TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SEREKALI MKOANI GEITA YAWAANDAA VIJANA KUZITUMIA FURSA ZA BOMBA LA MAFUTA.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolous Kasendamila akipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mhe Sakina Mohamed (mwenye skafu) pamoja na Vijana wa Skauti katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe iliyo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe mkoani Geita tayari kuzindua Konganano la Vijana kuzitambua na kuzitumia fursa za Bomba la Mafuta Mei 29, 2023.

Na Urban Epimark, GEITA

Serekali katika mkoa wa Geita imeandaa Kongamano maalumu la kuwaandaa vijana kuzijua na kuzitumia vyema fursa zitakazo tokana na mradi wa Bomba la Mafuta linalo jengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Pangani Tanga linalopita wilayani Mbogwe katika mkoa wa Geita.

Kongamano hilo la siku mbili lililo fanyika Mei 29 & 30, 2023 katika Mji wa Masumbwe wilayani Mbogwe liliandaliwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Sakina Mohamed (mwenye skafu na kilemba) na kuzishirikisha taasisi za urasimishaji na uwezeshaji kutoa mafunzo kwa vijana ikiwemo GS1-Tanzania.

Kongamano hilo lililo funguliwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolous Kasendamila na kufungwa hapo jana Mei 30, 2023 na Mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigela liliongozwa na Kaulimbiu "Vijana amkeni Mbogwe kuna fursa" na viongozi hao walipongeza mafunzo yaliyo tolewa na kuzishukuru taasisi zilizo shiriki kutoa mafunzo hayo.

Wenyeji wa mji wa Masumbwe wilayani Mbogwe mkoa wa Geita wakiwa katika Kongamano la Vijana lililofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe Mei 29, 2023 lililohusu kuwaanda vijana kutumia fursa. Mada mbalimbali zilitolewa na taasisi za urasimishaji na uwezeshaji zikiwe SIDO, GS1-Tanzania, VETA, NSSF, TRA, TWCC, Mradi wa Bomba la Mafuta pamoja na Halmashauri zote za mkoa wa Geita.

Mbali na GS1-Tanzania iliyofundisha umuhimu wa Barcodes kwenye bidhaa na faida zake kwa watengenezaji wakiwemo wajasiriamali na wenye viwanda, taasisi zingine zilizo toa mafunzo ni SIDO, VETA, NSSF, TRA, TWCC, Mradi wa Bomba la Mafuta pamoja na Halmashauri zote sita (6) za mkoa wa Geita.

Mwakilishi kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Bw Theophil Charles katika mada yake aliyo toa alisema,  mradi unatarajia kutangaza nafasi za ajira 120 kwa vijana walio soma masomo ya sayansi na pia kutangaza zabuni mbalimnali za ununuzi wa bidhaa na huduma, hivyo vijana wajiandae vizuri kuzitumia fursa zisije kuwapita.

Mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mhe Sakina Mohamed (kulia) akimkabidha mmoja wa Vijana wa wilaya ya Mbogwe kitabu chenye mwongozo wa milango ya mafanikio kimaisha kwa vijana ili kiwasaidie kuzielea njia za mafanikio ya kiuchumi kwa vijana wakati wa Kongamano lililo andaliwa na Mkuu huyo wa wilaya kwa siku mbili Mei 29 & 30, 2023.

Nae Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Geita Ndg Manjale Magambo alimshukuru sana Mwenyekiti wa CCM Taifa ambae pia ndie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuupendelea mkoa wa Geita na kuwaletea viongozi vijana wenye weledi, ubunifu na uchapa kazi wa hali ya juu.

Kwa niaba ya UVCCM mkoa wa Geita, Ndg Magambo amempongeza  Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mhe Sakina Mohamed ambae ni kijana pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chato, wote vijana kwa kupewa uteuzi na Rais Dkt Samia kuja kutoa mchango wao mkoani Geita.

Katika kongamano hilo mada mbalimbali zilifundishwa mojawapo ni kutoka taasisi ya GS1-Tanzania inayohusu umuhimu wa Msimbomilia au Barcode kwenye vifungashio vya bidhaa pamoja na faida zake. Katika picha Mwakilishi wa GS1-Tanzania katika kongamano hilo Bw Urban Epimark akiwasilisha mada ya Utambuzi wa bidhaa kidigitali kwa mfumo wa Barcode na QR Code yaani "Products Traceability System"

Halikadhalika Mwenyekiti huyo wa UVCCM alimtaja Mkuu wa mkoa wa Geita  Mhe Martine Shigela kwamba nae ni kijana ambae CCM wote nchini wanamfahamu kwa uchapa kazi wake na hivyo kuwataka wananchi wote wa mkoa wa Geita kutoa ushirikiano kwao ili walete maendekeo Geita kwa haraka.

Mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mhe Sakina Mohamed (kushoto) akimkaribisha kwenye kongamano hilo Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe Deusdedit Katwale (mwenye kaunda kulia) wakati wa kupokea wageni mbalimbali. Baadae wakati kutoa salamu, Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe Katwale alimpongeza DC mwenzie wa Mbogwe Mhe Sakina Mohamed kwa ubunifu mkubwa kwa vijana na hivyo amekuja kuja kujifunza kwenye kongamano hilo ili nae akaandae kwa wilaya ya Chato. Alitoa zawadi ya shilingi Milioni moja kama mtaji kwa vijana wa wilaya ya Mbogwe. Mhe Sakina Mohamed, DC wa Mbogwe yeye alimwakiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kuhakikisha vikundi vyote vya vijana wilayani humo vina patiwa usajili na kusaidiwa vikue.

Mkuu wa chuo cha ufundi cha VETA wilayani Chato mkoa wa Geita Bw Frank Kafuko (pichani) akiwasilisha mada kwa vijana jinsi Chuo cha VETA kilivyo na fursa za kuwaanda vijana kiujuzi hata kama hawana sifa za ufaulu wa kidato cha Nne, waje wasome kozi ndefu kupitia VETA wataweza kupanda kitaaluma hadi kufikia Chuo Kikuu na hivyo kuwa mahiri katika ujuzi wa kazi na kuweza kuajirika na kujiajiri pia.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolous Kasendamila (katikati kulia kwa DC Sakina Mohamed) akiwa katika picha ya pamoja na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mhe Sakina Mohamed (mwenye skafu na kilemba) pamoja na waheshimiwa wageni wa meza kuu akiwemo Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe Deusdedit Katwale (mwenye kaunda suti ya bluu) na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Geita Ndg Manjale Magambo (wa pili kutoa kushoto, au kulia kwa DC Sakima Mohamed) na nyuma walio simama ni wakufunzi wa mada mbalimbali katika kongamano hilo walio toka kwenye taasisi za SIDO, NSSF, VETA, TWCC, GS1 Tanzania, Mradi wa Bomba la Mafuta nk. Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa Ndg Kasendamila kwa niaba ya chama na serikali yake iliyopo madarakani alizishukuru kwa dhati taasisi zote zilizo acha majukumu yao na kuja wilayani Mbogwe kutoa mafunzo hayo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments