Na Theresia C
Method,
Lusaka,
Zambia-Oktoba 2, 2024: Tanzania kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), imechukua uongozi wa mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda
wa SADC, ikiwa ni mara ya pili kushika nafasi hiyo muhimu. Katika hotuba yake
ya uzinduzi wa mkutano wa mwaka wa wakuu
wa mamlaka za kupambana na rushwa kwa nchi za SADC, Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU, Crispin Francis Chalalima, ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa kamati ya
SADC ya kupambana na rushwa (SACC), ametahadharisha kuhusu hatari kubwa ya
rushwa katika utoaji wa misaada wakati wa dharura.
Chalamila
ameeleza kuwa majanga ya dharura kama vile mlipuko wa magonjwa na athari za
mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kufungua milango ya rushwa katika hatua
mbalimbali za ugawaji misaada, ikiwa ni pamoja na udanganyifu, ubadhirifu wa
mali, na ukiukwaji wa maadili ya ununuzi. “Mchakato wa utoaji misaada upo
katika hatari kubwa ya kudhibitiwa na rushwa kwa sababu ya haraka na udharura
wa hali zinazokuwepo,” alisema Chalamila, huku akiongeza kuwa pia kunaweza
kutokea matumizi mabaya ya ngono (sextortion) kama mojawapo ya aina za rushwa
zinazoweza kutokea.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalalima, ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa kamati ya SADC ya kupambana na rushwa (SACC),
Mkutano huo, ukiwa na kaulimbiu: "Kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika usimamizi wa majanga na huduma za magereza katika ukanda wa SADC", umeangazia changamoto zinazokabili nchi wanachama wa SADC katika kukabiliana na rushwa wakati wa kushughulikia dharura. Chalamila alisisitiza umuhimu wa mikakati imara ya kanda ili kuhakikisha misaada inafika kwa walengwa kwa uadilifu na uwazi.
Aidha, Chalamila alimpongeza Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Monica Chipanta Mwansa wa Zambia, kwa uongozi wake imara katika kutekeleza mpango mkakati wa SADC wa kupambana na rushwa (2023-2027), ambao umejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa misaada na majanga.
Mkutano
huo wa siku tatu, uliofanyika jijini Lusaka, umehudhuriwa na wawakilishi kutoka
nchi 14 wanachama wa SADC, huku Tanzania ikiongoza mapambano hayo kwa mara ya
pili baada ya kuwa mwenyekiti mwaka 2017/2018. TAKUKURU inatarajiwa kuendelea
na juhudi hizi kwa mwaka wa 2024/2025, ikiwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
ukanda wa SADC unakuwa na mazingira safi na huru dhidi ya vitendo vya rushwa.
0 Comments