TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

BENKI KUU YA TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KUPITIA UNUNUZI WA DHAHABU ILI KUIMARISHA AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI

Na Theresia C Method;

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeonyesha mafanikio makubwa katika ununuzi wa dhahabu safi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Novemba 2024, benki hiyo ilifanikiwa kununua takriban tani moja ya dhahabu safi, ikiwa ni rekodi ya kihistoria. Kiasi hicho cha dhahabu kinajumuisha kilo 872 zilizotolewa katika mwezi Oktoba mwaka 2024 pekee, ambazo zinathamani ya Dola za Kimarekani milioni 74.

Dkt. Anna Lyimo, Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya BoT, alieleza kuwa pamoja na dhahabu zaidi ya kilo 300 waliyoinunua mwaka 2023, BoT sasa ina kiasi kikubwa cha dhahabu katika mfumo wa dhahabu fedha. Alisisitiza kuwa hatua hii inasaidia kuongeza thamani ya fedha za Tanzania, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, na kuchangia katika utulivu wa uchumi wa taifa.

Katika semina iliyoandaliwa na BoT kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Dkt. Lyimo alisisitiza kuwa ununuzi wa dhahabu umeonekana kuwa na manufaa makubwa kuliko uwekezaji mwingine kwa miongo miwili iliyopita, hasa katika kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani. Aliongeza kuwa dhahabu ni bidhaa yenye thamani inayoweza kupatikana kwa urahisi, na kwamba matumizi yake katika kujenga akiba ya fedha za kigeni yameonyesha faida kubwa kwa nchi.



Dkt Anna Lyimo akiwasilisha mada katika semina hiyo 

Mkurugenzi wa BoT tawi la Mwanza, Gloria Mwaikambo, alifungua semina hiyo na kusema kuwa lengo kuu ni kutoa uelewa wa kina kwa waandishi wa habari kuhusu shughuli za kifedha na uchumi, na hivyo kuwawezesha kutoa taarifa sahihi kwa umma. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari ni muhimu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za uhakika zinazohusiana na uchumi na fedha za taifa.


Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza Gloria Mwaikambo.

Semina hii ilihudhuriwa na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, na Kagera, na ilikuwa ni sehemu ya juhudi za BoT kuimarisha elimu kuhusu shughuli zake za kifedha na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

 


Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza, Gloria Mwaikambo (katikati mbele mwenye suti ya sketi)na baadhi ya watumishi wa benki hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari Kanda ya Ziwa walioshiriki semina hiyo.



 


Post a Comment

0 Comments