Na Theresia Method-Geita;
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliongoza uzinduzi wa
Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini kwa mwaka 2025 yaliyofanyika katika
viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, mkoani Geita, Septemba 22,
2025.
Maonesho haya,
yaliyoanzishwa mwaka 2018, yamejikita katika kuimarisha sekta ya madini nchini
kwa kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha watanzania wote.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia
sahihi na kuwa na uongozi bora ili kufanikisha maendeleo endelevu katika sekta
ya madini, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025.
Maonesho hayo
yamekuwa jukwaa muhimu la kukutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka serikalini, sekta binafsi, wachimbaji wakubwa na wadogo, taasisi za
fedha, wajasiriamali hadi wafanyabiashara. Kaulimbiu ya mwaka huu
ilikuwa; “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya
Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.”
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitembelea mabanda mbalimbali.
Siku moja kabla ya uzinduzi wa maonyesho hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita (Samwel Shoo),alieleza kuwa Tume ya Madini imeshiriki kwa mara ya nane mfululizo katika maonyesho hayo, ambapo mwaka huu iliandaa huduma za elimu kwa wadau wote kuhusu teknolojia za kisasa katika utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Katika maonesho
hayo, Bodi ya Bima ya Amana (DIB) iliibuka kuwa miongoni mwa taasisi
zilizovutia watu wengi kwa utoaji wa elimu muhimu kuhusu kinga ya amana kwa
wateja wa benki na taasisi za kifedha. Bw. Nkanwa Magina, Mkurugenzi wa Kinga
ya Amana na Uwekezaji wa DIB, alieleza kuwa bodi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, na kuendelea kufanya kazi
chini ya vifungu vya 36 hadi 42 vya Sheria ya Mwaka 2006, ikiwa na lengo la
kuwalinda wateja wadogo dhidi ya kupoteza amana zao iwapo taasisi za fedha
zitakumbwa na changamoto.
“Bodi hii ilianza
rasmi mwaka 1994 kwa kazi kuu maalumu, moja ni kulipa fidia ya bima ya amana kwa
kiwango cha shilingi milioni saba na laki tano kwa kila mwenye amana katika kila benki au taasisi ya kifedha, na pili
ni kujenga imani ya wateja katika mfumo rasmi wa kifedha nchini” alisema Bw.
Magina .
Mapokezi kwa DIB
katika maonesho hayo yalikuwa chanya sana. Wananchi wengi walitembelea banda
hilo na kueleza kuridhishwa kwao na elimu waliyopewa. Mkuu wa Kitengo cha
Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw. Lwaga Mwambande, alisisitiza kuwa
taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ili
kuhakikisha huduma zake zinafika kwa Watanzania wengi zaidi, wakiwemo wale
wanaotumia mifumo ya kifedha isiyo rasmi kama VICOBA na SACCOS.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, alitumia jukwaa hilo kutoa rai kwa DIB kuongeza juhudi za kupanua huduma zake hadi kwenye vikundi vidogo vya kifedha visivyo rasmi.
“Watanzania wengi bado wanaweka fedha kwenye maeneo ambayo hayajasajiliwa
rasmi, na hivyo kupoteza mamilioni ya shilingi wanapokumbwa na changamoto. Ni
wakati sasa wa kuongeza kasi ya kulinda mitaji ya wananchi wetu,” alieleza DC Komba.
Kwenye majibu
yake, Bw. Mwambande alisema DIB imeshapokea ushauri huo na itaendelea
kuimarisha ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na taasisi nyingine ili
kufikia kundi hilo kubwa la wananchi wanaotumia mifumo isiyo rasmi.
“Kinga ya Shilingi
milioni 7.5 kwa kila mteja inatosheleza asilimia 99 ya wamiliki wa amana
nchini. Lengo letu si tu kulipa fidia endapo benki itafungwa, bali kuhakikisha
wananchi wana imani ya kudumu na mfumo rasmi wa kifedha,” alisema Bw.
Mwambande.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita (RMO), Dkt. Omari Sukari, naye hakuachwa nyuma katika kutoa pongezi kwa Bodi ya Bima ya Amana kwa kushiriki maonesho hayo na kutoa elimu kwa jamii kuhusu usalama wa fedha zao.
“Nimejifunza kwamba hata kama benki
ikifilisika, fedha zangu ziko salama kwa sababu kuna bodi inayozilinda. Hii ni
habari njema kwa Watanzania wote,” alisema Dkt. Sukari. mwenye shati la kitenge.
Aliipongeza DIB
pia kwa kuanza kuchukua hatua za mapema kuokoa benki zinazopitia changamoto
kabla hazijafungwa, jambo alilolielezea kuwa ni mwelekeo sahihi wa kujenga
uthabiti wa sekta ya fedha nchini.
Wananchi wengi
waliotembelea banda la DIB walieleza kufurahishwa na namna walivyopokelewa kwa
ukarimu na kufundishwa kwa kina kuhusu namna fedha zao zinavyolindwa. Salama
Aron, ni mmoja wa washiriki wa maonesho hayo, alisema “Nimejifunza kwamba fedha
zetu benki zipo salama hata kama benki itafungwa. Tunalindwa na Bodi ya Bima ya
Amana.”
Maonesho ya mwaka
huu yalihitimishwa rasmi Septemba 28, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Dkt. Doto Biteko, aliyesema maendeleo ya sekta ya madini nchini yameongeza
masoko ya madini hadi kufikia 43 na vituo vya ununuzi kufika 109.
Dkt. Biteko
alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuongeza ushirikishwaji wa Watanzania
katika mnyororo mzima wa thamani ya madini kutoka kwenye utafiti, uchimbaji,
uchenjuaji hadi biashara ya madini ili kuhakikisha rasilimali za taifa
zinawanufaisha wananchi moja kwa moja.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
akihutubia wananchi wakati wa kufunga Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya
Madini kwa mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Bombambili, mkoani Geita.
Zaidi ya washiriki 900kutoka ndani na nje ya Tanzania
walishiriki katika maonesho haya ya kihistoria, ambayo si tu yalionesha
teknolojia mbalimbali, bali pia yamefungua fursa ya elimu, ushirikiano na
ujenzi wa uchumi imara kwa Watanzania kupitia sekta ya madini na kifedha.
















0 Comments