Na Mwandishi wetu;
Picha: Mgombea Ubunge wa Jimbo la Busanda kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jafari Rajabu Seif akikadidhi fomu kwa Sarah Yohana kutoka INEC
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Busanda
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jafari Rajabu Seif, ametangazwa rasmi
kuwa mgombea wa nafasi hiyo baada ya kurejesha fomu na kukidhi vigezo vyote
vilivyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo 27/8/2025 na Bi. Sarah Yohana kutoka INEC, ambaye amethibitisha kuwa Dkt. Jafari amerudisha fomu kwa wakati na kutimiza masharti yote yanayohitajika kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu Dkt. Jafari Rajabu Seif amesema zoezi la uchukuaji fomu lilifanyika salama na leo Agosti 27, 2025 nimerudisha fomu na nasubili saa kumi kupata matokeo.
Akizungumza baada ya uteuzi huo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Geita, Renatus Sangano, ameeleza kuwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulifanyika kwa mafanikio makubwa.
"Leo tarehe 27 Agosti 2025, saa
kumi jioni tumepokea taarifa rasmi kutoka INEC kuwa mgombea wetu ametimiza
masharti yote na ameteuliwa rasmi. Tunajipanga kwa kampeni. Hatupambani kwa
ajili ya mtu mmoja, bali tunapambana kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi," amesema Sangano.
Ameongeza kuwa wakati ratiba ya kampeni ikisubiriwa kutolewa, wana CCM wanapaswa kujiandaa kwa mshikamano na nidhamu, ili kuhakikisha ushindi mkubwa kwa chama kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.
Kwa upande wake, Diwani mteule wa Kata ya Nyarugusu, Samantha Shabani Makula, ameelezea furaha yake kwa uteuzi wa Dkt. Jafari, akimwelezea kuwa ni kiongozi wa vitendo na siyo wa maneno.
“Mimi sipendi michakato. Tumepata
mwakilishi ambaye hatupotezi muda kwenye siasa zisizo na tija. Jimbo la Busanda
liko salama, Kata ya Nyarugusu iko salama, na Taifa liko salama chini ya
uongozi wa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan,” amesema Makula kwa
kujiamini.
Naye Katibu wa CCM Kata ya Nyarugusu, Ezekiel Ernest, akiwa na wananchi wa kata hiyo, ameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, akisema kuwa Dkt. Jafari ni chaguo la wananchi na anakubalika kwa kila kundi ndani ya jamii. “Tunashukuru sana kwa kupata mgombea kutoka eneo letu. Ni fahari kwetu na dhamira yetu ni kuhakikisha anashinda kwa kishindo,” ameeleza.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyarugusu, Oscar P. Ngalawa, amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kushikamana na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za maendeleo na kampeni zitakapoanza. Pia ametoa wito kwa vijana kujiunga na shughuli za kichama na kijamii kwa maendeleo ya eneo hilo.
Uteuzi huu rasmi wa Dkt. Jafari Rajabu Seif umeibua ari na hamasa mpya ndani ya CCM Busanda, huku wakisubili ratiba ya kampeni kutolewa rasmi.
0 Comments