TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MAANDAMANO YA AMANI MANYARA YALENGA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA

Na mwandishi wetu;

Katika kuadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, maandamano ya amani yamefanyika leo mkoani Manyara, yakilenga kuhamasisha jamii kutokomeza ukatili wa kijinsia. Maandamano hayo yalianza katika viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Babati na kumalizika katika ukumbi wa White Rose, huku waandamanaji wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 10.

Tukio hili limewashirikisha makundi mbalimbali, yakiwemo wafanyabiashara wa mkoa wa Manyara, wanavyuo, waandishi wa habari, maafisa usafirishaji, na wadau wengine. Maandamano haya yameandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Lengo kuu ni kueneza ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

Katika hotuba yake, Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Paschal Mhagama, ameweka wazi kuwa rushwa ya ngono bado ni changamoto kubwa. Amebainisha kuwa kwa mwaka 2023, makosa 28 pekee ya rushwa ya ngono yaliripotiwa, idadi inayoonyesha muamko mdogo wa wahanga kuripoti vitendo hivyo. Mhagama amesema kuna  umuhimu wa jamii kutoa taarifa kwa vyombo husika. “TAKUKURU ipo tayari kushughulikia malalamiko hayo kwa weledi” amesisitiza Paschal Mhagama.


Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Paschal Mhagama

Amesema pia kuna madhara makubwa ya rushwa ya ngono, huku akihimiza uwajibikaji na mshikamano wa jamii katika kutoa ushirikiano wa kufichua wahusika wa vitendo hivyo.



Post a Comment

0 Comments