo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya NEEC Prof. Kamuzora alifika pia katika banda la Benki ya Azania na kuitaka benki hiyo isichoke kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati hapa nchini kwa kuwawezesha kupata mikopo ya kuendeleza biashara zao kwani serikali ina thamini sana mchango wa Benki ya Azania katika ujenzi wa uchumi nchini.

Msemaji wa Benki ya Azania katika  banda la maonesho hayo, ambae pia ni Meneja wa Benki ya Azania katika mkoa wa Geita Bi Rhoda Baluya kwa niaba ya uongozi wa benki hiyo alipokea ushauri huo na kusema Benki ya Azania haita choka na ipo tayari muda wote kuendelea  kuwahudumia watanzania.

Katika maonesho ya Sita ya mifuko ya program za uwezeshaji wananchi hapa nchini yanayo endelea mjini Kigoma katika viwanja vya Mwanga Community Centre, taasisi ya GS1-Tanzania inayo toa leseni za Barcodes kwa bidhaa za wenye viwanda nchini ilishirikiana vyema na NEEC pamoja na taasisi zingine kutoa elimu ya urasimishaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi. Katika picha Mwakilishi wa GS1-Tanzania katika maonesho hayo Bw Urban Epimark (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Kikundi cha kutengeneza mafuta ya Mawese cha Wanawake Wajasiriamali Kinazi, kutoka Kata ya Kinazi, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Bi Lisia Sluanus (kushoto) fomu ya kupata Leseni ya Barcode kwa bidhaa za kikundi hicho jana Mei 26, 2023. Mwingine kulia ni mwanachama wa kikundi hicho.

Maonesho hayo ya Sita ya mifuko ya uwezeshaji yana hitimishwa leo Mei 27, 2023 na Mgeni Rasmi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa. 

Katika maonesho ya Sita ya Mifuko ya Program za Uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayo endelea mjini Kigoma, taasisi mbalimbali zilitoa mafunzo kwenye madarasa yaliyo andaliwa ya Ujasiriamali. Katika picha ni Afisa Mahusiano na Huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati wa Benki ya Azania Bw Peter Maganga akitoa mafunzo ya aina za mikopo ya benki hiyo kwa wajasiriamali jana Mei 26, 2023. Aliye keti mbele kidogo kushoto ni Meneja wa Benki ya Azania mkoa wa Geita Bi Rhoda Baluya.

Katika picha Mwakilishi wa GS1-Tanzania katika maonesho ya Sita ya Mifuko ya Program za Uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayo endelea mjini Kigoma, jana Mei 26, 2023 alipokea maombi ya kupatiwa Leseni ya Barcode kutoka kikundi cha Nyamnyinya cha kutoka Kata ya Bukuba, Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Anaepokea fomu hiyo kushoto ni Mwenyekiti wa kikundi hicho Bi Monika Tuza na kulia ni Katibu wa kikundi hicho Bi Rhoda Peter.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments