TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 8.6 KWAAJILI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA VIJIJINI

Mkuu wa mkoa wa Geita , Mhe. Martine R. Shigela 

Na Theresia C Method;

Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 8.6 kwa ajili ya kuwafikishia nishati safi ya kupikia maeneo ya vijijini, ikiwa ni hatua muhimu katika kupambana na uchafuzi wa mazingira na uharibifu unaosababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa. Mpango huu ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kukuza matumizi ya nishati safi na endelevu, na unatarajiwa kunufaisha jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Deusdedith Malulu, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ameeleza hayo katika ziara yake, ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, amezungumzia mpango huu na kusema kuwa majiko ya gesi  kutoka Manjis yanauzwa kwa bei ya punguzo la asilimia 50% ambayo ni kiasi cha shilingi 17,500 kwa kila moja, jambo litakalowawezesha wananchi wengi vijijini kupata nishati safi kwa bei nafuu.

Mpango huu wa nishati safi ya kupikia ulizinduliwa rasmi mwezi Mei mwaka 2024, na unalenga kupunguza matumizi ya nishati chafu katika nchi nzima. Malulu alifafanua kuwa jumla ya majiko ya gesi 452,000 yameshasambazwa nchi nzima, yakigharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.6.

Katika Mkoa wa Geita, jumla ya majiko 16,275 yatatolewa, ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 pamoja na vifaa vyake vya ziada. Majiko haya yatauzwa kwa bei ya punguzo la asilimia 50. “Majiko haya yatauzwa kwa bei ya punguzo la asilimia 50, kupitia kampuni ya Manjisi, msambazaji rasmi wa majiko haya,” alisisitiza Mhandisi Malulu.


Deusdedith Malulu, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, ameeleza kuwa mpango huu umekuja wakati muafaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata nishati safi kwa bei nafuu. Amesema kuwa mkoa wa Geita una vijiji 486, na vijiji 483 kati ya hivyo vimeshapata huduma ya umeme, huku vijiji vitatu vilivyobaki katika kata ya Izumacheli, vikitarajiwa kupata umeme kupitia nishati ya sola hivi karibuni.

Shigela aliongeza kusema kuwa, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za nishati, msambazaji wa nishati kutoka kampuni ya Manjisi ahakikishe kuwa kila mmoja anapata mitungi ya gesi na mahali pa kujaza gesi karibu na maeneo yao.

Tumaini David, Meneja Masoko na Mauzo kutoka kampuni ya Manjisi, ameahidi kuhakikisha kuwa kampuni yao inafikia wananchi wote, akitaja matumizi ya vitambulisho vya taifa (NIDA) ili kuepuka watu kuchukua majiko mengi kwa ajili ya biashara. "Lengo letu ni kuhakikisha tunatimiza agizo la serikali la kuwafikia wananchi wote na kuwapatia majiko haya ya nishati safi," alisema David.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi za serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira na kuboresha afya ya wananchi kwa kupunguza madhara ya matumizi ya kuni na mkaa.





Post a Comment

0 Comments