Na Mwandishi wetu:
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs - UTPC) imejipanga kushiriki kikamilifu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia kupitia kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2024. Kampeni hii inalenga kuelimisha jamii na kuhamasisha hatua za dhati za kupinga ukatili wa aina yoyote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mwaka huu, maadhimisho yataanza kwa uzinduzi rasmi mkoani Manyara kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Manyara. Uzinduzi huu utakuwa mwanzo wa kampeni itakayoendelea kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe kwa jamii nzima. Kampeni hii inalenga kutoa elimu ya kina kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na mbinu za kuutokomeza.
Kupambana na ukatili wa kijinsia ni
sehemu muhimu sana na juhudi zitakakiwa ili kuleta maendeleo endelevu. "Tunaposhiriki
katika juhudi hizi, tunachangia moja kwa moja kufanikisha lengo namba tano la
maendeleo endelevu (SDG5), ambalo linadhamiria kutokomeza ukatili wa kijinsia
ifikapo mwaka 2030," alisema Kenneth Simbaya, Mkurugenzi wa UTPC.
Kwa kushirikiana na taasisi za kiraia, viongozi wa dini, na wadau wa maendeleo, UTPC itaendesha mijadala na semina mbalimbali. Kupitia majukwaa ya kidigitali, wataalamu watashiriki kutoa elimu na maarifa kuhusu namna ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa ufanisi.
Kampeni ya mwaka huu itahusisha uzinduzi wenye matukio mbalimbali pamoja na mijadala inayowalenga wadau wa sekta zote. Kisha, kampeni itaendelea kwa nguvu kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. "Tunaamini kwamba suala la unyanyasaji wa kijinsia ni suala la elimu. Watu wakielimishwa ipasavyo, tunaweza kufanikisha azma ya kutokomeza ukatili wa kijinsia," alisema Simbaya.
UTPC inatoa wito kwa jamii nzima
kushiriki kikamilifu katika kampeni hii, ambayo inalenga kuleta mabadiliko
chanya katika maisha ya kila mmoja, nchi na dunia. Kwa kushirikiana, tunaweza kujenga jamii
yenye usawa, haki, na maendeleo.
0 Comments