TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SERIKALI YAGAWA PIKIPIKI KWA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII NCHINI.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu Dkt Dorothy Gwajima akiikokota moja ya pikipiki zilizo tolewa na serikali ili zitumiwe na maafisa maendeleo ya jamii nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Charles Msonde jijini Dodoma leo Mei 17, 2023

Na Mwandishi wetu, DODOMA.

Serikali imegawa jumla ya pikipiki 85 kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata 85 nchini ili kuwezesha utekekezaji wa majukumu yao.

Akikabidhi pikipiki hizo zitakazokwenda kwenye mikoa 21  Halmashauri 47 na kata 85 nchini, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inafanya jitihada kuweka mazingira wezeshi ya utendaji kazi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopo huku ikiendelea  kushughulikia changamoto ya upungufu wao.

Dkt. Gwajima amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ajira 800 za Maafisa Maendeleo ya Jamii ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa uhaba uliopo.

"Jitihada hizi zote zinazofanywa na Serikali  kwa lengo la kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi, hususan wanawake ambao katika kipindi cha nyuma walisahauliwa katika elimu na mipango ya maendeleo hivyo kuwanyima fursa ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Nchi yetu" amesema Dkt. Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu Dkt Dorothy Gwajima akikata utepe kuashirikia kukabidhi pikipiki zitakazo tumiwa na maafisa maendeleo ya jamii katika mikoa 21 nchini. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt Charles Msonde na viongozi wengine jijini Dodoma leo Mei 17, 2023.

Aidha, Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wamekuwa ni kiunganishi kikuu katika Jamii kati Wanawake na fursa za mikopo pamoja na wataalamu wa fani mbalimbali kwenye upatikanaji wa teknolojia sahihi za uzalishaji, uchakataji, masoko na vifungashio kwa Wanawake Wajasiriamali.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Amon Mpanju akieleza lengo la Wizara  kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kununua pikipiki hizo zenye thamani ya sh. milioni 314 ni kuhakikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wanaamsha na kuchechemua ari ya maendeleo, kubainisha fursa zilizopo ndani ya jamii na kuhimiza kuzitumia.

Mpanju amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa kuhimiza masuala ya maendeleo  ngazi ya msingi, kuwawezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii kurahisisha majukumu yao na kuiomba Ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya mgao kwaku zingatia mahitaji halisi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalumu Dkt Dorothy Gwajima (kushoto) akipongezwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Charles Msonde (kulia) baada ya kukabidhi pikipiki jijini Dodoma leo Mei 17, 2023

"Vigezo tulivyotumia ni kugawa pikipiki hizi kwenye mikoa yenye inayoongoza kwa vitendo vingi vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kata zilizopo pembezoni na maeneo yenye Maafis Maendeleo ya Jamii wachache zaidi" ameongeza Mpanju.

Akipokea pikipiki  hizo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amebainisha kuwa changamoto mojawapo ya Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na uhaba ni usafiri ambapo kwa juhudi za Halmashauri hadi sasa zilizopo ni pikipiki 77 pekee.

Ameongeza kwamba, anatambua juhudi za pamoja za Serikali na  mageuzi makubwa hasa mapango wa taifa wa kusimamia maendeleo  ngazi yamsingi.

"Wananchi ndio wawe kitovu cha kuleta maendeleo kwa kuibua, kupanga na kufuatilia maendeleo yao hivyo wanahitaji mageuzi mapya kifkra" amesema Dkt. Msonde.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu Dkt Dorothy Gwajima akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Charles Msonde (mwenye suti ya kijivu) pamoja na maafisa wengine akijaribu kuendesha pikipiki hizo baada ya kuzikabidhi jijini Dodoma leo Mei 17, 2023.

Dkt. Msonde amempongeza Waziri Dkt. Gwajima na Wizara anayoiongoza kwa jitihada wanazochukua  kuhakikisha pikipiki hizo 85 zinapatikana.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments