Na Urban Epimark, SINGIDA.
Maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyo fanyika mwaka huu kitaifa mkoani Singida kuanzia Mei 18 hadi 21, 2023 yamekuwa ya mafanikio makubwa kwa jamii na sekta nzima ya misitu na nyuki kwa kutoa Elimu kwa njia ya makongamano na uoneshaji bidhaa kwenye maonesho.
Maadhimisho hayo yaliyoratibiwa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana vyema na wadau mbalimbali wakiwemo Mradi wa kuendeleza ufugaji nyuki nchini yaani BEVAC, Wakala wa kuendeleza misitu yaani TFS lakini pia Jukwaa la Ufugaji nyuki yaani TABEDO na zingine nyingi.
Katika makala hii fupi tutaangazia jinsi Jukwaa la Ufugaji Nyuki yaani TABEDO linavyo tekeleza kwa vitendo dhima ya kushirikishana kwa wahitimu wa vyuo vikuu nchini katika kujiajiri hususani kupitia tafiti zao wanazo fanya wakiwa vyuoni lakini pia kwa kuzingatia agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mohamed Mchengelwa kuwezesha vijana kujiajiri.
Hotuba ya Mgeni Rasmi siku ya kufunga maonesho hayo ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani ambae alikuwa ni Waziri mwenye dhamana na Maliasili na Utalii nchini Mhe Mohamed Mchengelwa katika maagizo yake kwa watendaji wa wizara, alisisitiza kwamba
"Ipo fursa kubwa ya vijana wanao hitimu vyuo vikuu kuweza kujiajiri katika sekta ya misitu na nyuki kwani bidhaa zitokanzo na mdudu nyuki ikiwemo Asali zinahitajika kwa kiwango kikubwa duniani na kutoa rai kwamba vijana wasaidiwe wajikusanye, watengeneze vikundi na serikali kupitia Wizara ikisaidiana na Jukwaa la Ufugaji Nyuki (TABEDO) iweze kuwajengea uwezo ili wajiajiri katika sekta ya Nyuki"
Maagizo haya Waziri Mchengelwa aliyatoa mapema kwa Mwenyekiti wa TABEDO wakati alipotembelea banda la TABEDO na kumtaka Mwenyekiti wake Bi Rudia Hamudu kuhakikisha anaongeza idadi ya vijana walio jiajiri katikavsekta ya nyuki hadi sasa ambao ni takribani elfu 50 ambao Waziri alisema, hawatoshi.
"Serikali itaisadia TABEDO kuwajengea uwezo vijana ambao katika sensa ya watu ya mwaka 2022, imegundulika ni zaidi ya nusu ya watanzania wote hivyo, suluhisho kwa wao kupata mahitaji yao ni kujiajiri katika sekta ya nyuki" alisema Mhe Waziri Mchengelwa.
Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Nyuki nchini (TABEDO) Bi Rudia Hamudu anasema, tayari Jukwaa hilo limeshaanza kutekeleza maagizo hayo ya serikali kwa kusaidiana na wadau mbalimbali kuhakikisha vijana kutoka vyuo vikuu wanajiahiri kupitia sekta ya nyuki.
Bi Rudia anasema, katika dhima nzima ya kushirikishana, TABEDO inashirikiana vyama, taasisi na wadau wengine kuwajengea uwezo wanachama wake wakiwemo vijana baada ya kujiunga TABEDO ili kujifunza jinsi ya kuandaa vifaa stahiki vya kufugia nyuki, jinsi ya kuvuna Asali na kuisindika na kisha kuiweka kwenye vifungashio sahihi na kuziwekea alama za ubora pamoja na Barcodes.
Amelitaja Shirika la kuendeleza viwanda vidogo vidogo nchini yaani SIDO, lenye jukumu la kuwapatia wazalishaji wadogo ujuzi na maarifa ya kuandaa vifaa/mizinga, kuwafundisha jinsi ya kuitundika na kuvuna mazao ya nyuki kwa kuwajengea uzoefu na kuwaelekeza kwenye matumizi ya teknolojia sahihi na rahisi itakayo wapatia tija zaidi.
Ameitaja taasisi nyingine ya GS1-Tanzania ambayo umuhimu wake kwa Jukwaa la Nyuki (TABEDO) ni kuzipatia ithibati ya Msimbomilia kwenye bidhaa yaani Barcodes baada ya kuzifungasha kitaalumu ili kusaidia kuzitangaza kwenye masoko ndani na nje ya nchi kwa mifumo ya kidigitali.
TABEDO pia inahakikisha inawawezesha wanachama wake kushiriki katika maonesho mbalimbali na kwenye makongamano ambayo yanalenga kukuza zaidi ujuzi na utaalam wa kuzaliza bidhaa bora zenye ushindani sokoni na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na pia kwa Taifa.
Wakitoa ushuhuda wa jinsi TABEDO imekuwa ikisaidia vijana baada ya kuhitimu mafunzo yao vyuo vikuu ili kujiajiri na haswa kutokana na tafiti wanazo fanya, Mkurugenzi mwendeshaji wa kikundi cha Singida Beekeepers Bw Yasini Masenga ambae ni mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodona (UDOM) na mwenye shahada ya Biology anasema,
"Mimi ni mhitimu wa UDOM mwaka 2020 katika kitivo cha Biology. Nilipo kuwa chuoni nilifanya utafiti wa kuhusu nini faida za mdudu nyuki katika mkoa wetu wa Singida na hivyo kuvutiwa sana na sekta hii na hivyo kutaka kuendelea zaidi kujikita katika sekta hii ili kujiajiri" anaeleza Bw Yasini.
Yeye anaishukuru TABEDO kwa kumwonesha njia ya jinsi ya kujiajiri lakini pia anaushukuru mradi wa kuendekeza ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa na kuzalisha Asali kibiashara wa BEVAC ambao wao kwa pamoja ndio wamemfikisha alipo sasa na kuweza kujiajiri.
Singida Beekeepers inatengeneza bidhaa za dawa za tiba mbadala kwa kutumia Masalia ya nyuki walio kufa, na pia kujishughulisha na ufugaji nyuki, uchakataji wa Asali na ufungashaji wake, ujuzi ambao ameupata kutoka SIDO.
Mwingine mwenye ushuhuda kama huo ni Bi Salama Jima ambae pia ni mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambae ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni yake ya Bee Place inayo jishughulisha na uuzaji wa bidhaa za nyuki, vifaa vya uvunaji asali na mengine mengi.
Bi Salama anaishukuru TABEDO kwa kumlea na kumtafutia fursa za kujijengea uwenzo hadi kujiajiri mfano SIDO na taasisi zingine na pia kwenye makongamano mbalimbali na maonesho ya biashara, ameeleza Bi Salama.
Katika kuhitimisha makala hii, Mwenyekiti wa TABEDO Bi Rudia Hamudu anatoa wito kwa vijana wote nchini, kuitumia vyema fursa ya kujiajiri kupitia sekta ya nyuki.
Lakini pia amesema, agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mohamed Mchengelwa la kuitaka TABEDO kukusanya vijana wengi zaidi ili wizara iweze kuwajengea uwezo, kwamba TABEDO itajipanga vyema zaidi kulitekeleza na pindi maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani mwakani 2024, yatakayo fanyika mkoani Dodoma pawepo na hatua kubwa ya mafanikio zaidi kwa vijana kujiajiri kuptia sekta ya nyuki baada ya kuhitimu vyuo vikuu.
Mwisho.
0 Comments