Na Urban Epimark, SINGIDA.
Serikali imetoa wito kwa jamii nzima ya kitanzania kujifunza na kujua umuhimu na faida za mdudu nyuki ili iweze kumpenda na kumtunza vyema kwa njia ya kisasa kwa faida ya jamii nzima.
Wito huo umetolewa leo Mei 19, 2023 kwenye ufunguzi wa maonesho ya kitaifa ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyo anza jana Mei 18, 2023 na kuzinduliwa leo Mei 19, 2023 na Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe Peter Serukamba ambae amewakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Singida Mjini Mhandisi Pascal Muragili.
"Serikali inapenda kutoa wito kwa jamii nzima kujifunza na kuzielewa faida na umuhimu wa mdudu nyuki katika maisha ya kila siku, ambapo husaidia kuchavusha maua ya mimea mbalimbali ya kuzalisha chakula ambapo ndicho chanzo cha uhai wa viumbe akiwemo binadamu" alisema Mgeni Rasmi.
Akiwa katika ziara ya kutundika mizinga ya kisasa kwenye shamba la msitu wa Kataraka, katika Halmashauri ya wilaya ya Itigi, wilayani Manyoni, Mkuu wa wilaya Mhandisi Pascal Muragili alisema kuanzia mwaka 2017 hadi sasa 2023 serikali imekuwa ikitekeleza mpango mkakati wa ufugaji nyuki kisasa na pamekuwa na maendeleo makubwa.
Amezitaja takwimu za vikundi vya ufugaji nyuki kisasa kuwa vimeongezeka pamoja na pato linalo ingia serikalini kupitia sekta hii na kusema mdudu nyuki ni rafiki na mdau muhimu sana katika maisha ya jamii na kiuchumi kwa ujumla.
Nae Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki hapa nchi Bw Bivoyo Deusdedit katika taarifa yake mbele ya Mgeni Rasmi wakati wa utundikaji mizinga ya nyuki ya kisasa katika kata ya Kataraka, Halmashauri ya wilaya ya Itigi, wilaya ya Manyoni amesema, serikali imepania kubadilisha mtindo wa ufugaji nyuki kienyeji na kufanya uwe wa kibiashara.
Meneja mradi wa kuendeleza ufugaji nyuki kisasa wa BEVIC Bw Martin Mgallah, mradi unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) amesema, mradi umetoa mizinga 500 kwa vikundi 10 vya ufugaji nyuki ambapo kila kikundi kimepatiwa mizinga 50.
Bw Mgallah aliendelea kufafanua kwamba, mradi wa BEVAC unatekelezwa katika mikoa mitano nchini ikiwemo mkoa wa Singida, Tabora, Shinyanga, Katavi na Pemba..
Wakati huo huo vikundi vya ufugaji nyuki katika kata ya Kataraka, Halmashauri ya wilaya ya Itigi, wilaya ya Manyoni imeiomba serikali isaidie kutatua changamoto wanazo kabiliana nazo katika ufugaji nyuki ili waweze kupata tija zaidi.
Kiongozi wa vikundi hivyo vya ufugaji nyuki Bw Meshack Amos alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka wadudu waharibifu, ukosefu wa vifaa vya urinaji, ukosefu wa mawasikiano ya simu na barabara katika maeneo wanako fugia na ukosefu wa maji.
Wameiomba serikali kuongeza kina cha bonde lililopo ili kutunza zaidi maji wakati wa kiangazi na kuongezewa mizinga 300 katika mradi wao.
Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya Mhandisi Pascal Muragili alipokea maombi hayo na kuahidi atayafikisha serikalini ili yafanyiwe kazi.
Mwisho.
0 Comments