Na Victor Bariety-Geita;
Mkoa
wa Geita unaendelea kujipambanua katika ubora wa utekelezaji wa miradi ya
miundombinu, baada ya barabara ya Nyakafuru, iliyojengwa kwa kiwango cha lami
nyepesi, kutajwa kama mradi wa mfano kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
2025.
Barabara
hiyo yenye urefu wa kilomita 0.7, inayojengwa na mkandarasi Rumanyika
Investment Co. Ltd wa Karagwe kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 569,
imekuwa tumaini jipya kwa wakazi wa Masumbwe na wachimbaji wadogo wa dhahabu
waliokuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa za usafiri. Mradi ulianza Agosti
2024 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2025, chini ya usimamizi wa TARURA
Wilaya ya Mbogwe.
Ukaguzi wa kifedha na kiufundi bila doa
Kiongozi
wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameongoza ukaguzi wa kina
kwa kutumia mitambo ya kisasa na kupitia nyaraka zote za utekelezaji. Baada ya
ukaguzi huo, alisifu ubora wa kazi na kueleza wazi kuwa mradi huo hauna doa.
“TARURA
mmeweka alama nyingine kubwa. Huu ni uthibitisho kwamba fedha za umma
zikitumika ipasavyo, wananchi wananufaika kwa vitendo,” amesema Ussi.
Wachimbaji
wafunguka hisia zao
Wakati
wa uwekaji wa jiwe la msingi, wachimbaji wadogo wa Nyakafuru walifurika
wakishangilia, wakisisitiza kuwa mradi huo umewafungulia ukurasa mpya wa
maisha.
Masumbuko Ibazu, mchimbaji mdogo, amesema kwa msisitizo:
“Barabara
hii ilikuwa kero kwa miaka mingi. Tulipata mateso kusafirisha mawe na tulilipa
gharama kubwa sana. Marais walipita wakiahidi, lakini hakuna aliyetekeleza. Leo
mama Samia ametutengenezea barabara ya ndoto. Wachimbaji wa Nyakafuru tunasema
wazi – wapinzani wasijaribu kusogelea huku. Hii ni barabara ya wananchi, ni
barabara ya maendeleo. Hatutaki maneno ya upinzani, tunataka vitendo kama
hivi.”
Naye Kahigi Jeremiah aliweka wazi hisia za wengi:
“Mama
ni mama tu, anajua uchungu wa watoto wake. Ametunyamazisha kwa vitendo, siyo
maneno. TARURA wamefanya kazi kubwa na wamewachongea wapinzani kwa wachimbaji.
Nyakafuru sasa ni ngome ya maendeleo – hakuna nafasi ya wapinzani.”
Fursa za kiuchumi na kijamii
Meneja wa TARURA Mbogwe, Mhandisi Patrick Chacha, alibainisha kuwa barabara ya Nyakafuru haitabaki kuwa alama ya usafiri pekee, bali ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Barabara
hii inarahisisha usafirishaji wa watu na mazao, inafungua uwekezaji mpya na
inachochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.
Taswira ya Geita yazidi kung’ara
Barabara
ya Nyakafuru imekuwa mradi wa nne mfululizo kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru ndani
ya siku nne bila kubainika kasoro, baada ya barabara ya Nzera, barabara ya
Kasco na daraja la Kharumwa–Nyijundu.
Mfululizo
huu wa mafanikio umeimarisha taswira ya Geita kitaifa, tofauti na miaka
iliyopita ambapo baadhi ya miradi ya Mwenge ilikataliwa kutokana na dosari. Safari
hii, miradi ya TARURA Geita imekuwa kioo cha mfano, ikionesha dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Wananchi
sasa wameshuhudia kodi zao zikigeuka barabara na madaraja yanayorahisisha
maisha yao ya kila siku, huku wachimbaji wa dhahabu wa Nyakafuru wakisisitiza
kuwa barabara hii ni ushindi wa vitendo, unaowafanya kutokubali tena maneno ya
wapinzani.
0 Comments