TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

IRAMBA YAAMKA: AHADI ZATIMIA, FURSA ZAMIMINIKA KUPITIA MIKONO YA RAIS SAMIA NA MWIGULU

Na Victor Bariety;

Uwanja wa Kiomboi jana ulikuwa bahari ya kijani na njano. Vumbi la Iramba lilisimama kwa muda, likishuhudia historia ikiandikwa. Maelfu ya wananchi walijitokeza, si kwa kushuhudia tu, bali kwa kuunga mkono safari ya maendeleo ambayo sasa imeonekana kwa macho yao.


Katika jua kali la Septemba 10, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alipowasili Iramba alilakiwa kwa nderemo, nyimbo na shangwe zisizoelezeka. Mapokezi hayo yalikuwa ishara ya heshima na ukaribu wa wananchi kwa kiongozi wao mkuu, aliyerejea kuzungumza nao kuhusu matunda ya Ilani ya CCM.


Soko la Madini: Dhahabu Yaitwa Nyumbani


Akiwahutubia wananchi, Rais Samia alianza kwa kufungua ukurasa wa uchumi wa Iramba – madini. Kwa msisitizo alisema:

“Soko la madini la Shelui sasa linafanya kazi. Zaidi ya gramu milioni 1.5 zimeuzwa hapa, zenye thamani ya shilingi bilioni 192. Fedha hizo zimeingia moja kwa moja mikononi mwa wachimbaji wetu wa Iramba.”

 


Kauli hiyo ililipuliwa kwa shangwe. Wachimbaji wadogo, waliokuwa wakihesabiwa kama kivuli, leo ni mashujaa wapya wa uchumi wa wilaya. Leseni zilizokuwa zikishikiliwa bila kutumika sasa zimegawanywa upya. Leseni 32 zimetolewa kwa vikundi tisa vya wachimbaji wadogo wa hapa hapa, na leseni nane za uchenjuaji madini zimepewa kwa eneo la Sekenke.

Kilimo cha Umwagiliaji: Shamba Mara Mbili, Tija Mara Mbili

Ndoto ya mkulima wa Ishishi, Kata ya Msingi, imepata jibu. Serikali inatekeleza mradi wa umwagiliaji wenye thamani ya shilingi bilioni 34.

Mzee mmoja wa kijiji hicho alieleza:

“Hapo awali tulilima mara moja tu kwa mwaka tukitegemea mvua. Lakini sasa, kwa umwagiliaji huu mpya, tutalima mara mbili na kuvuna mara mbili. Huu ni ukombozi wa mkulima mdogo.”


Ajira kwa Vijana: Gesi, Barabara na Fursa Mpya


Rais Samia pia aliwakumbusha vijana kuwa mradi wa bomba la gesi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga unapita Singida, na tayari unazalisha ajira nyingi.

“Mkishindwa kuchangamkia nafasi hizi, vijana wa mikoa jirani watazichukua, na nyinyi mtabaki mnaangalia,” amesitiza.

Zaidi, serikali inakamilisha barabara za Kiomboi–Mtulia na Iguguno–Sibiti kwa kiwango cha lami. Barabara hizo zitafungua mji wa Kiomboi kibiashara na kuimarisha mawasiliano kati ya Iramba na wilaya jirani.

Mwigulu Nchemba: Mwana wa Iramba, Shujaa wa Iramba

Katika umati huo, pia alikuwapo Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba – mwana wa Iramba. Jina lake limekuwa kivutio na kielelezo cha matumaini. Kwa pamoja na Rais Samia, wameonekana kama mhimili wa heshima na maendeleo kwa wananchi wa Singida.

Kijana mmoja alisikika akisema:

“Samia ni mama wa taifa, Mwigulu ni mtoto wetu wa hapa. Wote wawili wameturudishia hadhi ya Iramba.”


Hitimisho: Kura ya Shukrani

Kadri jua lilivyokuwa likizama, nyimbo na shangwe za CCM ziliendelea kugonga anga. Rais aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kutoa kura ya shukrani kwa chama chao.

Kwa wananchi wa Iramba, kura si karatasi tu – bali ni uthibitisho kwamba safari ya maendeleo iendelee. Dhahabu imegeuka neema, mashamba yanatoa matumaini mapya, barabara zinafungua biashara, na vijana wanaona ajira mbele ya macho yao.

Na katika taswira hii, majina mawili yameunganishwa – Samia na Mwigulu – viongozi wanaochora ramani mpya ya Singida na Tanzania.

 

Mwisho 

Imeandaliwa na Victor Bariety

 0757 856 284

 

Post a Comment

0 Comments