Mkuu wa dawati la Jinsia wanawake na watoto wilaya ya Geita Christina Katana akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mwangimagi mjini Geita. |
Salum Maige,Geita.
Februari 28,mwaka huu serikali kupitia wizara ya elimu sayansi na teknolojia ilitoa waraka wa elimu Na.01 wa mwaka 2023 kuhusu uboreshaji wa huduma ya mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi kuwa na watoa huduma wawili wa kike na wakiume ikiwa ni mkakati wa kudhibiti unyanyasaji na ukatili kwa watoto.
Hatua hiyo ya serikali ni baada ya kutokea kwa matukio ya unyanyasaji yanayodaiwa kufanywa na makonda na madereva kwa wanafunzi wanaosoma shule zinazotoa huduma ya usafiri wa mabasi hivyo wizara hiyo ikatoa maelekezo kwa wamiliki wa shule kuhakikisha mabasi yanakuwa na wahudumu hao.
Matukio yaliyoripotiwa ni madai ya baadhi ya makonda,madereva na watoa huduma wa mabasi hayo kuwafanyia ukatili wa kingono baadhi ya wanafunzi wanapowarudisha nyumbani hasa nyakati za jioni.
Katika mkoa wa Geita tayari kuna hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa za kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa kupitia waraka huo yanazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuanza kutoa elimu kwa wamiliki wa shule wanaotoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi pamoja na waratibu elimu kata.
Akizungumzia hatua hizo Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Geita Nelson Ndifwa amesema, amezunguka wilaya zote tano za mkoa wa Geita na kufanya vikao vya kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa agizo la serikali la kuhakikisha mabasi yanakuwa na watoa wawili wa kike na kiume.
Amesema ,kabla ya kufunguliwa shule julai 3,mwaka huu kutafanyika ukaguzi wa magari yote yanayotoa huduma hizo yanakuwa na rangi za njano,watoa huduma wawili,viti kuwa na mikanda kwa ajili ya usalama wa watoto.
Kadhalika,ameongeza kuwa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani litahakikisha mtoto anatoka na kurudi nyumbani akiwa salama bila kunyanyaswa au kufanyiwa ukatili wa namna yoyote.
“Na niwaonye tu wamiliki wa shule ,mtoto kusimama ndani ya gari sio kitendo kizuri,tumeshatoa maelekezo kwa wamiliki wa shule kuhakikisha magari yote yanakuwa na mikanda na watoto wakae kulingana na viti vilivyomo sio kubeba zaidi ya uwezo wa gari”,anasema Ndifwa.
Katika kuhakikisha usalama wa mtoto unafuatwa ,ameshauri kuwa,kila shule kuwa na afisa usafirishaji atakayekuwa anaratibu masuala ya usafiri kila siku kwa kuzingatia ratiba ya safari za watoto na kwamba mtu huyo atahakikisha magari hayo yanafanyiwa ukaguzi kila wakati.
“Afisa huyo pia atakuwa na kazi ya kuhakikisha gari linaloondoka kwenda kuchukua watoto na kupeleka watoto nyumbani linakuwa na watoa huduma wawili,huwezi kusajili wanafunzi wengi halafu ukawa na magari machache,tutafuatilia kila hatua ,jambo la kuwalundika watoto kwenye gari ni ukatili ambao haukubaliki pia”anasema Ndifwa.
Mkuu wa dawati la jinsia,wanawake na watoto wilaya ya Geita mkaguzi msaidizi wa Polisi Christina Katana amevitaja viashiria vilivyoonekana na kusababisha serikali kutoa waraka huo ni kunyanyasika kwa watoto hasa mtoto kwanza kuingia kwenye gari na wa mwisho kushuka.
“Mtoto wa kwanza kuingia kwenye gari ndiye anakuwa hatarini zaidi kufanyiwa unyanyasaji na ukatili kwani anachukuliwa nyumbani mapema,na mtoto wa mwisho anazungushwa kwenye gari zaidi ya masaa mawili hadi jioni naye yupo kwenye wakati mbaya wa kufanyiwa vitendo hivyo”anasema Katana.
Ameongeza kuwa, kitu kinachokwaza wapinga ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto ni idadi kubwa ya watoto wanaobebwa kwenye gari na kusababisha watoto wakati mwingine kubebana na kusimama ndani ya gari kitendo ambacho ni kumnyanyasa na kumkatili mtoto.
Kamishna wa Elimu Tanzania Dk.Lyabwene Mtahabwa |
0 Comments