TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MWANAFUNZI ESTER NOAH ASIBEZWE, ASAIDIWE ARUDI DARASANI

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera, amekemea baadhi ya waalimu wa Shule ya Sekondari Panda Hill kupunguza adhabu ya viboko kwa wanafunzi badala yake wawasaidie kimalezi wanafunzi hao kwa njia nyingine.

Na Urban Epimark, MBEYA

Sakata la binti aliyepotea mkoani Mbeya Elizabeth Noah (18) anae soma kidato cha Tano Shule ya Sekondari Panda Hill na baadaye kupatikana alikopatikana, wazazi tunalo jambo la kujifunza hapa.

Mijadala inayoendelea tangu apatikane binti huyu kwenye makundi mbalimbali, kurusha picha zake, kumbebesha lawama zote ama kumuona hafai kwenye jamii bila kujadili namna ya kumsaidia, sio sahihi.

Tuelewe kwamba hakuna mzazi anayependa kuona mwanaye anaharibikiwa, na zaidi mtoto anapokosa  anahitaji kurekebishwa, kusaidiwa kurudi kwenye mstari ingali bado mapema.

Samaki mkunje angali mbichi.

Tuelewe kuwa, mtoto anapo zaliwa ni wa jamii, na tunatamani sana jamii irudi kwenye misingi ile ya malezi shirikishi ambapo kila mwana jamii analo jukumu la kumlinda na kumpa malezi mtoro wa jirani hata kama sio wa kumzaa na dhamira hii ni ya ukale, uzamani,  kwamba mtoto wa mwenzio ni wako.

Mwanafunzi Ester Noah (18) mwonekano wake alipokuwa shuleni. Ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Panda Hill, mkoani Mbeya anae soma kidato cha Tano mchepuo wa sayansi masomo ya PCB.

Ukimuona anaharibika au anaharibikiwa shiriki kumbadilisha, shiriki kumtoa huko, na mzazi mwenye mtoto ukisikia mwanao ana fundishwa kurekebika, usiwe mkali, litambue hilo na ushukuru.

Ulimwenguni wa sasa umeharibika, watu  wamekuwa wawindaji, wana lazimisha mzazi kukosa nguvu kumdhibiti mwanae. Kila aendako yupo kwenye mawindo, utamdhibiti nyumbani, akienda ibadani au dukani atakutana na wawindaji, akienda shuleni  atakutana nao njiani, akiwa shule atakutana nao, kila mahali wapo.

Mzazi ana nafasi ya kuzungumza na mtoto, ana nafasi ya kumsaidia, lakini wakati mwingine mtoto anashawishiwa, ana shawishika, anarubunika, nae anazo akili zake binafsi mbali na mzazi au mlezi, ndio maana nguvu ya pamoja inahitaji kuwalinda watoto wetu, husani wa kike na hata wa kiume kwa ulimwengu wa sasa.

"Mtoto wa mwenzio ni wako jamii, nisaidieni kumlinda, kumrekebisha na kumweka sawa bila kushiriki kumharibu"

Kwa sakata la mwanafunzi wa Panda Hill, kuharibika ama kuharibiwa kwake, kurubuniwa au kurubunika kwake, kunyoa kiduku ama kukutwa alikokutwa,  hakumuondolei ubinti wake, au utu wake na wakati mwingine mzazi huwa hapendi, ama hashiriki kufanya awe hivyo, ama kufanya hayo, bali binti huyu  anahitaji kusaidiwa na jamii  kubadilika.

Mwanafunzi Ester Noah baada ya kupotea na kupatikana akiwa na hofu nyingi. Jamii inao wajibu wa kumsaidia aweze kurejea tena shuleni.

Kuyaweka yaliyo tokea hadharani na mtandaoni ni kuongeza tatizo liwe kubwa zaidi. Ni kuharibu kesho  yake iwe ya mashaka na ya  kuvunja moyo zaidi.

Hatupaswi kumhukumu kuwa hafai tena kwenye jamii, anayo nafasi ya kubadilika, kurekebishika, kwa hiyo tumsaidie. 

Kitendo hicho kitamuathiri baadaye na kinaweza kumharibu zaidi yeye na kizazi chake, kitaharibu kesho yake kama kitachukuliwa ndivyo sivyo.

Wanao mbeza na kumkashifu na kumpa maneno ya ovyo ovyo, wavae viatu vya mzazi wa huyu binti, kisha waone ingekuwa wako wangejisikiaje.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera (kushoto) anastahili pongezi kwa juhudi kubwa aliyo ifanya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Jamii ya watu mkoani Mbeya, kuhakikisha binti mwanafunzi Ester Noah (18) wa Shule ya Sekondari Panda Hill anapatikana. Katika picha, mwanzo kulia ni Mama mzazi wa Ester, Bi Isalia Iyobu wakiwa ofisini kwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya baada ya mwanafunzi huyo kupatikana Juni 23, 2023 mtaa wa Ifisi, Mbalizi Mbeya.

Hivyo tunapaswa kumshukuru Mungu amepatikana akiwa hai tena mwenye afya njema. Asikilizwe, asaidiwe aweze kurudi darasani. 

Huyu binti ni hazina ya Taifa. Anasoma masomo muhimu na magumu ya mchepuo wa PCB, sio jambo dogo. Akisaidiwa baadae anaweza kuja kuwa Daktari wa kutibu watu, tumsaidie.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments