Na Urban Epimark, SINGIDA
Serikali leo Mei 21, 2023 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani iliyo ambata na na maonesho ya bidhaa za mazao ya nyuki pamoja na utoaji elimu juu ya faida za mdudu nyuki kwa ustawi wa mazingira na upatikanaji wa chakula kwa binadamu na viumbe vingine, serikali imezidua rasmi mwongozo wa utunzaji shamba la ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali.
Pia serikali imetoa maagizo kwa wakala wa usimamizi wa misitu nchini (TFS) kwa kushirikiana na wataalam wengine katika wizara ya maliasili na utalii kuandaa kwa muda wa miezi miwili mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa Asali kutoka tani elfu 33 kwa mwaka hadi kufikia tani 138 kwa mwaka ili Waziri aweze kuuzindua na kuanza kutumika.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mohamed Mchengelwa ametoa maagizo hayo leo Mei 21, 2023 akiwa mkoani Singida kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyo fanyika kitaifa viwanja vya Bombadia mjini Singida na yeye akiwa Mgeni Rasmi.
"Kwa niaba ya serikali nawahakikishieni kwamba, serikali inawathamini sana ninyi nyote mnao jishughulisha na ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali, hivyo inawapongeza sana. Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuiongezea tija sekta ya nyuki na asali ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa, na hii inawezekana kabisa" alieleza Mhe Waziri Mchengerwa.
Mbali na kuzindua mwongozo wa utunzaji shamba la ufugaji nyuki, Waziri Mchengerwa alisema pia kwamba wakati umefika vijana wanao hitimu vyuo vikuu nchini waweze kusaidiwa na serikali kujiajiri kupitia sekta ya nyuki na uzalishaji asali hivyo kuiagiza TFS iandae mpango mkakati huo mapema na kuuwasilisha kwake ili auzindue uanze kazi.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Bw Deusdedit Bivoyo wakati akitoa salamu zake kwa Mgeni Rasmi, ambae ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mohamed Mchengelwa alianza na kutoa nukuu ya Mkurugenzi mstaafu wa Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) kwa kusema hivi, nanukuu
"Nyuki wana jukumu muhimu sana katika kuongeza mazao ya chakula na kuhakikisha usalama wa mazao ya chakula na lishe na bila kuwa na nyuki, FAO haitaweza kutimiza lengo lake la usalama wa chakula bila nyuki" mwisho wa kunukuu.
Mkrugenzi huyo wa Misiti na Nyuki alimweleza Mhe Waziri dhamira ya Idara ya Misitu na Nyuki katika kutekeleza lengo la FAO kuhusu usalama wa chakula na lishe, hivyo kumsihi Waziri azindue mwongozo wa kutumia katika mashamba la ufugaji nyuki na pia kuzindua Duka la kuuzia Asali ili kutunza ubora wake ikiwa sokoni.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalihudhuriwa na umati wa watu wakiwemo wafugaji wa nyuki na wazalishaji wa Asali kwa njia ya kisasa, pamoja wa taasisi mbalimbali za serikali na binafsi pamoja na zile zilizopo chini ya wizara ya maliasili na utalii, Waziri Mhe Mchengerwa alitunuku pia Tuzo maalumu kwa niaba ya serikali kwa makundi mbalimbali na taasisi na watu binafsi kwa kutambua mchango na juhudi zao katika kuendeleza sekta ya nyuki na Asali.
Baadhi ya waliopatiwa Tuzo hizo ni Mhe Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu mstaafu wa serikali awamu ya Nne, na Meneja wa Mradi wa BEVAC Bw Martin Mgallah ambae mradi anao usimamia wa kuendeleza ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa na uzalishaji wa Asali kibiashara unatekelezwa vyema katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida, Shinyanga, Katavi na Pemba.
Sherehe hizo zimefanyika hapa nchini mwaka huu 2023 kwa mara ya Nne tangu Umoja wa Mataifa (UN) ulipo tangaza mwaka 2017 kuwa kila Mei 20, itakuwa ni Siku ya Nyuki Duniani na mwakani 2024, maadhimisho hayo hapa nchini yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma.
Mwisho.
0 Comments