Na Salum Maige, Geita
Maisha ya watoto katika mitaa,vijiji na Vitongoji vinavyounda kata ya Nyanguku Halmashauri ya mji wa Geita yako shakani kama juhudi za makusudi hazitafanyika za kuthibiti kuzagaa kwa wanyama hatari aina ya fisi ambao wameanza kuingia kwenye makazi ya watu.
Hali hii inatokana na baadhi ya matukio ya wanyama hao kukimbiza watoto nyakati za asubuhi wanapokwenda shule na nyakati za usiku, na wakati mwingine hushambulia mifugo zikiwemo mbuzi,kondoo na ng’ombe.
Kutokana na hali hiyo kamati ya ulinzi na usalama kata ya Nyanguku imelazimika kufanya mikutano ya hadhara kuwaelimisha wananchi juu ya kuchukua hatua za haraka kuwalinda watoto dhidi ya wanyama hao hatari ambao wamekuwa wakiishi pemezoni mwa milima iliyo jirani na makazi ya watu.
Hatua hiyo inakuja wakati wakazi wa kata ya Nyanguku wakiwa hawajasaua tukio la mtoto mwenye umri wa miaka saba kufariki dunia mwaka 2021 baada ya kunyakuliwa na fisi na kuonekana baadhi ya mabaki ya mwili wake pembezoni mwa vichaka.
Fisi wenye njaa wakiwa mawindoni |
Katika mkutano uliofanyika mtaa wa Kakonda ,mtemi wa sungusungu kata hiyo,Mathias Kahindi amewataka wazazi na walezi kulinda usalama watoto wao kwa kuwasindikiza wakati wa kwenda shule ili wasishambuliwe na wanyama hao hasa nyakati za asubuhi ambapo wanyama hao huonekana njiani wakati wakirudi kwenye hifadhi yao.
“Tupo kwenye ziara ya kufanya mikutano ya hadhara kwa wananchi tunawaelimisha kuwalinda watoto dhidi ya wanayama hao ambao sasa wameshamili kuonkana kwenye makazi ya watu,pia tumepiga marufuku watoto kuzagaa kwenye maeneo ya senta nyakati za usiku”anasema Kahindi.
Ameongeza kuwa,wamezuia watoto kuzagaa mtaani nyakati za usiku mwisho saa moja ili kuthibiti tishio la wanayama hao kushambulia watoto hasa wale wadogo na wakati mwingine kuwalinda na matukio ya ukatili yakiwemo ya ulawiti na ubakaji.
“Imezoeleka matukio mengi ya fisi kushambuliwa watu yanawatokea watoto wadogo chini ya miaka minane ambao umri wao ni mdogo zaidi na hawana uwezo wa kijitetea,aidha kwa kukimbia au kupiga mayowe ili kupata msaada kwa watu wazima”,anasema kiongozi huyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kakonda Joseph Mshindi amesema, kuna milima ipo kusini mwa mtaa huo ambayo inasemekana wanyama hao wanainshi humo inapofika mida ya saa 12 jioni huanza kuzagaa kwenye makazi ya watu.
“Hawa wanyama kwa kweli wanaoekana na kuna kipindi waliwakimbiza watoto wanaenda shule na hivyo tunaendelea kuwasisitiza wazazi kuhakikisha wanasimamia ulinzi wa watoto wao na litakuwa jambo la kusikitisha mtoto kupoteza maisha kwa sababu ya kushambuliwa na fisi”anasema mwenyekiti Mshindi.
Mwenyekiti huyo amepongeza hatua ya kamati ya ulinzi na usalama kufanya kampeni ya kuwaelimisha wananchi kuhusu ulinzi wa watoto wao dhidi ya matukio ya fisi kushambulia watu na kuthibiti matukio ya watoto kulawitiwa na kubakwa.
Sophia Mathias mkazi wa mtaa huo,amesema,usalama wa watoto uko shakani hasa muda wa asubuhi wanapoenda shule lakini kwa sasa wanajitahidi kuwasindikiza watoto wao lakini baadhi ya wazazi na walezi hawafanyi hivyo jambo linalohatarisha usalama kwa watoto.
“kwetu hapa kuna siku watoto walikimbizwa na fisi wanaenda shule mida ya asubuhi lakini baada ya kupiga mayowe na walikuwa wengi fisi walitokomea machakani,na watoto ambao ni wa kulinda zaidi ni wale wa awali ,darasa la kwanza na pili”anasema Shida Kadikilo.
Mkaguzi wa polisi kata ya Nyanguku Denice Stephano amewataka wananchi kusimamia haki za watoto ambapo mzazi au mlezi anao wajibu wa kutimiza majukumu yake ya kusimamia usalama wa mtoto.
“Wananchi mnao wajibu wa kusimamia haki za mtoto,baadhu ya haki hizo ni pamoja na mtoto anahitaji kuishi na kulindwa,hivyo niwaombe wananchi tuwe mstari wa mbele kusimamia haki hiyo,watoto,hawa ndiyo viongozi wa baadaye”anasema mkaguzi huyo akiwa kwenye mkutano wa hadhara.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa kata hiyo ambaye ni mtendaji wa kata John Shatta amesema baada ya kuwepo kwa tishio la wanayama hao wamekaa kikao na kukubaliana kuwa,watoto wanaosoma katika shule ya msingi Kakonda wawe wanafika shule muda wa saa 1:30 asubuhi ili kuwalinda na wanyama hao.
“Tunafanya utaratibu wa kuwaelimisha wananchi wawe walinzi wa watoto wao,kata yangu kuna wanayama hao ni wengi sana ,na ukumbuke tukio lililotokea mtaa wa Nyakato ambapo kuna mtoto alichukuliwa na fisi na tukaambulia ubongo wake na viungo vichache vingine havikuonekana” anasema Shata.
Hata hivyo,Shata amesema,wanyama hao wamekuwa wakipotea inapotokea maofisa wanyama pori kwenda kuwasaka ili kuwathibiti jambo ambalo limekuwa likihusishwa na imani za kishirikina.
Meneja wa wakala wa huduma ya Mistu Tanzania(TFS)wilaya ya Geita Almas Mggalu alipotafutwa kuzungumzia hatua zinazochukuliwa na taasisi hiyo kithibiti wimbi la kuzagaa kwa wanyama hao alisema viongozi wa mitaa wanatakiwa kutoa taarifa za wanyama hao ili kuwathibiti kabla hawajaleta madhara kwa binadamu wakiwemo watoto.
Katika kipindi cha mwaka jana wa 2022 watoto wawili Mariam Mateso(5) na Nile Hassani(5) ambao walikuwa wakisoma darasa la awali walipoteza maisha huko katika halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita baada ya kushambuliwa na fisi.
Mwisho.
0 Comments