Na Editha Edward;
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amesifu mafanikio ya miradi iliyotekezwa na Wakala wa
Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Nyang'hwale.
Hiyo ni mara ya tatu ndani ya siku chache, miradi ya TARURA mkoani Geita kusifiwa na kiongozi wa mbio za Mwenge. Ussi amepongeza ujenzi wa barabara ya Nzera (Geita), barabara ya Kasco (Manispaa ya Geita) na sasa mradi wa ujenzi wa boksi la kalavati katika barabara ya Kharumwa–Nyijundu.
“Niwapongeze sana TARURA, popote
nilikopita nikiwa na mwenge huu, nimeona miradi ya kiwango cha juu. Hata
huu mradi, nimeukagua, nimepitia nyaraka zote na hakuna chembe ya shaka. Huu
ni uthibitisho kwamba, fedha za wananchi zinatumika kwa haki, ndiyo maana
nauzindua rasmi” ameeleza Ussi
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na
Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyang’wale, Mhandisi John Msita, mradi huo,
umegharimu shilingi 579,680,000.00 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kwa mwaka
wa fedha 2023/2024.
Taarifa inaeleza mradi ulikuwa na
kazi tatu, ujenzi wa maboksi ya kalavati mawili ya zege na
matengenezo ya kilometa moja ya barabara ya changarawe. Utekelezaji ulianza
Juni 18, 2024 na kukamilika Aprili 14, 2025 chini ya mkandarasi D4N Company Ltd
ya Kahama.
Aidha, kiongozi wa mbio za mwenge,
ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Nyang’wale na Geita, kujitokeza
katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu na wakachague viongozi kwa kuzingatia
amani ya nchi
0 Comments