Na Victor Bariety;
Tarehe 9 Septemba 2025, historia mpya imeandikwa Kigoma Mjini. Clayton Chipando, anayejulikana zaidi kwa jina la kisanii Baba Levo, alizindua rasmi kampeni zake za kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uzinduzi huu, uliopewa jina la “Uzinduzi wa Kihistoria”, ulichanganya siasa na burudani, ukihudhuriwa na maelfu ya wananchi waliomiminika Mwanga Community Centre kushuhudia mwanzo wa safari mpya ya kisiasa.
Tofauti na wanasiasa wengi
waliomtangulia, Baba Levo aliweka mbele kipaji chake cha sanaa. Aliambatana na
msafara mkubwa wa wasanii wa Bongofleva na vichekesho. Miongoni mwao ni Nyago
Man, mkimbizi kutoka Kambi ya Nyarugusu anayejulikana kwa miondoko ya
kinigeria. Uzinduzi huu ulikuwa na mvuto wa kipekee, uliothibitisha kwamba
siasa pia zinaweza kuwa jukwaa la ubunifu na umoja.
Siasa za Kejeli: Elimu Kama Silaha ya
Ubaguzi
Pamoja na shamrashamra hizo, makundi ya wapinzani yamejitokeza na kuanza kumchafua Baba Levo. Hoja yao kuu ni kwamba hana elimu ya juu, kwa hiyo hatakuwa na uwezo wa kuchambua mikataba ya kitaifa au kushiriki mijadala ya bunge kwa weledi. Wamekuwa wakimtaja Zitto Kabwe, msomi wa chuo kikuu na mpinzani wake mkuu, kama kigezo cha “mgombea bora zaidi.”
Lakini hoja hii ni siasa za upotoshaji. Ni jaribio la kuigeuza elimu kuwa kigezo cha kuamua uwezo wa mtu kuongoza. Ukweli ni kwamba, uongozi si karatasi ya shahada; uongozi ni kipaji, dhamira na moyo wa kutumikia wananchi.
Takwimu Hazidanganyi: Kigoma ni Wengi
Bila Shahada
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS):
82.2% ya wakazi wa Kigoma wana elimu ya msingi (darasa la saba) ndiyo kiwango cha juu walichokifikia.
22% hawajawahi kuingia darasani kabisa.
Ni 2.9% tu wamefikia elimu ya chuo kikuu au ngazi ya juu zaidi.
Hii maana yake ni kwamba zaidi ya
asilimia 100 kati ya kila wananchi 82 wa Kigoma wako katika kiwango cha elimu
sawa na Baba Levo au chini yake. Baba Levo anawaakilisha wengi; yeye ni kioo
cha changamoto zao. Kile wanachokipitia wao ndicho alichokipitia yeye, na sasa
anataka kukipeleka bungeni ili kiwe historia.
Mifano Hai: Darasa la Saba
Walioandika Historia
Si mara ya kwanza kwa wabunge wenye elimu ya msingi kuacha alama kubwa katika siasa za Tanzania.
Joseph Kasheku Musukuma, aliyekua Mbunge wa
Geita, licha ya kuwa darasa la saba, amekuwa kinara wa mijadala mikali
bungeni na amefanya kazi kubwa jimboni mwake. Ni kielelezo kwamba elimu siyo
kizuizi cha ufanisi.
Hussein Amar Kassu, aliyekua Mbunge wa
Nyang’wale, naye akiwa darasa la saba, amepigiwa debe na wananchi kutokana na
kazi kubwa alizofanikisha jimboni.
Mifano hii inathibitisha wazi: kipimo cha uongozi siyo shahada, bali ni mchango halisi kwa wananchi.
Sauti ya Wadau
Wadau wa siasa na jamii wamekuwa wakitazama kwa makini mchuano huu wa Kigoma Mjini. Baadhi yao wanasema hoja ya elimu imegeuzwa silaha ya kisiasa badala ya kuwa chachu ya mjadala mpana wa maendeleo. Wanaona kuwa uhalisia wa maisha ya wananchi—hasa kundi kubwa lililoishia elimu ya msingi—ndilo linalopaswa kuwa kipimo cha nani anastahili kupewa dhamana ya uongozi.
Wachambuzi wa mambo ya kijamii pia
wanabainisha kuwa siasa za ubaguzi wa elimu zinaweza kuua ushiriki wa vijana na
wananchi wa kawaida katika uongozi. Badala yake, wanasema, siasa zinapaswa kuwa
jukwaa la kila mmoja, awe na shahada au darasa la saba, mradi awe na dhamira
safi na uwezo wa kutatua changamoto za wananchi.
CCM Iliona Mbali
Ikumbukwe kuwa awali Baba Levo hakushinda kura za maoni ndani ya CCM. Hata hivyo, chama kilirejesha jina lake na kumpa ridhaa ya kugombea. Uamuzi huu ni ushahidi kwamba CCM haikufanya makosa. Iliamua kusimama na kiongozi anayewakilisha kundi kubwa la wananchi—wale wa kipato cha chini, wale waliopambana na changamoto za elimu, wale ambao sauti zao mara nyingi hazisikiki.
Kama diwani wa zamani Kigoma, Baba Levo alionyesha uongozi wa karibu na wananchi, jambo lililompa heshima na sifa kemu kemu ndani na nje ya jimbo.
Hitimisho: Kigoma Iache Ubaguzi wa Elimu
Wananchi wa Kigoma Mjini wanapaswa kujiuliza swali moja rahisi: tunataka mbunge wa karatasi au mbunge wa watu?
Elimu ni jambo jema, lakini si kigezo cha pekee cha uongozi. Tanzania inahitaji viongozi wanaotoka moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi wa kawaida, wanaojua changamoto si kwa vitabu, bali kwa macho na miguu. Baba Levo ni sauti ya wengi, ni mwakilishi halisi wa changamoto za Kigoma, na ndiye chaguo sahihi kuelekea Oktoba 29.
Wana Kigoma, huu si wakati wa kumtazama mtu kwa shahada yake. Huu ni wakati wa kuamua nani ataenda bungeni kuwasemea matatizo yenu, na Baba Levo ndiye mtu huyo.
Mwisho
Imeandaliwa na Victor Bariety
0757-856284
0 Comments